Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mazoezi ya Cheka Dar si mchezo, akimsubiri Mfilipino Dom

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku tisa kabla ya pambano la ubingwa wa UBO Internatoional la Cosmas Cheka na Alvin Lagumbay, kocha Daudi Muhunzi amemuongezea ‘dozi’ ya mazoezi Cheka ili kumjengea stamina.

Cheka amepiga kambi Kinondoni Msiriri jijini Dar es Salaam chini ya makocha watatu wakiongozwa na Muhunzi tayari kwa pambano hilo la Desemba 26 litakalopigwa Dodoma.

Kocha Muhunzi amelazimika kumfanyisha Cheka mazoezi ya kunyanyua taili la trekta kwa kutumia mikono au miguu, mazoezi ambayo anasema ni ya kumjenga stamina na nguvu za mikono bondia huyo.

“Anacheza na Mfilipino, asili ya mabondia wa nchi hiyo wana kasi sana, hivyo inabidi kufanya mazoezi ambayo yatampa nguvu na kasi ya mikono ili kuendana na mpinzani wake,” alisema Muhunzi.

Akizungumzia mazoezi hayo, Cheka alisema ni mazuri lakini hayazoweleki. “Kweli yananijenga na naona kuna utofauti katika uchezaji wangu, ila ndiyo hayazoweleki,” alisema Cheka ambaye pia anajifua kwa kupigana ana kwa ana na mabondia Hamis Maya, Francis Miyeyusho, Mwinyi Mzengela na Shomari Pendeza.

Mazoezi mengine ambayo bondia huyo amekuwa akifanya ni kukimbia umbali mrefu kwenye mchanga mwingi akiwa amembeba mtu mwingine, kupiga ‘pad’, kunyanyua vyuma na kuruka kamba.

Cheka atazichapa na Lagumbay, bondia namba nne nchini Ufilipino akiwa ameachwa kwa nafasi tatu na nguli wa dunia, Manny Pacquiao katika uzani wa welter pambano la raundi 10 litakalopigwa kwenye Ukumbi wa Chinangali.

Cheka atapanda ulingoni akibebwa na uzoefu, ingawa atakutana na rekodi za mpinzani wake anayetumia zaidi mkono wa kushoto (southpaw) kama ilivyo kwa Pacquiao. Sifa nyingine ya Lagumbay ni uwezo wa kulazimisha matokeo ya Knock Out (KO) ambapo katika mapambano 12 aliyoshinda, 10 ameshinda kwa KO. Kidunia, Lagumbay ni wa 317 kati mabondia 2,358 kwenye uzani wake na ameshusha uzito hadi wa super light ili kuzichapa na Cheka - bondia wa 336 kati ya 2,322 duniani na wanne kati ya 86 nchini.

Promota wa pambano hilo, Salum Viduka alisema litatanguliwa na mengine saba ambapo Nasser Mafuru, Undule Langson na Joseph Martin watazichapa kuwasindikiza.

Undule atazichapa na Alex Kachewele, Martin Joseph dhidi ya Philip Okololo na Nasser atazichapa na Ibrahim Makubi.

Wengine ni Kudra Tamim dhidi ya Yuko Mchawi, Jaylan Mohammed na Ally Gwede, Mussa Chitepe na Said Mondi ilhali Dorothea Muoza atazipiga na Agnes Kayage.