Lemar akumbuka shuka kumekucha

MADRID, HISPANIA. MAJUTO ni mjukuu wahenga walisema. Winga Mfaransa, Thomas Lemar amekiri kujutia uamuzi wa kupiga chini chaguo la kujiunga na Liverpool wakati wababe hao wa Anfield walipompa ofa hiyo miaka mitatu iliyopita.
Winga huyo wa zamani wa AS Monaco kwa sasa anakipiga Atletico Madrid, mahali ambako maisha yake yamekuwa magumu kutokana na kushindwa kumshawishi kocha Diego Simeone kumpanga kila wakati kwenye kikosi chake cha kwanza.
Kipindi hicho akiwa Monaco, Liverpool walipeleka ofa ya kuhitaji saini ya mshambuliaji huyo na wababe hao wa Ligue 1 walipandisha bei na kuwafanya mabosi wa Anfield kurudi nyuma na kuahirisha mpango.
Lakini, sasa Lemar anajuta na kufikiria kwamba ni heri angelazimisha uhamisho huo pengine mambo yangekuwa tofauti na ilivyo kwa sasa ambapo amekuwa akisugua tu benchi huko Wanda Metropolitano.
Akizungumza na Telefoot, Lemar alisema: “Majuto? Inawezekana. Siwezi kuficha hilo, nilikuwa na huzuni kiasi.
“Jambo likishapita limepita, hivyo najaribu kutofikiria snaa. Napiga kazi nikiwa na matumaini kuna klabu itakuja kwenye dirisha lijalo.
“Napokea kila ofa. Mimi ni mwanasoka, napenda mpira. Siwezi kufunga milango.”
Lemar anaripotiwa kwamba anaweza kutimkia kwenye Ligi Kuu England anakotakiwa na Arsenal.