Lamine baibai, Rasta Mkongo ndani

Thursday July 29 2021
lamine pic
By Charity James

YANGA kiroho safi imeachana na Lamine Moro na Mwanaspoti linajua kwa asilimia kubwa mbadala wake ni rasta wa DC Motema Pembe, Hennock Inonga Baka. Ingawa pia wanaendelea mazungumzo na Mkongo mwingine, Marcel Kalonda ambaye nafasi yake inaonekana kuanza kufifia kutokana na simu ya Kocha maarufu Florent Ibenge ambaye amewaambia Yanga wamchukua Hennock.

Yanga inaimarisha safu yao ya ulinzi, ambayo msimu ulioisha iliruhusu mabao 21 katika mechi 34. Ukuta wa Yanga msimu ulioisha uliundwa na Lamine Moro, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha na Adeyun Salehe.

Tayari jana Jumatano, Yanga iliachana na aliyekuwa nahodha wao, Moro, ili kuendelea kuboresha zaidi ukuta wao.

Yanga wamethibitisha kupitia taarifa yao kamili kuwa Yanga ni  wamefikia uamuzi wa kuachana na Moro ambaye ameitumikia Yanga kwa mwaka mmoja na nusu huku akiwa mkali wa mabao ya vichwa.

Hatua ya kusitisha mkataba huo Mwanaspoti linafahamu kwamba beki huyo aliitwa juzi katika kikao na mabosi wa Yanga na jana wakakubaliana kusitisha mkataba baina ya pande hizo mbili.

Hata hivyo, uamuzi huo wa Yanga hautokani na kiwango cha beki huyo, Mwanaspoti linafahamu hatua ya Moro kutofautiana na kocha wa timu hiyo, Nesreddine Nabi pamoja na kuyumba kwa nidhamu yake hivi karibuni.

Advertisement

Msimu huu uliomalizika Moro alianza vyema kuiongoza Yanga kushinda mechi nyingi, huku akifanikiwa kuifungia timu yake mabao manne akiwa ndiye beki mwenye mabao mengi.

Inaelezwa katika makubaliano hayo Yanga na Moro wamekubaliana watalipana mshahara wa mwezi mmoja.


Advertisement