Karia: Sina mahaba na Simba

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema hana mahaba na Simba kama ambavyo watu wanamhusisha na kwamba, hajawahi kuichukia Yanga, bali anaipenda Coastal Union ya Tanga ambako ndiko nyumbani kwao.

Karia aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Alisema yeye kama rais wa shirikisho hilo hana timu anayoipendelea kati ya hizo timu mbili, huku akiweka wazi ushabiki wake kuwa upo Coastal Union na anaishabiki tangu akiwa mdogo na ni mwanachama halali.

“Mimi kama ni mahaba ya timu yako Coastal Union na iko kubaya, inaishia shimoni, ila kusema nina mahaba na Simba inatoka wapi au naichukia Yanga kwa sababu gani.

“Mimi hata ugomvi na Yanga sina, ni maneno ya watu tu, lakini katika maisha ukiwa kiongozi hauwezi kumfurahisha kila mtu na sio kwamba utendaji wangu utamfurahisha kila mtu, kuna mwingine nitamkera kutokana na utashi wake,”alisema.

Alisema kwa nafasi aliyonayo na mapenzi yake Coastal Union, basi isingekuwa katika nafasi iliyopo hivi sasa ambapo inashika nafasi ya 16 ikiwa imecheza mechi 29 na kukusanya pointi 33.

“Mahaba yangu kwa Simba nimeyaonyesha vipi, kwa Yanga nawachukia vipi, mahaba yangu yako Coastal nayo inaenda kwenye shimo.

“Toka mdogo naiona Coastal Union, hawa wengine nimewakuta huko, kama kweli nina tabia hiyo nishindwe kufanya kwenye timu yangu ambayo ni mwanachama, ila siwezi kufanya hivyo.”

Aliwataka wadau wa soka kuacha kasumba za kuzusha vitu ambavyo sio vya kweli, kwani haviwezi kusaidia kuleta maendeleo yoyote.