Kambi ya Simba mambo ni moto, Zoran aachiwa panga

Zoran: Kwa mziki huu, mmeumia

KAMBI ya Simba inaendelea kunoga, huku kocha Zoran Maki akisaliwa na wiki kama moja tu kukamilisha programu zake kabla ya kuja kuwasha mitambo katika tamasha la Simba Day kisha kuliamsha dude mbele ya watani wao kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 13.

 Simba iliondoka nchini Julai 14 na kuanza mazoezi siku iliyofuata katika hoteli ya kishua ya Mercure Ismailia Forsan Island na hadi kufika leo imefikisha siku 13 za kutengeneza kikosi na imebakiza siku nane kati ya 21 zilizopangwa kwa ajili ya kambi hiyo iliyopo chini ya kocha Zoran.

Katika siku 13 za kujifua, Zoran amezitumia kujenga utimamu wa miili ya wachezaji, kuongeza pumzi na kutambulisha mbinu mbalimbali watakazozitumia kwa msimu ujao na kuwafanya wachezaji kucheza kwa kuelewana na kutengeneza mifumo zaidi ya miwili tofauti.

Ili kuhakikisha anajua maendeleo ya timu, Zoran alicheza mechi mbili za kirafiki, ya kwanza dhidi ya Ismaily na kutoka sare ya 1-1 kisha kuifumua Al Akhdood kwa mabao 6-0 na jana ilikuwa uwanjani tena kwa mchezo wa tatu dhidi ya Haras El Hadood.

Katika mechi mbili za awali, wachezaji Patrick Phiri, Augustine Okrah, Mohamed Ouattara, Pape Sakho, Meddie Kagere na Clatous Chama walitakata na kumfurahisha kocha, ambaye kwa sasa amekabidhiwa panga na kuwakata nyota wa kigeni waliozidi ili kubakiza 12 wanaotakiwa na kanuni.

“Nina furaha na tulichokifanya hadi sasa, maendeleo yanaonekana kwa mchezaji mmoja mmoja na timu nzima kwa ujumla, tumebakiza siku chache hapa ambazo tutazitumia kumalizia maandalizi ya msimu ujao na baada ya hapo naamini tutakuwa tayari kwa mapambano,” alisema Zoran.

Kocha huyo ana kibarua cha kufyeka majina mawili ya nyota wa kigeni, huku taarifa za awali zikisema kuwa, Chris Mugalu amekuwa wa kwanza kupitiwa na panga hilo, japo bado haijathibitishwa hadi sasa.

Mbali na Mugalu, nyota wa kigeni waliosajiliwa Simba na ambao wanatakiwa kupunguzwa kutoka 15 hadi 12 ni pamoja na Meddie Kagere, Taddeo Lwanga, Sadio Kanoute, Victor Akpan, Joash Onyango, Henock Inonga, Clatous Chama, Peter Banda, Pape Ousmane Sakho, Moses Phiri, Mohamed Ouattara, Augustine Okrah, Nelson Okwa anayetarajiwa kutua kambini muda wowote na Cesar Manzoki ambaye dili lake limekwama.

Pamoja na kutakiwa kufyeka mastaa wawili wa kigeni, Zoran pia atatumia siku nane hizo kupata kikosi cha kwanza na mfumo namba moja atakaokuwa anautumia kwenye mechi zake nyingi.

Kocha msaidizi wa kikosi hicho, Seleman Matola aliliambia Mwanaspoti kinachoendelea kambini ni zaidi ya burudani kwani kocha Zoran amewaambia wachezaji wote wapambane kwani hakuna mwenye uhakika wa namba ndani ya kikosi cha kwanza hivyo kila mtu afanye kazi kumshawishi.

Matola alisema kauli hiyo imeongeza morali ndani ya kikosi hicho na ongezeko la wachezaji wapya limeleta picha mpya na ushindani.