'Chama la Wana' muhimu pointi tatu

Muktasari:
- Kocha huyo wa zamani wa timu za Ndanda FC, Mbeya City na Tanzania Prisons, amezungumza hayo baada ya juzi kikosi hicho kushinda bao 1-0, dhidi ya Transit Camp, ikiwa ni ushindi wa pili mfululizo baada ya kuifunga pia Kiluvya United 1-0.
KOCHA mkuu wa Stand United 'Chama la 'Wana', Meja Mstaafu Abdul Mingange amesema, licha ya timu hiyo kupata ushindi mwembemba wa bao mojamoja katika michezo miwili iliyocheza hadi sasa, hawana hofu juu ya hilo kwani muhimu kwao ni kupata tu pointi tatu.
Kocha huyo wa zamani wa timu za Ndanda FC, Mbeya City na Tanzania Prisons, amezungumza hayo baada ya juzi kikosi hicho kushinda bao 1-0, dhidi ya Transit Camp, ikiwa ni ushindi wa pili mfululizo baada ya kuifunga pia Kiluvya United 1-0.
"Muhimu kwetu ni pointi tatu kwa sababu hata huo ushindi mwembamba tunaoupata sio rahisi, timu zote zimejipanga vizuri hivyo niwapongeze wachezaji kwa kujituma na kuhakikisha tunashinda, mwenendo huu ni mzuri na tunataka kuendelea hivyo."
Mingange aliongeza, kwa muda aliokaa na timu hiyo anaamini itakuwa na mtazamo tofauti chini yake kwa maana ya uchezaji, huku akiushukuru uongozi kwa kutambua uwezo wake na kumpa nafasi, hivyo atakipambania kikosi hicho kufanya vizuri zaidi.
Kocha huyo anakumbukwa zaidi msimu wa 2022-23 alipoipandisha Mashujaa Ligi Kuu Bara na sasa anakipambania kikosi hicho kurejea tena katika ligi hiyo ya juu, baada ya kushuka msimu wa 2018/2019, kilipomaliza kikiwa nafasi ya 19 kati ya timu 20 na pointi zake 44.