Bale asema Madrid wamemtoa kafara

Muktasari:
Bale bado hafahamu kuhusu hatima ya maisha yake huko kwenye kikosi cha Los Blancos na kusema kila kitu kinapaswa kuzungumzwa kwa umakini ili kufikia mwafaka.
MADRID, HISPANIA.SUPASTAA Gareth Bale amesema amekuwa akifanywa mbuzi wa kafara huko kwenye Klabu ya Real Madrid.
Staa huyo wa kimataifa wa Wales alikaribia kabisa kupigwa bei kwenda China miezi miwili iliyopita, lakini sasa ameamua kufunguka kuhusu maisha yake yalivyo Santiago Bernabeu, ambapo kila timu inapofanya vibaya, basi lawama zote zinaelekezwa kwake.
Bale alisema waulizwe Real Madrid kilichotokea kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini pia winga huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur alisema hana furaha licha ya kwamba Kocha Zinedine Zidane ameamua kumrudisha kikosini.
Bale bado hafahamu kuhusu hatima ya maisha yake huko kwenye kikosi cha Los Blancos na kusema kila kitu kinapaswa kuzungumzwa kwa umakini ili kufikia mwafaka.
"Nafahamu nimekuwa nikifanywa mbuzi wa kafara mara nyingi tu, nimekuwa nikichukulia hiyo kama changamoto, licha ya kwamba si wakati wote," alisema.
"Mwishoni mwa msimu uliopita mambo yalikuwa magumu sana, si kwa upande wetu tu kwa timu nzima. Kwa sasa naona hali imebadilika na kuwa tofauti. “Nimeshangaa kwa sababu nafahamu wengi walikuwa wanajua kipi kitakachokwenda kutokea. Kwenye soka kweli chochote kinawezekana, ni mchezo mmoja wa uchizi, kuna mambo yanatokea si wote waliokuwa na uhakika kwamba yatatokea. Mimi ni profesheno, huwa nakaa tu kimya."
Bale kwa sasa yupo kwenye kikosi chake cha Timu ya Taifa ya Wales na kubwa linalomshangaza ni kurudishwa tena kwenye kikosi cha Los Blancos na Kocha Zinedine Zidane, wakati alishasema kwamba hamtaki kwenye timu.