Babu Njenje afariki, kuzikwa leo Kisutu

Muktasari:
- Babu Njenje ni miongoni mwa wakongwe waliotamba katika muziki wa bendi na kuiweka The Kilimanjaro.
MWANAMUZIKI mkongwe wa bendi ya Kilimanjaro maarufu kama Wana Njenje, Mabrouk Hamis Omar almaarufu kama Babu Njenje amefariki dunia leo Jumapili, Mei 24, 2020 jijini Dar es salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu mmoja wa watu wa karibu na Babu Njenje, Babu Ally alisema mzee Njenje amefariki alfajiri ya leo.
"Mzee amefariki alfajiri ya leo na msiba wake upo Upanga hapa alipokuwa anaishi na taratibu zote za msiba zinafanyika hapa nyumbani kwake.
"Alikuwa anasumbuliwa na kiharusi kwa takribani miaka mitano, juzi juzi pia akapata kiharusi kingine, ndugu yangu niache kidogo nipo kwenye kikao," alisema.
Babu Njenje, ambaye ametamba akiwa na bendi ya Kilimanjaro, ameacha watoto wawili mpaka umauti unamfika.
Mkongwe huyu anakumbukwa kwa nyimbo zake kama Njenje, Kinyaunyau na nyingine nyingi zilizowahi kutamba miaka ya nyuma.
Njenje atazikwa katika makaburi ya kisutu leo saa kumi jioni (10:00).