Arsenal waandamani kwa tajiri wao awape pesa za kusajili

Muktasari:
- Arsenal walipeleka ofa ya Pauni 40 milioni huko Palace kumtaka Zaha, wakaambiwa pesa yao haitoshi na sasa wamekua kwenda kwa mmiliki wao Kroenke awapatie pesa
LONDON, ENGLAND. ARSENAL wamevumilia wamechoka na sasa wameamua kwenda kugonga hodi kwa mmiliki wao awape pesa za kufanya usajili katika dirisha hili.
Mabosi wa Arsenal wamepanga kuzungumza na bilionea mmiliki wa timu hiyo, Stan Kroenke wakimtaka awape pesa kuongezea kwenye bajeti yao ya usajili.
Kocha Unai Emery amepewa Pauni 40 milioni za kufanya usajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya baada ya kikosi hicho kushindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kocha huyo Mhispaniola anataka wachezaji wapya watatu kwenye kikosi chake akiwamo winga wa Crystal Palace, Wilfried Zaha, ambaye klabu yake inahitaji Pauni 80 milioni ili kumpiga bei.
Chaguo jingine la Emery ni beki wa kushoto Kieran Tierney, ambaye klabu yake ya Celtic inahitaji Pauni 25 milioni, huku mchezaji watatu anayesakwa na kocha huyo ni beki wa kati na hivi karibuni walidaiwa kupeleka ofa ya Pauni 50 milioni huko Leicester City wakimtaka Harry Maguire.
Kocha Emery anataka kuboresha kikosi chake ili kukifanya kuwa na nguvu ya kurudi kwenye Top Four ya Ligi Kuu England msimu ujao. Awali, Emery aliambiwa auze wachezaji ili apate pesa ya kusajili nyota wapya, lakini shida inakuja sehemu moja kwamba hakuna anayewataka wachezaji wake anaowauza akiwamo Mesut Ozil, ambaye mshahara wake anaolipwa Pauni 350,000 kwa wiki umekuwa tatizo kubwa.
Arsenal walipeleka ofa ya Pauni 40 milioni huko Palace kumtaka Zaha, wakaambiwa pesa yao haitoshi na sasa wamekua kwenda kwa mmiliki wao Kroenke awapatie pesa. Pesa ya kusajili huko Arsenal ni shida hata hizo Pauni 25 milioni wanazotaka kuwapa Celtic kumsajili Tierney, wameomba walipe kwa awamu tatu, mbili za Pauni 10 milioni ndani ya miaka miwili, kisha itamalizia Pauni 5 milioni.