Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ali Kiba

Muktasari:

  • Lakini, ishu ya kukata na shoka ni wageni waliohudhuria ambapo Gavana wa Jiji la Mombasa la Kenya anakotoka mkewe, Amina Khalef, Hassan Joho, alikuwepo ndani ya nyumba na kundi kubwa la marafiki zake aliokuja nao.

ILE sherehe ya harusi ya mkali wa Bongo Fleva, Ali Kiba, iliyofanyika jijini Dar es Salaam juzi Jumapili imekata kiu ya mashabiki wake wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa jumla.

Lakini, ishu ya kukata na shoka ni wageni waliohudhuria ambapo Gavana wa Jiji la Mombasa la Kenya anakotoka mkewe, Amina Khalef, Hassan Joho, alikuwepo ndani ya nyumba na kundi kubwa la marafiki zake aliokuja nao.

Harusi hiyo ya Kiba ambayo ilikuwa siri katika hatua zake za awali, ilianzia Mombasa ndoa ilipofungwa Aprili 19 ambapo ni wadau wachache kutoka Tanzania walihudhuria ikiwemo familia ya Kiba na msanii Ommy Dimpozi ambaye ni rafiki yake wa karibu. Ndoa ilifungwa asubuhi saa 12 katika msikiti wa Ummul Kulthum, mfungishaji akiwa Sheikh Mohamed Kagera.

Baadaye ilifuatiwa na sherehe kubwa iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Gavana Joho, ambaye ni rafiki wa karibu wa Kiba.

Ni kutokana na hali hiyo Kiba aliahidi kufanya sherehe tena Tanzania ili watu wengi wa kwao waweze kushiriki.

Waalikwa

Katika sherehe ya Dar es Salaam iliyofanyika Diamond Jubilee, Kiba alijikuta akiwakutanisha watu mbalimbali maarufu. Kwa upande wa wana siasa, alikuwepo mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Salma Kikwete, ambaye alitambulishwa kuwa ni mama mlezi na alisema kama sio kusafari hata mumewe, Jakaya Kikwete, angekuwepo.

Mbali ya Salma ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, walikuwepo pia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Ummy Mwalimu), Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira (Antony Mavunde), Waziri wa Maliasili na Utalii (Dk. Hamis Kigwangalla) na Mbunge wa Chalinze (Ridhiwani Kikwete).

Wengine waliohuduria ni Gavana Joho, ambaye ni rafiki wa karibu na Kiba na ambaye aliambatana na msafara wa watu zaidi ya saba na kuwa na meza yao.

Kwa upande wa wasanii walikuwepo wengi baadhi ni Mwana FA, Christian Bella, Vanessa Mdee, Mimi Mars, Eshi Buheti, Idrissa Sultan na Ommy Dimpoz, aliyekuwa pia mmoja wa wanakamati.

Wadau wa soka nao hawakukosekana ambapo Haji Manara, Msemaji wa Simba alinogesha sherehe hiyo ikizingatiwa aliingia ukumbini hapo akitoka uwanjani baada ya timu yake kuifunga Yanga bao 1-0.

Manara alikuwa kivutio tangu alipoingia na kuanza kusalimiana na watu kabla ya kuelekea katika meza aliyokuwa amepangiwa kukaa. Kwa wachezaji walikuwapo Emmanuel Okwi wa Simba na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga.

Katika serehe hiyo iliyoanza majira ya saa moja jioni na kuisha saa sita usiku, waalikwa pia walitoa nasaha kwa maharusi ambapo Salma Kikwete, aliwasihi maharusi na wasanii wengine kulinda ndoa zao na kuweka mambo ya umaarufu pembeni.

Dk. Kigwangalla yeye alitangaza kuwapa ofa Kiba na mkewe kutembelea kivutio chochote cha utalii watakachoona kinawafaa katika fungate yao na kuahidi gharama zote atalipa yeye.

Mavazi

Katika harusi hiyo, nguo maalumu kwa wanaume ilikuwa kanzu ya rangi nyeupe, maziwa au dhahabu wakati kwa wanawake ilikuwa ni vazi la staha la rangi hizo pia, hali iliyofanya waalikwa nao kupendeza mno.

Pia mavazi hayo yalifanya kuwepo kwa uvaaji wa staha na hata aliyekuja kavaa nguo ya ajabu alianza kujishtukia kwa kuwa kulikuwa pia na wanafunzi wa madrasa ya Karikaoo wakinogesha shughuli hiyo kwa kupiga madufu.

Pamoja na watu wengi kupendeza, baadhi ya watu waliokuwa kivutio ni pamoja na mtoto wa Kiba, Prince Sameer, aliyevaa nguo iliyofanana na ile ambayo baba yake aliivaa akiwa anafungishwa ndoa mjini Mombasa.

Mwingine aliyekuwa kivutio na vazi lake ni msanii Idrissa Sultan, kiasi ya kwa wasiomfahamu vizuri Kiba, wangeweza kudhani ndiye alikuwa bwana harusi.