#WC2018: Sura zilizoonekana Russia 2018 zanasakwa England

Muktasari:
- Kucheza kwa kiwango bora kwenye Kombe la Dunia kunamfanya mchezaji husika kuwindwa na timu mbalimbali na hilo halina tofauti na fainali za Kombe la Dunia 2018 zinazofanyika huko Russia.
ASIKWAMBIE mtu, wanasoka ni wajanja sana. Wengi wao wamekuwa wakitumia fainali za Kombe la Dunia kama sehemu ya kubamba dili za kuhamia kwenye timu nyingine.
Kucheza kwa kiwango bora kwenye Kombe la Dunia kunamfanya mchezaji husika kuwindwa na timu mbalimbali na hilo halina tofauti na fainali za Kombe la Dunia 2018 zinazofanyika huko Russia.
Hawa hapa mastaa 10 wanaotamba kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, ambao majina yao yanahusishwa na klabu za Ligi Kuu England.
Huenda wakanaswa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Mateo Kovacic - Man United
Kung’ara kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia akiwa na kikosi cha Croatia kumemfanya Kovacic kuwa kwenye rada za klabu za Ligi Kuu England, ambapo Manchester United imeonyesha dhamira ya dhati ya kuhitaji huduma yake. Kovacic ni mmoja kati ya wachezaji walioifanya Croatia kuwa na wakati mzuri kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia, ambapo usiku wa jana Jumapili ilitarajiwa kumenyana na Denmark.
William Carvalho - Everton
Kiungo mkabaji wa Ureno, William Carvalho angeweza kuichezea Angola kwenye soka la kimataifa kwa sababu alizaliwa Luanda kabla ya kuamua kuitumikia Ureno.
Staa huyo kwa muda mrefu alikuwa akiitumikia klabu ya Sporting CP ya Ureno kabla ya kuripotiwa kwamba mkataba wake umevunjwa hivi karibuni na kuwafanya Everton kupiga hesabu za kwenda kuinasa huduma yake baada ya kuvutiwa na kiwango chake cha kiuchezaji kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia za huko Russia.
Alisson Becker - Liverpool
Kipa wa Brazil, Alisson Becker ni mmoja kati ya mastaa waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia ambao majina yao yamehusishwa na vigogo wa Ligi Kuu England.
Liverpool na Chelsea kwa nyakati tofauti zimehusishwa na mpango wa kumsajili kipa huyo anayechezea Klabu ya AS Roma.
Hata hivyo, Liverpool ambao wameonekana kupania zaidi kuipata saini yake watakabiliwa na upinzani mkali katika kupata huduma yake kutokana na kuwapo na vigogo wengine wa Hispania wanaomtaka pia.
Alisson, ndiye kipa namba moja wa Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia.
Aleksandr Golovin - Chelsea
Mwanzoni kabisa, supastaa wa Russia, anayetamba kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 zinazofanyika kwenye ardhi ya nchi yao, jina lake lilihusishwa na Arsenal kabla ya bilionea mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich kuripotiwa kuingilia kati na kumtaka staa huyo atue kwenye kikosi chake huko Stamford Bridge.
Kuna uwezekano mkubwa staa huyo wa CSKA Moscow akaihama timu hiyo na kutua kwenye Ligi Kuu England baada ya fainali hizi za Kombe la Dunia kufika ukingoni ambapo timu yake ya Russia jana Jumapili ilitarajia kumenyana na Hispania kwenye hatua ya 16 bora.
Sergej Milinkovic-Savic - Man United
Kiungo wa Serbia kwa muda mrefu kabla hata ya fainali za Kombe la Dunia 2018 hazijaanza huko Russia, Sergej jina lake lilikuwa linahusishwa na Manchester United.
Staa huyo amekwenda kwenye fainali hizo akiwa na kikosi chake cha Serbia na kufanya mambo makubwa licha ya timu hiyo kukomea kwenye hatua ya makundi. Sergej bado jina lake linahusishwa na wababe hao wa Old Trafford licha ya kwamba imeshamnasa kiungo wa Kibrazili, Fred.
Hivi karibuni, Sergej alifichua kitu kuhusu hatima yake, akisema anaweza kubaki kwenye kikosi chake cha Lazio.
Nabil Fekir - Liverpool
Staa huyo wa Ufaransa, Nabil Fekir aliripotiwa kupima hadi afya kwa ajili ya kujiunga na Liverpool kabla ya dili hilo kukwama katika dakika za mwisho na bosi wa Lyon kufichua jambo jipya akisema Manchester United nayo imekuja kutaka kumnasa huduma ya kiungo huyo mshambuliaji.
Kwa timu za Ligi Kuu England, Liverpool na Man United ndizo zilizoonyesha nia ya kutaka huduma yake, licha ya kwamba Barcelona nayo ilitajwa kutaka saini yake aende akarithi mikoba ya Andres Iniesta kwenye kikosi hicho cha Nou Camp.
Dries Mertens - Chelsea
Mshambuliaji Dries Mertens ni staa wa Napoli anayefanya mambo makubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia akiwa na kikosi cha Ubelgiji.
Kikosi chake kimefanya vizuri na kutinga hatua ya 16 bora ya fainali hizo. Kwenye kikosi cha Ubelgiji, Mertens amekutana na mastaa kadhaa wa Chelsea, akiwamo Eden Hazard na hivyo kufichuka kwa ripoti za kwamba wawili hao wanaweza kwenda kucheza pamoja pia huko Stamford Bridge. Mertens anaripotiwa kwenda Chelsea hasa kwa kipindi hiki ambacho aliyekuwa Kocha wa Napoli, Maurizio Sarri akihusishwa na mpango wa kutua Stamford Bridge kwenda kuchukua mikoba ya Antonio Conte.
Lucas Torreira - Arsenal
Injini ya Uruguay hii kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Huduma yake matata kabisa kwenye sehemu ya kati ya uwanja iliifanya timu hiyo ya Uruguay kuvuna matokeo mazuri kabisa huko Russia na sasa imetinga hatua ya robo fainali tena kwa kuitupa nje Ureno ya Cristiano Ronaldo kwenye hatua ya 16 bora.
Torreira ameripotiwa kuwa kwenye rada za Kocha Unai Emery akitaka aende akaongeze nguvu kwenye sehemu ya kiungo ya timu yake kuifanya kuwa imara zaidi sambamba na Granit Xhaka, ambaye ametamba kwenye Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Uswisi.
Robert Lewandowski - Chelsea
Poland haikuwa na maajabu kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, ikikomea hatua ya makundi tu licha ya kikosi chake kuwa na straika matata kabisa, Robert Lewandowski.
Fainali za Kombe la Dunia za Russia zilitumika pia kumtazama Lewandowski kama atakuwa na faida kwa timu nyingine zinazomtaka baada ya hivi karibuni kufichua kuwa anatarajia kuachana na Bayern Munich kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Chelsea ilitajwa kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo, lakini saini yake inaweza kuiingiza kwenye vita na Manchester United baada ya kudaiwa nayo inamhitaji aende akashindanie nafasi na Romelu Lukaku huko Old Trafford.
Benjamin Pavard - Arsenal
Umeona lile bao lake kwenye mechi ya hatua ya 16 bora dhidi ya Argentina? Lilikuwa matata kwelikweli. Benjamin Pavard ameonyesha kiwango kizuri kabisa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia akiwa na kikosi cha Ufaransa ambacho kwa sasa kimetinga hatua ya robo fainali huko mchango wake kwenye timu ukiwa ni kitu muhimu kilichoifikisha hatua hiyo.
Pavard ni jina la staa mwingine aliyeonekana kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 jina lake kuhusishwa na klabu za Ligi Kuu England, huko kwenye kikosi cha Arsenal ambacho msimu ujao kitakuwa chini ya Kocha Unai Emery, aliyetua Emirates baada ya kuachana na Paris Saint-Germain ya Ufaransa.