#WC2018: Sura za Ballon d’Or

Muktasari:
- Xavi na Andres Iniesta mwaka 2010 na Franck Ribery miaka mitatu baadaye, ndiyo peke yao walijaribu kuwatikisa wakali hao kwenye tuzo hiyo, lakini bado walishindwa kuwang’oa kwenye utawala wao.
TANGU upite mwaka 2007, hakuna mchezaji yeyote ambaye haitwi Lionel Messi au Cristiano Ronaldo amewahi kubeba tuzo ya Ballon d’Or. Lakini, mwaka huu 2018 kumeanza kuonyesha taswira ya kwamba kutakuwa na jina jipya nje ya wakali hao wawili wanaotamba kwenye La Liga.
Xavi na Andres Iniesta mwaka 2010 na Franck Ribery miaka mitatu baadaye, ndiyo peke yao walijaribu kuwatikisa wakali hao kwenye tuzo hiyo, lakini bado walishindwa kuwang’oa kwenye utawala wao. Kuna wakati Neymar aliaminika kwamba angewapora ubabe wakali hao, lakini majeruhi yametibua, kabla ya kwenda kuonyesha kiwango cha hovyo kabisa huko kwenye Kombe la Dunia 2018 nchini Russia. Ronaldo na Messi walitupwa nje mapema sana kwenye michuano hiyo. Jambo hilo limewafanya wale wachezaji waliobaki kwenye Kombe la Dunia kuwa na nagasi ya kubeba Ballon d’Or. Kuna timu nne zilizobaki kwenye Kombe la Dunia 2018 kwa sasa ambazo ni Ufaransa, Croatia, Ubelgiji na England.
Ufaransa: Kwenye kikosi hicho kuna mastaa wawili, Kylian Mbappe na Antoine Griezmann wanaweza kutikisa na kuibuka vinara kwenye Ballon d’Or. Mbappe ameonekana kuwa kwenye kiwango kizuri sana katika fainali hizo, huku Griezmann akienda mdogomdogo kuthibitisha uwepo wake katika michuano hiyo. Kwa supastaa Paul Pogba kama atafanya maajabu zaidi kwenye nusu fainali na fainali basi anaweza kuwapindua Wafaransa wenzake hao, lakini kwa kutazama hali ilivyo kwa sasa ni Mbappe na Griezmann ndiyo wenye nafasi ya kuchuana kwenye Ballon d’Or.
Croatia: Kwenye kikosi cha Croatia, kuna staa matata kabisa ambaye hatajwi sana, Luka Modric, lakini moto wake ni hatari. Hakika kama staa huyo ataendelea na ubora wake huo, hakuna ubishi jina lake litakuwa kwenye ile orodha ya wanaokimbizia tuzo ya Ballon d’Or. Kiungo huyo wa Real Madrid ametoka kubeba Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo kama ataisaidia Croatia kunyakua ubingwa wa dunia, basi hakuna kitakachomzuia Modric asibebe Ballon d’Or.
Ubelgiji: Kikosi hicho cha kocha Roberto Martinez kinaundwa na mastaa wengi sana wa maana. Kuna vichwa vitatu kwenye chama hilo la Ubelgiji wanaweza kuingizwa kwenye mchakamchaka wa kuwania tuzo hiyo ya Ballon d’Or. Vichwa hivyo ni Kevin De Bruyne, Eden Hazard na Romelu Lukaku. KDB alibeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita akiwa na Manchester City, huku Lukaku alifunga mabao ya kutosha tu kwenye kikosi cha Manchester United ana amefunga mara nne kwenye Kombe la Dunia, huku Hazard akiwa kwenye ubora mkubwa sana kuisaidia Ubelgiji kufika ilipofika kwa sasa.
England: Kinara wa mabao kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 ni Harry Kane, ambaye yupo kwenye kikosi cha England. Hadi sasa staa huyo ameshatupia mara sita na kuifikisha England kwenye hatua ya nusu fainali. Kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, alishindwa kidogo tu kubeba Kiatu cha Dhahabu baada ya kufunga mabao zaidi ya 30 akiwa na kikosi chake cha Tottenham Hotspur. Kane ni jina unalotarajia kuliona kwenye orodha ya wanaowania Ballon d’Or kwa mwaka huu.