Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ZeKICK: Msimu wa kibabe sana

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara umefikia tamati baada ya kila timu kukamilisha mechi zake 15, huku msimamo ukiweka dalili za mbio za farasi wawili.

Yanga inayoongoza mbio za ubingwa ikiwa na pointi 39, imeizidi kwa pointi 15 timu inayoshika nafasi ya tatu ya Azam FC yenye pointi 24 na kuleta dalili za vita ya ubingwa kuwa ni ya timu mbili za juu kwani Simba. ukilinganisha na timu nyinginezo, ndiyo iliyo karibu zaidi na vinara, ikiwa na pointi 31, yaani pointi 8 nyuma ya Yanga.

Timu 16 zote zimemaliza mzunguko wa kwanza kwa kila mmoja kuvuna alichopanda na ni Yanga tu ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja kati ya 15 iliyocheza tofauti na timu nyingine.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya matukio ambayo yamejitokeza katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baada ya kumalizika kwa Yanga kuongoza ligi.


MABAO YALIYOFUNGWA

Mabao 228 yamefungwa katika nusu ya msimu kwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara huku Yanga akiwa ni kinara wa upachikaji wa mabao na Tanzania Prisons ikiwa ni timu iliyofunga mabao machache zaidi wakifunga 8 tu sawa na Mtibwa Sugar.

Yanga ambao ni vinara wa kuchana nyavu za wapinzani kufikia sasa msimu huu, wamefunga mabao 25 na ndio waliofungwa mabao machache zaidi (4) kwenye michezo 15 waliyocheza wakati Tanzania Prisons wamefunga mabao nane tu kati ya michezo 15 ya mzunguko wa kwanza waliyocheza na ndio timu inayoburuza mkia kwenye msimamo. Ruvu Shooting iliyo katika nafasi ya 13, ndiyo timu iliyofungwa mabao mengi zaidi (21).


BOCCO SIKU 203 BILA BAO

Nahodha wa Simba John Bocco ambaye ndiye mshindi wa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita akitupia kambani mara 16, msimu huu pamoja na kupata nafasi ya kucheza hajafanikiwa kufunga bao hata moja kwenye ligi.

Mara ya mwisho Bocco kuifungia timu yake kwenye ligi ilikuwa Julai 18 mwaka jana kwenye mechi dhidi ya Namungo.

Mbali na Bocco washambuliaji wengine ambao hawajazifungia timu zao ni Chris Mugalu ambaye alifunga mabao 15 msimu uliopita, Yusuf Mhilu wa Simba ambaye alifunga mabao tisa akiwa Kagera Sugar, David Molinga, Herritier Makambo na Prince Dube ambaye ametoka kuuguza majeraha na alikuwa kinara kwa timu yake msimu uliopita alipoifungia Azam FC mabao 14.


YANGA MBELE WEMBE NYUMA CHUMA

Yanga mbali ya kuwa vinara wa Ligi Kuu kwa kukusanya pointi nyingi zaidi (39), ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi (25) huku pia wakiwa vizuri kwenye kujilinda wakiwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi (4) baada ya mechi 15, na huku wakiwa hawajapoteza mechi hata moja.


MBEYA KWANZA HAIJASHINDA NYUMBANI

Ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu na haipo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo. imeshinda michezo miwili tu kati ya 15 iliyocheza na ushindi huo ialiupata ugenini.

Mbeya Kwanza ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 13 baada ya kushinda mechi mbili, sare saba na kupoteza michezo sita.


KADI NYEKUNDU 12, sita za simba

Kufikia sasa nusu ya msimu, kuna kadi nyekundu 12 zimetolewa, huku nusu ya hizo zikitolewa dhidi ya wapinzani wa Simba.

Wachezaji waliokula umeme kwenye mechi dhidi ya Simba ni Abdulaziz Makame wa Namungo, Anuary Jabir wa Dodoma Jiji, Jacob Benedicto wa Coastal Union, Juma Ramadhani wa Polisi Tanzania, Mpoki Mwakinyuke wa Mbeya City na Hamis Kiiza wa Kagera Sugar.

Kadi nyekundi mbili zimekwenda dhidi ya wapinzani wa Yanga, ambao ni Hamis Khalifa Nyenye wa Namungo na Santos Mazengo wa Ruvu Shooting.

Simba pia haijanusurika kwenye kula umeme kwani beki wake Henock Inonga alitolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union, huku wengine waliotolewa kwa kadi nyekundu ni Ismail Gambo wa KMC katika mchezo dhidi ya Coastal Union, Joseph Majagi wa Mbeya Kwanza dhidi ya Dodoma Jiji na Steven Duah wa Kagera Sugar kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.


LUSAJO AWAFUNIKA WAGENI

Pamoja na timu kubwa Simba, Yanga na Azam FC kufanya usajili wa maana kwa kujaza nyota wengi wa kigeni mastaa wao wa ushambuliaji hawajafua dafu mbele ya wazawa.

Mshambuliani wa Namungo, Reliants Lusajo amemaliza mzunguko huo wa kwanza akiwa kinara wa kufumania nyavu baada ya kutupia kambani mabao 10 kwenye michezo 15 ya timu yake. Mgeni anayemkaribia zaidi ni Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao saba akilingana na mzawa, George Mpole wa Geita Gold.


HAT-TRICK FINYU

Kufikia sasa nusu ya msimu, kwenye Ligi Kuu imeshuhudiwa hat-trick moja tu ya mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma aliyefunga mabao matatu peke yake wakati timu yake ilipoifunga Namungo 3-1 Novemba 27, 2021.


UKUTA CHUJIO

Mbali na Ruvu Shooting kuongoza kwa kufungwa mabao mengi, timu nyingi zimeruhusu mabao mengi zaidi (au idadi sawa na mechi 15) zilizocheza, ambazo Tanzania Prisons iliyoruhusu mabao 20, Dodoma Jiji ambayo imefungwa mabao 18, Mbeya Kwanza (17), KMC (16), Geita Gold (15), Coastal Union (15) na Mtibwa Sugar (15).


MATUKIO TATA:

PENALTI YA UTATA ILULU

Yanga ilikuwa ugenini kwenye Uwanja wa Ilulu wakialikwa na Namungo ambao ndio walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza kupitia kwa Obrey Chirwa katika dakika ya 52 akimchambua beki Dickson Job na kukwamisha mpira nyavuni akimuacha kipa wa Yanga, Djigui Diarra akiwa hana la kufanya.

Dakika ya 79 kiungo fundi wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliibua vita kwa wachezaji wa Namungo baada ya kujiangusha ndani ya box na mwamuzi kuashiria kupigwa kwa mkwaju wa penalti iliyotumbukizwa wavuni na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ akiwapa Wanajangwani pointi wasiyostahili katika sare ya bao 1-1.


BAO LA GEITA KUKATALIWA

Ilikuwa ni dakika ya 85 ya mchezo zikiwa zimebaki dakika tano mchezo kati ya Simba na Geita Gold umalizike kwenye Uwanja wa Mkapa Desemba Mosi, mchezaji George Mpole alifunga bao kwa kichwa ambalo lilikataliwa kiutata baada ya mwamuzi kuamua kwamba Shomary Kapombe alisukumwa.

Simba ilipata ushindi wa utata wa 2-1 katika mechi ambayo wengi waliamini ilipaswa kumalizika kwa sare.


PENATI YA UTATA KWA MKAPA

Mechi ya Simba na Polisi Tanzania ilichezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam Oktoba 27 nayo ilitawaliwa na kioja.

Dakika ya 86 ya mchezo Bernard Morrison alianguka eneo la hatari la Polisi Tanzania akiashiria kupigwa na beki wa timu hiyo aliyekuwa kwenye harakati za kuokoa mpira na ndipo mwamuzi kwenye mchezo huo kuamuru penalti ipigwe.

Penalti hiyo ilizua mzozo, lakini hatimaye ilipigwa na Rally Bwalya dakika ya tisini na kuisaidia timu yake kumaliza mchezo kwa ushindi wa bao 1-0 na kufanikiwa kuvuna pointi tatu nyumbani.


PENALTI YA UTATA MKWAKWANI

Bao mkwaju wa penalti lililofungwa dakika ya 90 baada ya mwamuzi Ahmed Arajiga kuamuru mkwaju wa penalti upigwe langoni mwa Mbeya City akiashiria mlinzi wa timu hiyo aliunawa mpira ndani ya boksi liliwapa kipigo cha kwanza cha msimu wanaMbeya waliolala 3-2.

Abdul Suleiman ‘Sopu’ alifunga mabao mawili, moja hilo la penalti na jingine likifungwa na Haji Ugando wakati mabao ya Mbeya City yalifungwa na Juma Liuzio na Richardson Ng’ondya kwa mkwaju wa penalti.


MCHEZO KUAHIRISHWA

Mechi ya Kagera Sugar dhidi ya Simba iliyopaswa kufanyika Desemba 18, 2021 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba iliahirishwa baada ya wachezaji wa Simba kuripotiwa kuugua mafua.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi ilithibitisha kuwa wachezaji 16 kati ya 22 wa timu hiyo waliosafiri kwenda Bukoba waligundulika wanaugua mafua makali na kifua, hali iliyochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa (Seasonal Infulenza).

Baadaye, Mtibwa Sugar pia walitoa taarifa kwamba nyota wao walikumbwa na tatizo kama lililowapata Simba wao, lakini waligomewa mchezo wao kuahirishwa na kuambiwa kuwa wapandishe wachezaji kutoka kikosi cha pili, Mtibwa B.

Hata hivyo, mechi ya Kagera ilipopangiwa tarehe mpya, Simba walilala 1-0 kwa bao la Hamis Kiiza, ambaye kisha alitolewa kwa kadi nyekundu kwa kupoteza muda.


MBEYA CITY YA MOTOO

Moja kati ya timu zilizowaacha vinywa wazi mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania msimu huu, ni Mbeya City ambao wametoka kucheza play off baada ya kufanya vibaya msimu ulioisha na kuzihenyesha timu kubwa.

Mbeya City ipo nafasi ya tano baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza ikikusanya pointi tano kati ya tisa ilizowania dhidi ya vigogo wa ligi Simba, Yanga na Azam baada ya sare mbili na ushindi dhidi ya Simba.

Mbeya City, ambao katika msimu wa kwanza 2013-14 walikamata nafasi ya tatu katika mzunguko wa kwanza wakiwa na pointi 27, baada ya hapo hawakuwa na matokeo mazuri hadi msimu huu ambao sasa wamemaliza kwa pointi 23 wakiwa nafasi ya tano kwenye msimamo.