ZEKICK: Kali za TFF 2021

Sunday December 05 2021
TFF PIC
By Imani Makongoro

SIKU 365 za mwaka 2021 zinaelekea ukingoni kabla ya kuanza mwaka mpya wa 2022.

Mwaka huu matukio mbalimbali yalitokea ndani ya Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF).

Yapo matukio au mambo mazuri yaliyoyafanyika. Lakini wahenga husema penye mazuri, mabaya pia hujitokeza. Mwaka huu TFF ilikuwa na matukio mengi ila haya ni sita yaliyokuwa gumzo nchini.


UCHAGUZI MKUU

Hili lilikuwa moja ya matukio yaliyokuwa gumzo nchini hasa kutokana na mchakato mzima ulivyoanza hadi uchaguzi wenyewe ulivyofanyika.

Advertisement

Vurugu mechi ilikuwa ni kwenye nafasi ya urais ambayo Wallace Karia alitetea kiti chake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 7 uliofanyika mjini Tanga.

Katika mchakato wa awali, wagombea tisa walijitosa kuchuana na Karia, lakini hadi siku ya uchaguzi Karia alikuwa mgombea pekee aliyeidhinishwa na mkutano mkuu kwa kuulizwa wanaoafiki waseme ndiyo na wasioafiki waseme siyo.

Licha ya Serikali kupitia Wizara ya Michezo kusisitiza uchaguzi huo utafanyika kwa kanuni na taratibu zilizowekwa, baadhi ya wadau walilalamikia kanuni za uchaguzi kabla ya Ally Salehe - mmoja wa wagombea aliyeenguliwa katika mchujo wa awali kufungua kesi Mahakama Kuu Dar es Salaam kupinga katiba ya TFF na kesi ndogo ya kupinga uchaguzi ambayo ilisikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki.

Hata hivyo, mahakama ilimtaka Salehe kufungua jalada upya katika kesi ya msingi ndani ya siku 14 huku ikiruhusu mchakato wa uchaguzi kuendelea.

Katika mchakato wa uchaguzi kipengele cha udhamini kiliwaengua kwenye mchujo wa awali Salehe, Ally Mayay na Oscar Oscar waliojitosa kuwania urais.

Abbas Tarimba, Deogratius Mutungi, Zahor Haji na Rahim Kangezi wao hawakurudisha fomu, hivyo wakajiondoa kwenye kinyang’anyiro wakati Evance Mgeusa na Hawa Mniga wakipenya kwenye mchujo wa awali sanjari na Karia.

Mniga na Mgeusa walienguliwa kwenye usaili kwa kukosa uzoefu na Karia kusalia mgombea pekee wa nafasi ya urais ambaye alipitishwa bila kupingwa kwenye uchaguzi mkuu.

Mchakato wa Karia kutetea kiti chake ulianza Juni 8 kwa aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Swedi Mkwabi, kumchukulia fomu na kusisitiza kwamba amemchululia Karia fomu hiyo akiwa kama mdau wa michezo na si vinginevyo.


MECHI TIMU YA TAIFA

Licha ya baadhi ya wadau kuyataja makombe waliyoshinda timu ya vijana na ile ya wanawake kuwa ni kawaida, lakini jitihada za nyota hao na ile ya TFF viliiwezesha Tanzania kutwaa vikombe hivyo vya mashindano ya Shirikisho la Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa vijana na Kusini mwa Afrika (Cosafa) kwa upande wa wanawake.

Ushindi huo uliwapa fursa vijana hao kwa nyakati tofauti kualikwa Ikulu na Rais Samia Suluhu Hassan mara mbili mwaka huu sambamba na kuwapa zawadi ya viwanja mjini Dodoma timu ya wanawake kama alivyowahi kufanya mtangulizi wake, Hayati John Magufuli kwa Taifa Stars wakati wa utawala wake.

Tukio lingine lililoipa shavu TFF ni lile la Taifa Stars kuongoza kundi J katika harakati za kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani.

Stars ilitakiwa kuifunga DR Congo nyumbani ili kujiimarisha zaidi kabla ya kucheza na Madagascar ugenini na kama ingeshinda mechi zote ingekuwa na nafasi ya kuingia 10 bora ili kutafuta timu tano ambazo zingeiwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia huko Qatar.

Licha ya hamasa kubwa ambayo wadau na Serikali waliionyesha kabla ya mechi hizo, bahati haikuwa upande wa Stars hivyo ikaondolewa kwenye harakati hizo.

Stars pia ilitolewa kwenye mashindano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) ambako ilimaliza mchezo wake wa kundi D Januari 27 kwa sare ya mabao 2-2 na Guinea na kufikisha pointi nne hivyo kushindwa kuzifikia Zambia na Guinea.

Kama ingeshinda ingefuzu robo fanali kwenye mashindano hayo yaliyofanyika Cameroon. Awali Stars ilichapwa na Zambia mabao 2-0 na kuifunga Namibia 1-0.


KUAHIRISHWA MECHI YA WATANI

Ilikuwa ni habari ya mjini ambayo kwa namna moja iliitia doa TFF hasa baada ya Yanga kuwa na hisia kwamba shirikisho hilo limekuwa likifanya uamuzi wa upendeleo kwa baadhi ya timu, ingawa Serikali iliingilia kati na kuitaka klabu hiyo na TFF kukaa chini na kumaliza tofauti zao.

Kabla ya agizo la waziri mkuu alilolitoa bungeni mjini Dodoma kwa kutaka wizara ya michezo, TFF na klabu hizo kukaa pamoja na kumaliza sintofahamu juu ya mechi hiyo, kueleza itachezwa lini na hatma ya viingilio vya mashabiki waliokuwa wamelipa, hali haikuwa shwari.

Mechi hiyo ya Mei 8 ilitangazwa kuahirishwa uwanjani tayari mashabiki wakiwa wameingia, ikiwa ni saa chache baada ya kutangazwa kusogezwa mbele.

Yanga waliugomea muda mpya na kuingiza timu uwanjani ambako walipasha na kisha kusubiri kwa muda wao kabla ya kuondoka na baadaye Simba waliwasili na wao kupasha kabla ya mechi hiyo kutangazwa kuahirishwa na kuibua sintofahamu Yanga wakisimamia kwenye hoja ya kanuni, ingawa baada ya siku kadhaa ilitangazwa tarehe mpya ya mchezo huo wa dabi.


USAWA ADHABU ZA TFF

Mei 30, baadhi ya wabunge walizungumza bungeni mjini Dodoma wakihoji usawa katika utoaji adhabu za TFF na kuitaka Serikali kulisafisha shirikisho kwa kile walichodai kuna upendeleo na unazi unaozorotesha soka nchini

Walisema hayo wakati wa kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Michezo kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba alisema viongozi wa klabu wamekuwa wakipewa adhabu za hovyo, huku kukiwa hakuna usawa katika utoaji adhabu

Aliitaka Serikali kusafisha mpira wa miguu ili kuleta matumaini yaliyotarajiwa kwenye soka akisisitiza mambo hayo yameathiri timu za taifa.

Suala hilo liliungwa mkono na Seif Gulamali ambaye alisema lazima kuwe na shirikisho ambalo halina unazi.

Naye Cosato Chumi, mbunge wa Mafinga Mjini alitaka TFF kuangalia kanuni zake ili kuwe na adhabu ambazo zinaweza kumjenga mtu ili kurekebika kuliko kumkandamiza zaidi.


MADENI

Moja ya vitu vilivyotia doa katika shirikisho hilo mwaka 2021 ni kutishiwa kushtakiwa kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa madeni.

Julai 20, mwanariadha mkongwe na mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Filbert Bayi alitishia kuishtaki TFF kwa kushindwa kumlipa kwa wakati Sh76.4 milioni ambazo analidai shirikisho hilo.

Bayi alisema taasisi yake inawadai TFF pesa hizo kwa miaka mitatu sasa ambazo zilikuwa ni gharama ya kambi kwa timu za vijana chini ya miaka 13, 15, 17 na ile ya wanawake ambazo zilikuwa na programu za mashindano ya kimataifa zilizoweka kambi katika taasisi hiyo iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Juni 3, 2019 taasisi hiyo iliingia makubalino na TFF ya miaka mitatu ya kutoa huduma za viwanja, usafiri, kambi na chakula wenye thamani ya Sh521.4 milioni ambazo walikubaliana zilipwe kwa awamu na kusalia Sh76.4 milioni ambazo Rais wa TFF, Karia alikiri hilo na kusema suala hilo lilikuwa linashughulikiwa na katibu mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidao.

Ingawa Bayi alidai muda wa makubaliano ya kulipa umepita kabla hata ya kifo cha mkewe Baya, Anna Bayi, Januari, mwaka huu, ambaye alikuwa akifuatilia deni hilo bila mafanikio na mabosi wa TFF kudaiwa kutopokea simu huku wakifuatiliwa ofisini walikuwa hafanikiwi kuonana nao na kutishia kushtaki Fifa ili apewe haki yake.


MIKATABA YA UDHAMINI

Licha ya changamoto za TFF mwaka huu unaoelekea ukingoni, Karia na timu yake wanaumaliza wakiwa wamefanikiwa kusaini mikataba mipya ya udhamini ambayo imeongeza hamasa, japo baadhi iliibua maswali kadhaa.

Novemba 23, TFF ilisaini mkataba wa miaka miwili na GSM wa Sh2.1 bilioni wa kuwa mdhamini mweza wa Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

NBC iliingia mkataba baina yake na TFF wenye thamani ya Sh2.5 bilioni, Oktoba 6 zikiwa zimepita siku 33 tangu TFF isaini mkataba na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wa haki za kurusha matangazo yanayobeba maudhui ya redio kwa mechi za Ligi Kuu Soka Tanzania Bara kuanzia msimu wa 2021/2022. Mkataba huo wa miaka 10 wenye thamani ya Sh3 bilioni ulisainiwa Agosti 3.

Kabla ya mikataba hiyo, habari ya mjini ilikuwa ni ule udhamini wa miaka 10 wa TFF na Azam Media uliosainiwa Mei 25 wenye thamani ya Sh265 bilioni.

Advertisement