Prime
Yanga ya Hersi inavyojitofautisha
Muktasari:
- Kuna mambo ambayo Yanga inaweza kujikita kuyazingatia, lakini timu zingine nazo zikapata fundisho kupitia kinachofanywa na rais wa Yanga, Hersi Said na safu ya uongozi ambao wamepindua mezani kibabe ndani na nje ya nchi.
CHAMA lako linayumba katika usajili? Kama jibu ni ndio na sababu zikawa sio kuhusu kipato ni namna ya kufanya mambo kwa hesabu basi soma hii.
Kuna mambo ambayo Yanga inaweza kujikita kuyazingatia, lakini timu zingine nazo zikapata fundisho kupitia kinachofanywa na rais wa Yanga, Hersi Said na safu ya uongozi ambao wamepindua mezani kibabe ndani na nje ya nchi.
Iko hivi. Hersi na wenzake wamefanikiwa katika kutafuta wachezaji bora wakifanya mambo kwa utulivu mkubwa hadi kufanikisha klabu hiyo kupata mastaa bora. Hebu angalia mastaa hawa.
Achana na kina Laurindo Dilson Maria Aurélio maarufu ‘Depu’ au Allan Okello walioingia katika dirisha dogo la usajili la msimu huu lililo wazi hadi Januari 30 sambamba na kina Hussein Masalanga, Mohammed Damaro na Emmanuel Mwanengo. Hapa chini ni mastaa ambao walitua Jangwani bila kutarajiwa chini ya mikakati ya Hersi na wasaidizi wake na kuifanya Yanga iwe tishio katika Ligi Kuu Bara ikibeba mataji mfululizo kwa misimu minne mfululizo.
BERNARD MORRISON
Hebu vuta picha namna rais huyo wa Yanga alivyomnasa Bernard Morrison kumsawishi na kuja nchini. Kipaji cha Morrison hakina shaka ilikuwa ni moja ya usajili bora Yanga, lakini hata alipohamia klabu zingine bado alithibitisha ubora wake.
STEPHANIE AZIZ KI
Mwingine ni Stephanie Aziz KI ambaye ukiacha Yanga, klabu nyingi nchini na nje zilikuwa zinahitaji huduma yake, lakini Yanga ndiyo ilimpata.
Nje ya Yanga mwandishi wa makala haya alikuwa wa kwanza kufanya mahojiano mara mbili na Aziz KI, na mara zote amekuwa akikumbuka namna bosi huyo wa Yanga alivyotumia ujanja kumfuata kwao, lakini pia nchini Morocco tena akienda huko wakati iliyokuwa klabu yake, ASEC Mimosas ikiwa inakwenda kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa ugenini dhidi ya RS Berkane. Ushawishi wa namna hiyo ukamkosha Aziz KI na kuamua kuzipiga chini ofa zingine na kukubali kutua Yanga.
CHADRACK BOKA
Beki wa Yanga ambaye alitua klabuni hapo akitokea FC Lupopo ya DR Congo ambapo awali wakati ubora wake unafuatiliwa, Hersi alitumia akili ileile akamfuata kwenye moja ya mechi kubwa nchini humo.
Kiongozi huyo wa Yanga aliushuhudia kwa macho ubora wa Boka, na baadaye kuamua kumaliza dili. Kipaji cha Mkongomani huyo hakina shaka akiendelea kufanya mambo ndani ya timu hiyo, kwani amewasahaulisha mashabiki wa Jangwani juu ya mtangulizi wake, Joyce Lomalisa aliyekuwa akifunika eneo hilo.
PACOME ZOUZOUA
Hesabu zilezile za Hersi zikaibeba tena hapa Yanga akamfuata kiungo huyo na kumshuhudia kwa macho akiwavuruga Waarabu na msimu ulipokwisha tu akamalizana naye fasta.
Hakuna shabiki aliyeamini kwamba Pacome angetua Jangwani, lakini mwamba amekuja kuwa pasua kichwa kwa wapinzani wa timu hiyo kutokana na ubora alionao, na kuifanya Yanga iendelee kuwakimbiza wapinzani wake katika Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (FA) na michuano ya kimataifa.
ALLAN OKELLO
Ni majuzi tu alimalizana na kiungo huyo wa Uganda aliyekuwa anawindwa na klabu nyingi zikiwemo zingine za hapa nchini.
Hersi alitua Uganda na kukutana na bosi wa Vipers, Lawrence Mulindwa kisha wakayajenga na juzi moto wa Okello ulionekana hadharani, akitoa risiti kwa kazi ambayo rais huyo wa Yanga alifanya kuinasa saini yake.
MAXI NZENGELI
Wakati Yanga inatafuta winga mzuri hesabu zilitua kwa Maxi Nzengeli miaka mitatu iliyopita na jamaa alifika DR Congo akiwafuatulia Union Maniema uwanjani.
Hersi kwenye mechi hiyo bila hata mchezaji kujua aliwaona wachezaji wawili bora Nzengeli na Agee Basiala. Hao wawili walikuwa kama pacha hatari kwa Wakongomani hao.
Hata hivyo, Hersi aliondoka na Nzengeli kwanza kisha akamuacha Basiala kwa makubaliano kwamba anataka kumsoma zaidi ambaye hata hivyo Lupopo ilishamchukua huku Nzengeli akiendelea kufanya balaa pale Yanga.
Wachezaji hao wanaonyesha kwamba klabu au hata viongozi wanatakiwa kutulia na kufanya mambo kwa hesabu kubwa ili kujiridhisha juu ya ubora wa wale wanaowataka.
Wachezaji wengi ambao wamefeli nchini ni wale ambao klabu zinaletewa au kuwaona kupitia vipande vya video. kuna msemo unasema hakuna mchezaji mbovu Youtube na sababu ni moja tu lile ni eneo la kuuza mchezaji ambapo vitaunganishwa vipande vya video kwenye maeneo aliyofanya vizuri na sio kuharibu.
GHARAMA ZIPO
Kupata kilicho bora kwa akili anayofanya Hersi sio kitu rahisi, kinahitaji gharama za fedha ambacho kinazishinda klabu nyingi, Hersi imekuwa rahisi kwake kutokana na imani na utayari wa mdhamini wa Yanga, GSM na ndio maana haishangazi kuona ikimleta Depu kutoka Ulaya sambamba na Okello na tayari wameshaanza kulipa kikosi kupitia mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa walioinyoa 6-0.
KAMATI NYINGI
Akili anayoitumia Hersi ni matokeo ya uamuzi wa kupunguza mlolongo wa usajili kufanywa na watu wengi. Mfumo huo bado upo kwenye baadhi ya klabu zetu ndogo na kubwa, ambapo unakuta usajili unafanywa na kundi la watu.
Lakini kwa Hersi hushauriana na wenzake kwa kila wanachopigia hesabu, ila mwishowe hufanya usajili inawezekana akawa yeye na kocha wake. Lakini huhakikisha mchezaji husika anafanya vizuri kwa kuwa ikitokea ameharibu lawama zinakuwa kwake na sio wengine. Inawezekana kukwepa presha hiyo ndio maana analazimika kuwa makini na kupata matokeo ya kupatia kuna nafasi kubwa kuliko kukosea, huku akiendelea kujifunza kwenye mazuri ili kuukuza mpira wa Tanzania.