Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga v Simba Muungano Cup, utamu wa game uko hapa!


NI Yanga dhidi ya Simba kwenye Fainali ya Kombe la Muungano itakayopigwa Aprili 29, hapa Uwanja wa Amaan Zanzibar na itakuwa mechi kubwa zaidi kwenye kilele cha mashindano hayo.


Timu zote mbili zimeonyesha ubora mkubwa kwenye mechi mbili za kila moja hadi zinafika fainali ambayo kuna vita sita za ubora kwa timu zote  zitakazokwenda kuamua nani ni mbabe wa mwingine.


Yanga sita, Simba nne

Yanga ndiyo timu iliyofunga mabao mengi hadi inatinga fainali na siyo zaidi ya Simba pekee bali kwa jumla Kombe la Muungano, ikifunga jumla ya mabao sita.

Mabao ya Yanga kwenye mechi zake hizo mbili za robo fainali na ile ya nusu fainali yalifungwa na mshambuliaji Prince Dube (matatu), akifuata viungo wake wawili Shekhan Ibrahim na Maxi Nzengeli wakati bao moja likipatikana kwa beki wa Muembe Makumbi City Suleiman Khamis  aliyejifunga wakati akipambana kuokoa kichwa cha shekhan.

Simba imefunga mabao manne ikiwa ni timu ya pili kupata mabao mengi nyuma ya Yanga na mabao yake yamefungwa na mshambuliaji suleiman Mwalimu aliyefunga mawili, wakifuata viungo Anicet Oura na Neo Maema ambao kila mmoja amefunga bao moja.

Simba ukuta mgumu, Yanga moja

Simba ndio timu iliyoonyesha ubora mkubwa kwenye ukuta wake ambao haujaruhusu bao lolote kwenye michezo hiyo miwili ya robo fainali na nusu fainali licha ya kutumia mabeki vijana kwenye mechi ya kwanza.

Yanga inafuaa nyuma ya wekundu hao, ikiruhusu bao moja pekee na aliyewatibulia ni kiungo wake wa zamani, Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC alipofunga bao la kufutia machozi kwenye mechi ya nusu fainali.


Yanga kipindi cha kwanza, Simba cha pili

Yanga ni hatari sana kipindi cha kwanza na imeonyesha inataka kumaliza mechi zake mapema. Katika mechi zake mbili imefunga jumla ya mabao matano yakipatikana ndani ya dakika 45 za kwanza.

Katika ubora huo, Yanga pia ndiyo timu iliyofunga bao la mapema zaidi likifungwa na Dube dakika ya tano kwenye mechi dhidi ya Azam na ni bao moja pekee limefungwa kipindi cha pili na mabingwa hao watetezi mfungaji akiwa Dube huyo huyo.

Simba yenyewe ina ubora wake na hadi inatinga fainali, haijafunga bao kipindi cha kwanza na yote manne yamepatikana kipindi cha pili.

Simba imekuwa ikicheza vizuri kipind cha kwanza lakini imekuwa ikikosa utulivu kwenye kumalizia nafasi na juzi dhidi ya Mlandege ilikaribia kufunga bao kipindi cha kwanza lakini shuti la Ellie Mpanzu liligonga mwamba.

Huku Dube, kule Mwalimu

Dube ndiye kinara wa ufungaji kwenye mashindano haya akiongoza kwa kuweka wavuni jumla ya mabao matatu akifunga katika mechi mbili tofauti, pia amekuwa na makali ya kumalizia nafasi tofauti na huko nyuma akijiweka kweye nafasi nzuri ya kuchukua tuzo ya mfungaji bora wa mashindano hayo.

Nyuma ya Dube yupo Mwalimu ambaye amefunga mabao mawili katika mechi mbili tofauti na utamu wa mabao yake ni yale ya kwanza katika ushindi wa timu hiyo.

Mwalimu amewabeba washambuliaji wazawa katika mbio hizo na usisahau mabao hayo mawili yote ameyafunga akitokea benchi na kubadilishia matokeo timu yake ukiwa ni mwendelezo wa ubora wake.

Vita ya Okello vs Chama

Kuna vita nyingine ya ubora na kule kwenye asisti kuna mbio ya viungo wawili, Allan Okello na Clatous Chama ambao wote wametengeneza asisti mbili kila mmoja.

Okello alikuwa mwiba sana kwenye mechi za Yanga na alitengeneza asisti mbili kwa mshambuliaji wake Dube, wawili hao wakitengeneza ushirikiano mzuri.

Kule Simba kuna Chama ambaye kabla ya timu yake kukutana na Mlandege hakuwa na asisti yoyote lakini kwenye nusu fainali akatengeneza mbili akiwapikia mabao Mwalimu na Oura katika mabao mawili ya kwanza ya ushindi wa mabao 3-0.

Barker vs Pedro

Kutakuwa na vita nyingine ya kiufundi kutoka kwa falsafa za makocha wote wawili.

Yanga ikiwa chini ya Pedro Goncalves imeonyesha kubadilika ikiwa na kasi kubwa ya kutibua mashambulizi, pia ikienda kufunga kwa mashambulizi ya haraka kasi ambayo huko nyuma haikuwa kubwa.

Simba ambayo ipo chini ya Kocha Steve Barker ina ubora kama huo ikiwa na kasi ya kwenda lango la mpinzani ikiwatumia viungo wake wa kati na wale wa pembeni kuharakisha mashambulizi hayo.

Twende tukaone itakuwa ni dabi ya ubora wa aina gani na timu ipi itaendeleza makali yake dhidi ya nyingine, majibu tutayapata leo, Aprili 29 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.