Mengo: Nidhamu ndiyo silaha yangu mpya
Muktasari:
- Mengo ambaye safari yake ya ngumi ilianza mwaka 2014 alipitia kipindi cha kupanda na kushuka na sasa amerudi akiwa na njaa ya mafanikio na ndoto ya kuandika historia nyingine.
KAMA ulikuwa unaamini safari ya bondia Hamza Mengo imefikia tamati basi jua kijana huyo anayetokea Vimo Gym amerejea upya baada ya kipindi kirefu cha kutoonekana ulingoni.
Mengo ambaye safari yake ya ngumi ilianza mwaka 2014 alipitia kipindi cha kupanda na kushuka na sasa amerudi akiwa na njaa ya mafanikio na ndoto ya kuandika historia nyingine.
Licha ya kuanza kucheza tangu mwaka 2014 lakini bondia huyo amecheza mapambano zaidi ya 10 huku matatu yakiwa kwenye rekodi ya Boxrec.
Kwa mujibu wa BoxRec, Mengo amecheza mapambano matatu ya kulipwa, akishinda moja na kupoteza mawili, huku vipigo vyake vyote vikitokana na maamuzi ya majaji, jambo linaloonyesha ushindani aliokutana nao ulingoni.
Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na bondia huyo safari yake ya ngumi na maisha mengine nje ye karia.
“Bado nina safari ndefu ya kupambana kwa sababu nimecheza mechi chache na kuna vitu napaswa kuboresha ili niandike rekodi nzuri kwenye mapambano yangu,” anasema Mengo.
HESHIMA KWANZA
Mengo anasema mafanikio ya bondia yanategemea nidhamu yake nje ya ulingo anaamini msingi wa mafanikio katika ndondi hauanzi ulingoni bali huanzia kwenye tabia ya bondia.
“Huwezi kufika mbali kama huna nidhamu. Lazima ufanye mazoezi kwa bidii, lakini zaidi ya yote umheshimu kocha wako na watu wanaokusimamia. Heshima ndiyo inayokufungulia milango mingi katika mchezo huu,” anasema bondia huyo
Anasema mabondia wengi wenye vipaji vikubwa hawafiki mbali si kwa sababu hawajui kupigana, bali kushindwa kuishi ndani ya misingi ya nidhamu.
Anasema kocha ndiye anayemjenga bondia, hivyo kumdharau au kupuuza maelekezo yake ni sawa na kuharibu safari yako mwenyewe.
“Ninaamini mtu asiye na heshima ni vigumu kufika mbali kwenye ndondi. Hata ukiwa na kipaji kikubwa kiasi gani, tabia ndiyo itaamua mwisho wako sasa huku mabondia wakishapata umaarufu wanawadharau wale waliowatoa.”
FAMILIA KIPAUMBELE
Anasema kwa sasa wazazi wameanza kuelewa michezo ni sehemu ya watoto wao kupata kipato tofauti na awali mambo yalikuwa tofauti.
Anatoa mfano wakati anaanza kupigana familia haikukubaliana naye lakini baadae wakaelewa jambo na anapewa sapoti kubwa.
“Unapokuwa na familia inayokuamini na kukusapoti unapata nguvu ya kupambana zaidi. Unajua kabisa kuna watu wanakuombea na wanategemea mafanikio yako, Huwezi kuuchukulia mchezo huu kama burudani tu, unapambana kuhakikisha familia yako inafurahia mafanikio yako.”
SAID BWANGA
Mengo anasema mmoja wa mabondia aliokuwa anawafuatilia na kumvutia hadi kuingia kwenye ndondi ni Said Bwanga.
Anasema alivutiwa na Bwanga kutokana na kutumia akili nyingi ulingoni na aina yake ya uchezaji ambayo ni mabondia wachache wanatumia.
“Nilikuwa navutiwa na uchezaji wake. Alikuwa amekamilika kuanzia miguu, mikono, mbinu na uvumilivu. Nilijifunza mambo mengi kwa kumuangalia,” anasema.
MANZESE, MABIBO
Anataja sababu ya kwa nini kuna wingi wa mabondia wanatokea Mabibo na Manzese akiamini vijana wengi hawana ajira hivyo ndondi ni kama sehemu yao ya kujikomboa kutoka kwenye mazingira magumu.
“Siku zote ngumi zinabebwa na watu waliopo katika mazingira magumu. Wengi wanaingia kwenye mchezo huu wakiamini ndiyo njia ya kuondoa umaskini.”
Anasema tofauti kubwa ipo kati ya mtu anayesema anac heza ngumi na yule anayesema ndondi ndiyo kazi yake.
Anaamini bondia anayechukulia ndondi kama ajira huwa tayari kujitoa kwa asilimia mia moja, kufuata ratiba zote za mazoezi na kupambana bila kuchoka kwa sababu anaamini humo ndimo maisha yake yalipo.
“Hiyo ndiyo sababu mabondia wengi wanaofanikiwa wanakuwa wamepitia maisha magumu.”
NJE NA NGUMI
Mengo anasema nje ya ngumi ni mfanyakazi aliyeajiri kwenye moja ya kampuni ingawa hakutaka kuweka wazi ni kampuni inayojishughulisha na nini.
“Huwa nafanya mazoezi mara mbili kwa siku hasa wakati nikikaribia kupanda ulingoni kwa hiyo najua kubalansi kazini na ulingoni.”
KIPIGO HIKI HATAKISAHAU
Bondia huyo anasema pambano ambalo hatasihau kwenye maisha yake ni mwaka 2018 alipokutana na bondia kutoka Makoko kwenye mapambano yake ya mwanzo.
Wakati huo hana uzoefu mkubwa aliingia ulingoni akiwa na ujasiri mkubwa wa kushinda pambano lile lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia. Mengo anasema mpinzani wake alimshambulia kwa kasi, akamwangusha chini na kumlazimisha mwamuzi kuhesabu.
“Nilianguka nikajiuliza, ‘imekuwaje?’ Nilikuwa bado sijaufahamu vizuri mchezo.” anaeleza
Kocha wake alipoona hali imekuwa mbaya akaamua kutupa taulo kuokoa afya yake lakini hadi leo pambano hilo halijafutika akilini mwake. “Ni pambano ambalo ningependa nilirudie. Limebaki kama kisasi ndani yangu.”
MALENGO YAKE
Anasema ndani ya miaka mitano ijayo anataka kupigana mapambano yatakayomtambulisha uwezo wake Afrika kwani hadi sasa hana pambano hata moja la kimataifa. “Kiukweli siwezi kusema kama nataka ubingwa wa WBO wakati sijapata ushindani na mabondia wa Afrika kwa hiyo kama nitapata mapambano naamini ndani ya miaka mitano nitakuwa bora.”
CHANGAMOTO
Anasema licha ya tasnia ya ngumi kukua nchini lakini bado kuna upungufu wa mapromota wa kutafutia mabondia mechi za kimataifa. “Hakuna bondia ambaye hataki kucheza nje muhimu apate maslahi yale anayoyataka lakini pia anapata uzoefu sasa sijajua mapromota hawapati mechi lakini kuna upungufu.”
Pamoja na hayo, kwa upande wake bondia anayemfuatilia zaidi duniani ni Ben White raia wa Uingereza, ambaye Mengo anamwona kama mwalimu wake.
“Huyo ndiye ambaye namba moja duniani na ninamkubali ni mtu ambaye ukimwangalia anavyocheza ni mtu hatari sana.”
Mengo anavutiwa na akili ya Ben White ulingoni.
“Kitu cha kwanza kinachomtofaiutisha na mabondia wengine, anatumia akili na anajua kucheza na akili ya mpinzani wake vilevile ni mwepesi.”