Yanga iliyoacha rekodi Kampala wakati Onyango akizaliwa Kenya

KAMA utani imetimia miaka 27 tangu vinara wa Ligi Kuu Bara kwa sasa, Yanga ilipoandika rekodi ya aina yake jijini Kampala.

Kwa waliosahau ni kwamba Januari, 1993 mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania, iliyosafiri kichovu kwenda Kampala, ilirejea nchini Kifalme baadaya kutwaa ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame).

Yanga ilitwaa ubingwa huo Januari 30, mwaka huo kwa kuinyoa SC Villa kwa mabao 2-1 katika mechi ya fainali ya kusisimua na kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kutwaa ubingwa huo nje ya ardhi ya Tanzania. Yanga ilirejea tena tukio kama hilo mwaka 1999 walipotwaa ubingwa wa michuano hiyo hapo hapo Kampala kwa kuifunga pia ScVilla.

Yaani wakati Yanga ikitwaa ubingwa huo wa pili kwao kwenye michuano hiyo, ndio kipindi ambacho eti beki wa Simba wa sasa kutoka Kenya, Joash Onyango alikuwa akizaliwa. Unabisha nini wakati tarehe za kuzaliwa kwa Onyango zinaonyesha ilikuwa saa 24 tu tangu Yanga ilipobeba ubingwa huo, kwani Onyango amezaliwa Januari 31, 1993.

Utamu wa taji lao la mwaka 1993, ni kwamba walitwaa kwa kuwapokea watani wao, Simba ambao walikuwa watetezi na walioenda kifalme katika michuano hiyo na kurejea kichovu wakitumia usafiri walioutumia vijana wa Jangwani waliosaidiwa na Reginald Mengi.

Ndio, Mengi ambaye kwa sasa ni marehemu akiwa mwenyekiti mtendaji wa Kampuni za IPP, alijitolea kuisafirisha Yanga kwenda Kampala baada ya waliokuwa wafadhili wa klabu hiyo enzi hizo wakiongozwa na Abbas Gulamali, Mohammed Viran, Ramesh Patwa, Murtazar Dewji na Muhsin Hassanali ‘kuisusa’ timu.

Wafadhili hao walikuwa wakipinga mipango ya Yanga kutaka kugeuzwa kuwa Kampuni na kuibua mgogoro mkubwa uliosababisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Augustine Lyatonga Mrema kuingilia kati kuiokoa klabu hiyo.

Achana na ishu hizo za kina Gulamali na wenzake na vita yao na uongozi wa kina George ‘Castro’ Mpondela’, ni kwamba katika michuano hiyo, Yanga ilifanya maajabu, huku nyota wake Edibily Lunyamila, Said Mwamba ‘Kizota’, Zamoyoni Mogella ‘Morgan’ a.k.a DHL ama Golden Boy na Hamis Gaga ‘Gagarino’ waliitikisa Kampala.

Yanga ilianza kwa kufumuliwa 3-1 na Villa kabla ya kuzinduka kwa Malindi kwa kuilaza 2-1 na kutinga nusu fainali waliyoinyoa Express kwa mabao 3-1 na kwenda zao fainali kukutana tena na Villa, huku wenzao Simba wakilitema taji hatua ya makundi.

Katika mechi ya fainali dhidi ya Villa, Yanga ilitanguliwa kufungwa bao dakika ya pili tu na George Akena kabla ya Kizota kusawazisha dakika nne baadaye na bao la ushindi likiwekwa kimiani na Lunyamila dakika ya 44, huku akimstaafisha soka aliyekuwa nahodha na beki nyota wa Villa na timu ya taifa ya Uganda The Cranes, Paul Hasule.

Mwanaspoti linakuletea jeshi zima lililocheza mchezo huo wa fainali na mahali walipo kwa sasa wachezaji walioweka heshima hiyo miaka 27 iliyopita, licha ya baadhi yao wakiwa wameshatangulia mbele ya haki.


1. Steven Nemes

Huyu ndiye aliyekuwa kipa namba moja wa kikosi hicho na alionyesha kliwango cha hali ya juu kabla ya wachezaji wa SC Villa kumuumiza na kumfanya atolewe katika kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Riffat Said aliyewashtukiza Waganda kwa mpira wake wa kwanza kuudaka kwa mkono mmoja.

Nemes aliyewahi kutamba pia na timu mbalimbali ikiwamo Majimaji, Simba na Taifa Stars kwa bado yupo hai na kwa sasa anashughulika na biashara binafsi.


2. Mwanamtwa Kihwelo ‘Diblo’

Beki huyu wa kulia aliyekuwa akimudu pia kucheza nafasi nyingine kwa ufasaha, ndiye aliyekamata shavu la kulia akiwaweka benchi kina Seleman Mkati na mkongwe David Mwakalebela.

Kwa sasa Mtwa anajishughulisha na ukocha na pia akifanya biashara ya vifaa vya michezo.


3. Kenneth Mkapa

Beki wa kushoto aliyekuwa hana utani na mtu iwe mazoezi ama uwanjani kwenye mechi ndiye aliyesaidiana na Mtwa kwenye upande wa ulinzi wa pembeni na SC Villa huenda bado hawajamsahau kwa namna alivyokuwa akikaba hadi kivuli.

Mkapa aliyewahi pia kutamba na Taifa Stars na kukaribia kutua Simba, kwa sasa ni kocha akifundisha timu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).


4. Willy Mtendamema

Beki wa kati aliyekuwa ‘bishoo’ kinoma akitambulika zaidi kwa panki lake na umaridadi wake uwanjani, ndiye aliyesimama kati akishirikiana na Issa Athuman.

Beki huyo alishirikiana na kikosi kizima cha Yanga kuwazima nyota wa wakati huo nchini Uganda ndani ya timu za Express na SC Villa kama kina Richard Kirumila, Issa Sekatawa, George Ssemogerere, Issa Sewanyana, William Nkemba, Suleiman ‘Sula’ , Katto, Godfrey Higenyi na Idd Batambuze.

Beki huyo wa zamani wa AICC, yupo Dar akifanya shughuli zake binafsi.


5. Issa Athuman

Licha ya kuwa ni kiungo mkabaji, lakini kwenye mchezo huo, kocha Nzoisaba Tauzany alimchezesha kama kitasa katika pambano hilo, huku kina Jumanne Shengo, Willy Martin ‘Gari Kubwa’ wakisubiri na Mgosi huyo ambaye kwa sasa ni marehemu hakufanya makosa, kwani alisimama vyema na kuilinda ngome ya Yanga.


6. Method Mogella ‘Fundi’

Utasema nini juu ya fundi huyo wa mpira aliyesajiliwa Yanga kutoka Simba aliyokuwa ametwaa nao ubingwa wa Kombe hilo la Kagame mara mbili mfululizo, 1991 na 1992. Jamaa aliupiga mwingi kama kawaida na kuchangia ushindi huo wa mabao 2-1.

Method alikumbwa na mauti miezi michache baada ya ubingwa huo wa Kagame na pia ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa Yanga. Alifariki Novemba 12, 1994.


7. Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’

Moja ya washambuliaji wakali waliowahi kutokea nchini, Mogella aliyefahamika pia kama Morgan na kubatizwa jina la DHL ndani ya kikosi cha Yanga kwa umahiri wake wa kugawa pasi murua kwa wenzake uwanjani, alipewa winga ya kulia.

Akiwa ndio kwanza amesajiliwa kutoka Simba, Mogella aliwasha moto kwelikweli Kampala akisababisha Abubakar Salum ‘Sure Boy’ asubiri nje.

Kwa sasa mkongwe huyo wa zamani wa Tumbaku, Simba, Volcano, anajishughulisha na biashara akiwa anaishi jijini Dar es Salaam.


8. Steven Mussa

Kiungo matata aliyekuwa ananyumbulika na fundi wa kugawa vyuma kwa wenzake, akishirikiana na Method waliwazima kabisa Waganda nyumbani na kuwa gumzo kubwa kwa kikosi kizima cha Yanga ambao walionyesha shoo ya kibabe Kampala.

Kiungo aliyewahi kuwahi pia na Tukuyu Stars na aliyekuwa akipokezana namba kikosini ndani ya Yanga na Hamis Gaga ‘Gagarino’ na Method kwa sasa ni marehemu.


9. Saidi Mwamba ‘Kizota’

Utasema nini juu ya mshambuliaji huyo aliyekuwa kugeuka kiungo na beki wa kati matata? Jiji la Kampala lilimtambua kwa shoo yake ya kibabe kwenye fainali hizo za Kagame, kwani licha ya kufunga bao la kusawazisha, lakini ndiye aliyeibuka Mfungaji Bora wa michuano kwa kufunga mabao sita, akimzidi Mathias Kaweesa wa SC Villa aliyefunga matano. Pia Kizota alitangazwa kama Namba 9 Bora wa michuano hiyo ya Kampala.

Kwa sasa Kizota ni marehemu kwani alikumbwa na mauti Februari 11, 2007 akitoka kuhushudia timu yake ya zamani, Simba ikingolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na Textil du Pungue ya Msumbiji kwa kugongwa na gari.


10. Mohamedi Hussein ‘Mmachinga’

Chinga One alikuwa noma. Uganda itabaki kumkumbuka kwani naye aliwatikisa kwa mabao yake kabla ya timu kufika fainali.

Katika mchezo huo wa fainali alicheza kama mshambuliaji namba mbili nafasi aliyoimudu zaidi na iliyomfanya aweke heshima kubwa katika soka la Tanzania kwa kuwa mfungaji bora wa muda wote mpaka sasa licha ya kustaafu soka.

Mabao yake 26 mwaka 1999 hayajawahi kufikiwa na yeyoye mpaka sasa katika Ligi Kuu na kwa sasa mshambuliaji huyo wa zamani wa Bandari Mtwara, Simba na Taifa Stars ni Kocha wa timu ya wanawake ya Yanga Princess.


11. Edibily Lunyamila

Akiwa amesajiliwa kutoka Biashara Shinyanga, Edibily Lunyamila alithibitisha kwamba yeye alikuwa ni zaidi ya mashine uwanjani. Winga huyo teleza aliwatesa na kuwagawisha Waganda kwa soka lake la kasi na chenga za kuudhi.

Ndiye aliyefunga la ushindi la fainali lililoipa Yanga taji lao la kwanza nje ya Tanzania na lililokuwa la pili kwao katika michuano hiyo, lakini kubwa zaidi ni kitendo cha kumstaafisha soka beki wa kulia wa SC Villa na Uganga The Cranes, Paul Hasule ambaye aliamua kutoka uwanjani kwa kuvua jezi kwa kukiri kushindwa kumdhibiti winga huyo, japo kocha wake walimrejesha uwanjani kumaliza mchezo na kutangaza kustaafu baada ya fainali hiyo ya aibu kwake. Unaambiwa shoo aliyopiga Lunyamila Kampala ilifanya wakazi wa mjini humo kuandika jina lake katika teksi, daladala na kibanda vyao vya biashara zikiwamo saluni.

Kwa sasa jamaa aliyewahi pia kukipiga Malindi na Simba na kuwahi kujaribiwa FC Cologne ya Ujerumani anajishughulisha na mambo yake binafsi jijini Dar es Salaam.

Akiba

- Rifat Said, aliyempokea Nemes baada ya kuumia, kwa sasa ni marehemu kwani alikubwa na mauti Mei 9, 2000.

- Hamisi Thobias ‘ Gagarino’: Kiungo huyo fundi aliyesajiliwa toka Simba alimpokea Steven Mussa kwenye mchezo huo wa fainali. Kwa sasa ni marehemu - alifariki dunia mwaka 1996.

- Aboubakari Salum ‘Sure Boy’: Winga huyo aliyesajiliwa Yanga kutokea Sigara kwa sasa anajishughulisha na mambo yake binafsi na kuna wakati alikuwa kocha wa Yanga B.

- David Mwakalebela: Beki huyo wa kulia aliwahi kutamba na Pamba na Taifa Stars bado yupo hai akijishughulisha na udereva katika kampuni ya Tasia.

- Willy Martin ‘Gari Kubwa’: Beki na nahodha wa zamani wa Simba, Yanga na Majimaji pamoja na Taifa Stars kwa sasa ni kocha anaishi Kyela, jijini Mbeya.

Kocha: Nzoisaba Tauzany, kocha huyo Mrundi aliyewahi kuzinoa pia Simba na Majimaji kwa sasa ni marehemu.