Yanga! Huo ndio mkuki kwa nguruwe
Muktasari:
Hiyo ni baadhi ya misemo ya Waswahili na wahenga ikijaribu kuonya watu kuhusu matendo yao ya kila siku hasa unapomfanyia mwanadamu mwenzio kwani ipo siku nawe yatakukuta. Kwani malipo ni hapa hapa duniani.
AMA kweli! Mtenda akitendewa hujihisi kaonewa. Pia siku zote mkuki kwa nguruwe mtamu kwa binadamu mchungu.
Hiyo ni baadhi ya misemo ya Waswahili na wahenga ikijaribu kuonya watu kuhusu matendo yao ya kila siku hasa unapomfanyia mwanadamu mwenzio kwani ipo siku nawe yatakukuta. Kwani malipo ni hapa hapa duniani.
Nimeanza hivi kwa kuangalia jinsi Wanayanga walivyochanyikiwa na kuumia baada ya kusikia wachezaji wao nyota Didier Kavumbagu na mdogo wangu Frank Domayo wamesajiliwa na Azam wiki hii.
Siyo habari njema hata kidogo kwa Yanga kuona nyota wao kama Kavumbagu na hasa Domayo wakiondoka bure na kujiunga na wapinzani wao Azam.
Kama ilivyokuwa kawaida ya binadamu ni wepesi kusahau hasa unapofanya kitu kwa mwenzako, miaka miwili iliyopita Yanga walimsajili Kelvin Yondani kutoka Simba, pia wakawanyang’anya Mbuyu Twite kabla ya kumpora Mrisho Ngasa kutoka kwa Azam.
Simba walihuzunika sana kwa kitendo hicho na kuwafanya baadhi ya mashabiki na wanachama kuwatishia maisha viongozi wao hadi rafiki yangu Kaburu kuamua kuchukua hatua ya kujiuzulu naye mwenyekiti Ismail Rage kama si jeuri yake naye alikuwa amekwenda na maji.
Hiyo haitoshi mwaka jana Yanga wametumia ujanja wa mjini wakamchukua Emmanuel Okwi wao na mashabiki wao walikuwa wakijiona ni wababe hakuna wa kuwagusa.
Sasa ni zamu yao amekuja mfalme mpya mwenye nguvu ya fedha tena si kubahatisha iliyokuwa imekamilika kila idara.
Naamini kama Bakressa akitaka kununua jengo la Yanga anaweza, siyo kuchukua wachezaji tu ambao kwa uzembe wa uongozi wa Yanga umewafanya kuondoka bure.
Viongozi wa soka hapa nchini hasa Simba na Yanga wamekuwa hawajali kuhusu mikataba ya wachezaji wao kwa sababu wanajua wachezaji ndio wenye shida ya kucheza katika klabu hizo, lakini siyo kinyume chake.
Maisha yamebadilika vijana wa sasa hatufanyi kazi sehemu kwa mapenzi ili unapata nini hapo ulipo leo na kesho yako itakuwaje.
Ndio maana umeona wachezaji wa Simba wanaenda Yanga na Yanga wanaenda Simba bila ya kujiuliza hasa wanapotangaza dau.
Mapenzi ya mahaba niue hakuna siku hizi, nipe pesa nifanye kazi kwako, kitu pekee kitakachomfanya mchezaji acheze kwa muda mrefu katika klabu yako ni kumwongezea masilahi na kumfunga kwa mkataba tu.
Hivi unadhani Steven Gerrard (Liverpool), Messi (Barca) Ronaldo (Real Madrid) ua Terry (Chelsea) wanapenda kuchezea timu hizo ni pesa tu imewaweka hapo ndio maana kila kukicha wanasaini mkataba juu ya mkataba.
Viongozi wa Yanga kwa kuzunguka kuwapa wachezaji wao mikataba kwa madai ya kusubiri uchaguzi walichokifanya ni sawa na kuhujumu timu yao.
Pia sijaona sababu ya TFF kujiingiza katika suala la Domayo na kutuma mtu wa kuchunguza kwa sababu Yondani alipojiunga na Yanga kwa mtindo huu wenyewe waliunda tume haikutoa majibu.
Nadhani wanachoweza kufanya kwa hili ni kumtoza faini Domayo kwa kukiuka kanuni za kambi au kumfukuza kwenye kambi ya Stars, lakini siyo kwenda Azam.
Kwa sababu mkataba wake na Yanga umebakiza mwezi mmoja hivyo yuko huru kusajili katika klabu nyingine yoyote apendayo bila ya utatizo.
Mwacheni Domayo acheze soka maisha ya mpira wa bongo ni mafupi sana acheni achukue pensheni yake mapema.