Yanga + Africans Sports + Toto Africans = ?
Muktasari:
Kwa wapenzi wa soka hasa, hakuna asiyejua udugu uliopo kati ya Toto African, African Sports na Yanga.
AFRICAN Sports ya Tanga, Toto African ya Mwanza, Mwadui ya Shinyanga na Majimaji ya Songea zimepanda daraja. Zote zitacheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Kwa wapenzi wa soka hasa, hakuna asiyejua udugu uliopo kati ya Toto African, African Sports na Yanga.
Pia, unaweza kuzihusisha Mwadui na Coastal Union kuwa na udugu wa karibu na Simba kwa njia moja ama nyingine.
Udugu wa Simba na Coastal unaonekana kama umekufa kutokana na timu hizo kuingia katika migogoro ya mara kwa mara ya kugombea wachezaji na hata kukoseshana ubingwa.
Mwadui inaweza kuhusishwa na timu hiyo ya Msimbazi kutokana na kocha wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kuwahi kuwa mchezaji na kocha wa Simba pia.
Lakini kamwe huwezi kuzitengenisha African Sports na Toto African kuwa na uhusiano wa kidugu na Yanga ya Dar es Salaam.
Wenyewe wanasema udugu wao ni wa damu si wa kuwatengenishwa hata siku moja! Ni Young (Yanga) African, Toto African na African Sports ambazo zimeunganishwa sana na siasa ambazo zimepitwa na wakati.
Pamoja na yote uhusiano huu siku zote umekuwa na manufaa kwa Simba na Yanga kuliko timu hizo nyingine za mikoani.
Katika michezo ya mwisho ya Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu ) ya mwaka 1988, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ulizikutanisha Coastal Union na African Sports, zilizokuwa zimegawanyika katika itikadi za Usimba na Uyanga.
Pia, siku hiyo, Simba na Yanga zilikuwa zinacheza Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijini Dar es Salaam.
Yanga ilikuwa na nafasi ya kuwa bingwa wa Tanzania Bara kama ingeifunga Simba na Sports ikiifunga Coastal. Aidha Coastal Union ilitakiwa kuifunga African Sports ili itwaye ubingwa na huku ikiomba Simba iifunge Yanga jijini Dar es Salaam.
Hapo palikuwa patamu! Sports haikutaka kabisa Coastal iwe bingwa kwa kuwa itawasumbua kwa kuwabeza, Simba nayo iliona ni heri Coastal Union iwe bingwa kwa kuwa haikutaka Yanga iwasumbue kwa makelele yao!
African Sports haikutaka kuelekezewa matarumbeta ya Coastal, hivyo ikaiahidi Yanga kwamba itaifunga Coastal Union na kuitaka Yanga iifunge Simba ili watwaye ubingwa.
Hadi mwisho wa michezo hiyo African Sports iliikung’uta Coastal mabao 2-0 lakini Coastal Union ilitawazwa kuwa bingwa wa Tanzania Bara baada ya Yanga kufungwa na Simba mabao 2-1.
Juzi, kiongozi mmoja wa African Sports aliliripotiwa akisema kwamba Yanga haikuwasaidia kurudi Ligi Kuu pamoja na kuifuata kuiomba msaada wa kifedha.
Uongozi wa Yanga uliikatalia Sports na kuiambia kwamba hawatambui udugu na klabu hiyo iliyotwaa ubingwa wa Muungano mwaka 1988, bali wanautambua udugu wao na Toto African ya Mwanza.
Hata hivyo, African Sports ilipata msaada wa kulala katika jengo la Yanga pale mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam wakati walipokuwa katika harakati zao za kupanda Ligi Kuu.
Mara baada ya kupanda daraja, Kocha wa Toto African, John Tegete amenukuliwa akisema kwamba Usimba na Uyanga ndiyo unaoua soka la Mwanza.
Inawezekana Tegete kuna kitu amekisahau. Mwaka 2010 akiwa Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba alikuwa sehemu ya itikadi hizo anazozisema leo.
Mara baada ya mwanaye, Jerry Tegete kufunga katika mchezo wa ligi katika uwanja huo, Tegete baba alisahau kazi yake na kwenda kukumbatiana na mwanaye na kushangilia ushindi huo.
Kabla ya hapo, mwanaye huyo alipotakiwa kusajiliwa na Simba wakati akisoma Shule ya Makongo, alikataa na kusema aachwe asome, lakini alipotakiwa na Yanga, haraka alitoa baraka zote.
Jiji la Mwanza limekosa Ligi Kuu kwa muda mrefu kutokana na itikadi za watu wanaojiita wa mpira kujigawa katika ‘dini’ mbili za Usimba na Yanga huku wakisahau kabisa kuzihudumia timu zao.
Toto imekuwa tawi la Yanga kwa muda mrefu na Pamba ilionekana kuwa kama tawi la Simba kwa kuwa ilikuwa ikiifunga Yanga mara kwa mara.
Kuna wafadhili waliwahi kujitokeza kutaka kuisaidia Toto lakini wakaitaka kuachana na itikadi zake za Uyanga jambo hilo lilikuwa gumu, watu wenye Toto yao walikataa katakata.
Toto imelowea kwenye Uyanga kwa kila kitu, kuanzia bango lao hadi jezi za timu hiyo. Ni sawa na Coastal ilivyokuwa haijielewi kwa Simba miaka ya nyuma. Ilifikia hatua Toto ilipokuwa ikicheza na Simba ilikuwa ikichukuliwa na watu wenye itikadi za Uyanga na ilipocheza na Yanga ilichukuliwa na wenye itikadi za Usimba.
Kuna wakati Simba ilipokuwa ikifanya vibaya mashabiki wake waliishangilia Azam FC na kuifanya timu hiyo nayo kuhusishwa Usimba, pia ilitokana na mmiliki wake kuwahi kuifadhili Simba miaka ya nyuma.
Binafsi naona ni bora timu hizi zikawa za kimikoa zaidi kama ilivyo Mbeya City kuliko kuwa matawi ya Simba na Yanga! Zicheze kwa manufaa yao si kwa niaba ya Simba na Yanga.