WPL ikirejea kuna mambo matatu

Muktasari:
- Twiga Stars itacheza dhidi ya Equatorial Guinea Februari 20 na marudiano Februari 26 kabla ya Februari 28 ligi hiyo ambayo imekuwa na msisimko kurejea kibabe ikishuhudiwa pia mchezo wa watani wa Jadi Yanga Princess dhidi ya Simba Queens Uwanja wa KMC Complex, Machi 04.
WIKI ijayo Ligi Kuu ya Wanawake inarejea baada ya mapumziko ya siku 28 kupisha timu za taifa kwenye mashindano ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) yatakayofanyika mwaka huu nchini Morocco.
Twiga Stars itacheza dhidi ya Equatorial Guinea Februari 20 na marudiano Februari 26 kabla ya Februari 28 ligi hiyo ambayo imekuwa na msisimko kurejea kibabe ikishuhudiwa pia mchezo wa watani wa Jadi Yanga Princess dhidi ya Simba Queens Uwanja wa KMC Complex, Machi 04.
Ukiachana na dabi hiyo, siku hiyo pia itapigwa dabi ya Wanajeshi kati ya JKT Queens na Mashujaa Queens ndugu wawili wanaotumia Uwanja wa Mej General Isamuhyo kama ilivyo kwa Yanga na Simba zinazoutumia KMC.
Hadi sasa zimepigwa raundi 12 za ligi ikisaliwa na mechi sita tu kuamua nani bingwa kati ya timu 10 zinazoshiriki ligi hiyo, mfungaji na mchezaji bora kwa maana ya MVP.
Mwanaspoti imekuchambulia mambo matatu ya kuyatazama zaidi ligi itakaporejea hasa ile vita ya kiatu inayowaniwa na warembo wa Simba na JKT.

MBIO ZA UBINGWA
Hadi sasa ikiwa raundi ya 12 Simba Queens na JKT Queens ndizo zina nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa ligi kutokana na pointi walizokusanya ingawa itategemea na matokeo ya mechi zijazo.
Simba inaendelea kusalia kileleni na pointi 34 ikiwa imecheza mechi 12, ikifuatiwa na JKT yenye pointi 29 na Yanga ya tatu na pointi 24, zote zikicheza michezo 11.
Ukiangalia msimamo ulivyo ni wazi kuna vita ya ubingwa hasa kwa Simba na JKT zilizopishana pointi tano, huku watani zikipishana 10.
Simba imekuwa na mwendelezo mzuri tofauti na JKT na imeongoza msimamo mara chache na zote ni kwa sababu Wana msimbazi haijacheza.
Ikumbukwe Simba ndiyo bingwa mtetezi na msimu uliopita ilionyesha ubabe ikiifunga pia JKT iliyomaliza nafasi ya pili nyumbani na ugenini na hivyo kukosa mpinzani mgumu, msimu huu raundi ya kwanza zilitoka sare ya bao 1-1 na kuonyesha upinzani dhidi yao wa nani ataibuka bingwa huku ikisubiriwa zitakapokutana tena na matokeo ya mechi zao nyingine.
Simba kwenye michezo hiyo 12, imeshinda 11 ikitoa sare moja dhidi ya JKT ikifunga mabao 43 na kuruhusu mabao saba, huku Wazee wa Mapigo na Mwendo wakiruhusu mabao matatu kwenye mechi 11, ushindi tisa na sare mbili.
Mbali na vita ya kuwania ubingwa lakini wapinzani hao wa ligi ya wanawake wana ushindani hadi kwenye ufungaji wa mabao wakitofautiana bao moja tu, JKT ikifunga 44 huku Simba 43.

VITA YA KIATU
Miongoni mwa mambo yanayosubiriwa kwa hamu ni vita ya kiatu inayoongozwa na mastaa Stumai Abdallah wa JKT anayeongoza ufungaji akiwa na mabao 18 na Mkenya Jentrix Shikangwa wa Simba mwenye 17.
Stumai ambaye ni mzawa amefikia mabao hayo 18 baada ya mchezo wa mwisho dhidi ya Mlandizi Queens akifunga saba katika ushindi wa mabao 12-0 akiweka rekodi mpya ya mchezaji aliyefunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja wa michuano hiyo.
Katika mabao hayo likiwamo moja la penalti, 13 ameyafunga kwenye mechi tatu tu, dhidi ya Mlandizi Queens (7), Alliance Girls (3) na Malndizi Queens (3).
Mbio hizi ni muhimu zaidi kwa Mtanzania huyu ambaye anatafuta rekodi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya misimu iliyopita kushuhudia zikienda Msimbazi.
Ni timu mbili tu za Simba Queens na Yanga Princess ambazo mshambuliaji huyu mzawa hajazifunga msimu huu, huku timu nyingine nane akiziadhibu vikali.
Mshambuliaji huyo ana hattrick tatu alizozifunga dhidi ya Mlandizi Queens (3), Alliance Girls (3) na Mlandizi Queens (7). Mabao saba aliyoyafunga kwenye mchezo dhidi ya Mlandizi alitupia dakika ya tatu, tano, 14, 18, 25, 36 na 88.
Nyota raia wa Kenya, Shikangwa anatafuta kiatu cha pili cha ufungaji bora baada ya kukibeba msimu wa 2022/2023 akitupia mabao 17.
Mabao yake 17 msimu huu hadi sasa ameyafunga katika mechi nane kati ya 12 za timu yake, huku akizionea zaidi Fountain Gate na Ceassia Queens alizozifunga nje ndani.
Shikangwa amefunga hat trick tatu dhidi ya Gets Program akitupia mabao matatu, Mlandizi Queens akitupia manne na Fountain Gate akifunga matatu. Pia amefunga mabao mawili mawili dhidi ya Alliance Girls na Ceassia Queens.

REKODI ZAO MISIMU MITATU
2022/23
Stumai mabao 14 mechi tisa
Shikangwa mabao 17 mechi 18
2023/24
Stumai mabao 19 mechi 18
Shikangwa mabao nane mechi tisa
2024/25
Stumai mabao 18 mechi 11
Shikangwa mabao 17 mechi 12

NAFASI YA TATU
Achana na mambo ya ubingwa, ligi itakaporejea miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kutazamwa kwa jicho la pili ni vita ya nafasi ya tatu ambayo Yanga imeendelea kushikilia hapo.
Tangu msimu uanze Wananchi hawajawahi kugusa baridi la kileleni ikiendelea kushikilia nafasi hiyo ambayo pia inatolewa jicho na Mashujaa Queens iliyopo nne bora.
Yanga ya Edna Lema 'Mourinho' imekusanya pointi 24 tofauti ya alama sita na Mashujaa yenye 18 ikishinda mechi tano, sare tatu na kupoteza michezo minne.
Hapa itategemea Yanga itashinda michezo yake kwani ikipoteza inaweza kuwa faida kwa Mashujaa ambayo nayo matamanio makubwa msimu huu ni kumaliza nafasi ya tatu na kushiriki mashindano ya ngao ya jamii kwa wanawake.

WASIKIE WENYEWE
Kocha wa Simba, Yussif Basigi alisema licha ya ugumu wa ligi hiyo lakini matamanio makubwa kwa Simba ni kuutetea ubingwa wao na kubwa zaidi kwake kuandika rekodi mpya ukiwa msimu wa kwanza tu.
"Matamanio yetu kama timu ni kushinda kila mchezo na kutetea ubingwa wetu, najua tunakutana na wapinzani wagumu nao wakitaka ushindi, lakini kwetu na kwangu mimi natamanani kuandika rekodi mpya," alisema Basigi ambaye ni msimu wa kwanza kucheza Ligi ya Tanzania akitokea Ghana.
Kocha wa JKT Queens, Esta Chabruma alisema kila timu imejipanga kushinda michezo yake lakini kwa upande wao watapambana vilivyo kuhakikisha hawapotezi mchezo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ubingwa.
"Unaangalia tunakimbizana na timu ambazo zinacheza vizuri na kushinda karibu kila mchezo, sisi JKT hatuangalii matokeo ya wenzetu kikubwa ni kushinda na kujiweka pazuri na mwisho wa msimu kujua nani anatwaa ndoo kwa sababu ligi bado mbichi."