Prime
Wallace Karia anaweza kuuingia mtego huu

KWA hali ilivyo ni kwamba, Wallace Karia ndiye mshindi wa uchaguzi wa kiti cha Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama hakutatokea jambo lisilo la kawaida na lisilotegemewa baada ya wanachama 46 kumuidhinisha, au kwa maneno mengine kumpigia kura kabla ya siku ya uchaguzi.
Lakini inaweza kuwa ni mtego iwapo kutakuwa na juhudi kama zile zilizofanyika mwaka 2002 za kumuondoa Mwenyekiti wa wakati ule wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga (Mungu amrehemu) kabla ya kuwa Shirikisho la Soka (TFF).
Wakati ule, ilikuwa nadra kwa mpinzani wake kupata hata robo ya kura, wadau waliokuwa nje ya mfumo wa uongozi waliunganisha nguvu na kumuondoa Ndolanga. Lakini sasa wapinzani wa Rais hawawezi hata kuomba kura au hata kufika katika boksi la kura.
Kama wanachama 46 wamempitisha Karia na jumla ya wapiga kura ni 76, maana yake waliomuidhinisha wamevuka nusu ya idadi ya wapigakura na kinachosubiriwa ni kuthibitisha rasmi kwa njia ya kuandika katika karatasi za kupigia kura.
TFF ina wanachama 47 ambao ni mikoa 26 ya kijiografia, vyama shiriki vitano (cha wachezaji, madaktari, marefa, makocha na wanawake) na klabu 16 za Ligi Kuu.
Kila mkoa una wapiga kura wawili, hivyo inawezekana na baadhi ya klabu (kama ile ambayo msemaji wake amejirekodi akisema mitano mingine kwa mgombea) nazo zimeafiki Karia aendelee, kitu ambacho si kibaya kama kikifanywa kwa nia njema na si kuzuia wengine kwa kubadili kanuni na sheria kwa malengo binafsi.
Ndio, CCM iliazimia kumuidhinisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa urais kwa chama hicho, lakini haikutanguliza kubadili kanuni na katiba yake ili kuweka ugumu kwa wengine waliokuwa wanadhamiria na haijabadilisha. Isitoshe mwanachama ambaye anaona ni vigumu kubadili hali hiyo, anapo pa kukimbilia kwa kuwa nchi imeruhusu siasa za vyama vingi. Hivyo, ugumu huo utakuwa katika utashi wa wanachama na si sheria na kanuni.
TFF imeweka ugumu huo katika sheria na kanuni na ndio maana inaonekana si rahisi kwa Karia kushindwa katika uchaguzi, ingawa pia si lazima ashindwe.
Kwa mujibu wa marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi, mgombea wa urais ni lazima aidhinishwe na wanachama watano kama idadi ya chini, lakini haijaweka kiwango cha juu cha idadi ya waidhinishaji. Hapohapo imekataza mwanachama kuidhinisha zaidi ya mgombea mmoja, ndio maana mgombea mmoja tu ameambulia idhini ya mwanachama mmoja aliyesalia baada ya Karia kuzoa 46. Yaani kanuni hiyo imetaka iwe kama ya ndani ya vyama vya siasa ambako mgombea hutafuta wadhamini wengi kuonyesha nguvu yake kwenye chama, ingawa haihusiani na kura kwa kuwa si wadhamini wote wanaoenda kupiga kura. Hii ya TFF inaonyesha idadi ya kura.
TFF ina idadi ndogo ya wanachama, yaani 47 tu huku kura zikiwa 76, na hivyo kuweka sheria kama hiyo ni kuzuia wengine kuingia katika uchaguzi.
Hadi sasa waliochukua na kurudisha fomu za kuwania urais ni sita, lakini ni Karia pekee aliyepata wadhamini watano wanaotakiwa na wengine 41 wa ziada.
Huyo mwanachama mmoja pekee aliyesalia ndiye anaweza kuweka pingamizi kwa Karia, kwa mujibu wa kanuni zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2021, zinazotaka wanachama pekee ndio wana haki ya kuweka pingamizi dhidi ya wagombea, tofauti na zamani wakati mwanafamilia yeyote alikuwa na haki hiyo.
Kwa hiyo mpira wa miguu hauna chaguo kwa sasa bali ni kusubiri tu taratibu zifuatwe ili Karia atangazwe kuwa rais, kitu ambacho hakitakuwa siha kwa mpira wetu.
Hata hivyo, bado Karia anasubiri kuruka viunzi kadhaa vya kiufundi kabla ya kujihakikishia ofisi kuu ya mchezo huo maarufu nchini.
Uamuzi wa kumuidhinisha uliopendekezwa na Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu mjini Moshi na baadaye kuungwa mkono na Rais wa Yanga, Hersi Said, ulifanywa mwaka mmoja uliopita wakati wa kuchangia moja ya ajenda za mkutano mkuu wa kawaida.
Katika miezi ya hivi karibuni, Yanga imeingia katika mgogoro mkubwa wa uendeshaji Ligi Kuu dhidi ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na baadaye TFF baada ya Simba kugomea mechi ya Machi 8 kwa madai kuwa ilifanyiwa fujo na kuzuiwa kuingia uwanjani kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi hiyo.
Mzozo huo ulikua mkubwa kiasi cha kufikia upande wa Yanga kuzozana na Karia, hasa vigogo hao wa Jangwani walipotaka viongozi wakuu wa Bodi ya Ligi wajiuzulu na Karia kuwajibu kuwa matakwa yao yanalenga kuharibu mafanikio yaliyopatikana na kusema kama wanataka sinema waende kucheza sinema zao.
Mzozo ukakua na kukua hadi kugusa mashindano ya Kombe la Shirikisho na kusababisha siri kadhaa za kifedha kuwekwa hadharani. Lakini Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliingilia kati na kusuluhisha.
Katika sakata hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto, aliyekuwa Mwenyekiti wa Coastal Union, alilazimika kuandika barua ya kujiuluzu baada ya kuongoza kikao kilichoahirisha mechi kiholela kwa kuhofia timu moja kushushwa daraja, huku Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Almasi Kasongo, Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka cha Dar es Salaam (DRFA) akisimamishwa.
Ilikuwa ni sharti la Yanga kwamba wawili hao pamoja na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, waondoke ndipo wakubali kucheza mechi yao na Simba, lakini baada ya Mnguto na Kasongo kuondoka, Yanga walikubali kuingia uwanjani.
Matokeo ya mgogoro huo yameonekana kwa upande wa Yanga. Haikuwa ajabu kuona Yanga ikimuidhinisha mgombea mmoja wa urais, Ally Mayay licha ya kuunga mkono azimio la Moshi. Pengine ilitumaini kuwa Mayay angepata wadhamini wengine wa kutosha na kuweka upinzani kwa Karia. Lakini hakuweza, mgogoro haukuwa umefika mbali hivyo.
Maana yake, endapo kutatokea lolote lile litakalosababisha wagombea wengine kuingizwa katika mchakato kwa kuibatilisha kanuni hiyo kiufundi, kuna uwezekano vita ya urais ikawa nguvu kwa Karia kama Yanga wataamua kuweka sumu kali kama kisasi.
Mbali na mgogoro huo inawezekana kuna mabadiliko makubwa ya misimamo yametokea tangu wajumbe wa mkutano mkuu walipopitisha Azimio la Moshi kulingana na matukio yaliyotokea katika miezi ya hivi karibuni, hasa sakata la mechi ya Simba na Yanga lililodumu kwa miezi mitatu na kuweka hadharani matatizo mengi katika uendeshaji na usimamizi wa mpira wa miguu.
Kama ni kweli walimuidhinisha baada ya kuchukua fomu, Karia hatakuwa na tatizo, lakini ikibainika kuwa barua za idhini zilishaandikwa hata kabla ya tarehe ya uchaguzi kutangazwa, uchaguzi utakuwa umefunguliwa upya na vita ya urais kuwa mpya huku sakata la dabi likiwa na nafasi kubwa.
Katika uchaguzi wa kiti hicho, Karia anapambana na wanafamilia wengine wanne waliochukua fomu na ambapo hawatarajii kufikia boksi la kura. Hao ni Ally Tembele, mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Mshindo Msolla, kocha mzoefu na rais wa zamani wa Yanga, Richard Shija, mjumbe wa zamani wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Ally Thabit Mbingo, ambaye si maarufu sana katika soka, na Mustapha Salum Himba, ambaye ni mjumbe kwenye kamati za Yanga.
Pamoja na kutopata wadhamini wa kutosha, wanafamilia hao wa soka wamerejesha fomu wakijua kabisa kuwa kanuni haziwaruhusu kufika chumba cha uchaguzi kwa kuwa wataenguliwa mapema.
MATARAJIO YAO
Kanuni zinaweza kubadilishwa? Inavyoonekana kanuni zimeshapitishwa na Msajili wa Vyama vya Michezo baada ya kutangazwa gazetini. Hapo ni suala la Msajili kukubali udhaifu na kuzirudisha kwake ili kuondoa kasoro inayoondoa usawa na haki katika uchaguzi. Hili liko mikononi mwake na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) haliwezi kulitangaza kama ni kuingilia shughuli za soka.
Moto wa mpira wa miguu au kaulimbiu kuu ni ‘fair play’ au mchezo wa haki na hii si uwanjani pekee, bali katika kila kitu kinachohusu mchezo huu maarufu duniani.
Ulaya wameingiza fair play hadi katika masuala ya kifedha kwamba mapato yatokanayo na mpira ndiyo hayo yatumike kugharimia mpira na matumizi yasizidi mapato.
Hivyo hata katika uchaguzi ni lazima kuwepo na Fair Play ili wote wale walio na mapenzi na mchezo huu wawe na haki sawa ya kuingia na kujaribu kile wanachoweza na si kufungiwa milango kana kwamba ni mchezo wa kitaaluma.
Pia kuna jitihada zinazoendelea za kutaka Baraza la Michezo (BMT) au kwa maneno mengine wizara inayohusika na michezo itangaze kuwa sheria ya uchaguzi za TFF inapingana na Sera ya Michezo ya 1995 inayotaka vipindi vya uongozi viwe viwili kwa jumla ya miaka nane au vitatu kwa jumla ya miaka tisa.
Hilo nalo haliwezi kuwa ni kuingilia kwa shughuli za mpira kwa sababu ni lazima vyama viheshimu mamlaka za nchi kisheria na kisera. Hilo ndilo lililotokea nchini Kenya, ambako mwenyekiti aliyetaka kutetea kiti chake alizuiwa kwa sababu alishamaliza vipindi vyake kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo na hivyo kulazimika kugombea nafasi ya makamu wa rais.
Na katika hilo, Mustapha Himbo ameshadokeza anachokusudia na pengine kitakuwa kimepewa nguvu na wenzake.
“Mimi kama mtia nia katika huu uchaguzi, nitatafuta haki yangu kwa sababu haiwezekani, nimesema haiwezekani hata kidogo nikatoa 500,000 yangu halafu mtu akaila,” alisema Himbo alipozungumza na waandishi baada ya kurudisha fomu.
“Nimehangaika kwa jitihada zote ambazo nimezifanya kwa uwezo wangu kupata at least (angalau) hizo endorsements (wadhamini) tano, lakini kila ninapopiga, kila ninapotawafuta wenye mamlaka ya hizo endorsements, wanasema zimeshatolewa.
“Nini maana yake? Kwamba mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF amekuja kuulaghai umma kwa kutuambia tukachukue fomu, either (ama) kwa kujua au kutojua kwamba endorsements zimeshachukuliwa. Kwa taarifa endorsements zinazotakiwa ni 47, lakini kwa taarifa zilizopo ni kwamba endorsements 46 zote zimeshatolewa.”
Himbo anasema kwa kuwa uchaguzi ni mchakato, uidhinishaji huo ulitakiwa ufanywe baada ya wagombea kuanza kuchukua fomu na si kabla.
Himbo anasema hakubali. Lakini ataishia wapi katika kudai haki yake? Au akipewa Sh.500,000 yake atanyamaza? Uwezekano wa kurudishiwa hizo fgedha haupo kikanuni, hivyo anajua atazidai wapi.
Mgombea mwingine, Shija, aliahidi kufikisha malalamiko yake kwa Kamati ya Rufaa ya TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) akitaja kuzuiwa kwa uchaguzi na kupinga uhalali wa Karia kupata udhamini wa vyama 46 na hivyo kuwanyima wengine fursa hiyo.
“Tukisema tuendelee na uchaguzi, tafsiri yake ni kwamba kuna mtu ataingia kwenye uchaguzi akiwa mgombea pekee, kitendo ambacho ni kunajisi uchaguzi,”alisema Shija ambaye hakupata udhamini.
Alisema mchakato wa uchaguzi unapaswa kurudiwa upya ili ufanyike katika mazingira ambayo wadhamini watakuwa huru na wagombea wote washiriki uchaguzi mkuu.
Njia yake kupitia mkono wa serikali katika michezo ilishafuatwa na wakili Cletus Tharcisiusy ambaye amewasilisha BMT barua ya pingamizi dhidi ya Karia kwamba anakiuka sera ya michezo ya mwaka 1995 kwa kugombea kipindi cha tatu.
”Nimekuja BMT kutoa malalamiko juu ya mabadiliko ya Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, hususani Ibara ya 37 juu ukomo wa muda wa kuongoza, ibaki miaka mitatu mara tatu na sio miaka minne mara tatu,” alisema Wikili Tharcisiusy.
“Kabla ya mabadiliko ya katiba ya TFF, rais alikuwa anakaa madarakani kwa miaka mitatu kwa vipindi vitatu kama atapata, ila ya sasa Rais wa TFF anakaaa madarakani miaka minne kwa awamu tatu kama atapata.
”Haya mabadiliko yamekiuka sera ya michezo ya taifa, kanuni na taratibu zinazotumika kuendesha mpira wa miguu.”
Hili ni eneo linaweza kubatilisha ushiriki wa Karia na ama kwa mamlaka ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kama kweli itazingatia sheria, kanuni na sera ya nchi, au Msajili wa Vyama vya Michezo kama atakakubaliana na hoja hiyo, kama ilivyokuwa kwa Nick Mwendwa alipojaribu kugombea kipindi cha tatu cha uongozi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).
Katiba ya TFF ilifanyiwa marekebisho mwaka 2019 kuweka vipindi vitatu vya miaka minne kwa urais na jumla yake kuwa miaka 12, tofauti na sera inayotaka jumla ya miaka nane tu, isipokuwa kwa Kamati ya Olimpiki ambayo vipindi vyake ni miaka mitatu.
Wagombea wengine hawajaweka bayana watafanya nini kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki, lakini inaonekana wengi wanasubiri Kamati ya Uchaguzi ifanye mchujo ndipo harakati rasmi zianze.
Katika uchaguzi uliopita, mgombea mmoja wa urais wa TFF, Ally Abdullah Saleh alifika Mahakama Kuu kufungua shauri la kupinga kuenguliwa katika uchaguzi na kuomba amri ya muda ya kuzuia uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 7, 2021 hadi shauri kuu lifanyiwe uamuzi.
Hata hivyo, Jaji E.E Kakolaki alisema katika uamuzi wa ombi la amri ya muda kuwa mlalamikaji hakuweza kuthibitisha athari ambazo zingepatikana kwa uchaguzi kufanyika wakati shauri kuu halijafanyiwa uamuzi.
Hakukuwa na mgombea aliyekata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF kupinga kuenguliwa au kupinga kanuni ambazo zilitumika kuwaengua kuwa zilikiuka misingi ya kidemokrasia, lakini inaonekana safari hii kobe ameinamisha kichwa. Tusubiri atakapokiinua.