Prime
Murtaza Mangungu, mbuzi wa kafara aliyelaza shingo

RAFIKI yangu Murtaza Mangungu. Huwa ni Mwenyekiti wa Simba wakati Simba inapopitia wakati mgumu. Ni kama ambavyo sasa hivi anarushiwa mawe kutoka kila pembe ya nchi. Akikwepa jiwe moja inabidi ainame tena kukwepa jingine. Maisha nyakati hizi huwa ni magumu kwake.
Simba ikishinda huwa nafasi yake ya Uenyekiti inaondoka. Hapewi sifa zozote wala hakumbukwi. Sifa zinakwenda kwa tajiri, Mohammed ‘MO’ Dewji. Sifa zinakwenda kwa Ellie Mpanzu. Sifa zinakwenda kwa Moussa Camara. Uenyekiti wake unaondoka ghafla. Simba ikiondoka bila ya taji uenyekiti unarudi kwa Murtaza Mangungu.
Simba imepigwa mara ya tano mfululizo na Yanga na ghafla Mangungu amekumbukwa. Tulishamsahau wakati Simba ilipofanikiwa kutinga fainali za Shirikisho Afrika na kucheza na RS Berkane ya Morocco. Baada ya Simba kutochukua Kombe la Shirikisho Afrika tulimuweka kiporo kusubiri pambano la watani. Bahati mbaya pambano la watani wa jadi lilikuwa linaamua hatma ya Simba kwa msimu mzima.
Kuna ambao wanamshutumu Mangungu kwa Simba kupokea vichapo vitano mfululizo kutoka kwa watani. Ukweli ni kwamba mashabiki wengi wanakwepesha goli. Wanaamua tu, kumuangushia lawama Mangungu. Bahati nzuri kuna watu wanapaswa kuwajibika ndani ya Simba na wanafurahi kuona lawama zinakwenda kwa Mangungu na sio wao.
Mashabiki wana hofu ya kumshutumu tajiri kwa sababu wanajua anaweza kususa. Mpira pesa katika nyakati hizi. Zama zile ambazo timu ilikuwa inaendeshwa kwa viingilio vya mechi, ingekuwa rahisi kuanzisha vurugu, lakini siku hizi Simba na Yanga zimeshika adabu kwa matajiri. Hapo katikati Yanga wakiwa na Yusuf Manji, huku Azam wakiwa na familia ya Bakhresa Simba ilishika nafasi ya tatu kwa misimu minne mfululizo.

Heshima kwa matajiri imerudi kwa kiasi kikubwa licha ya klabu zetu kuwa na vyanzo vingi vya mapato. Tatizo tumetanua goli kwa kuwa na matumizi makubwa klabuni. Kuanzia usajili wa wachezaji hadi huduma zao za kila siku. Ndio maana bado tuna heshima kubwa kwa matajiri kiasi kwamba hatuwezi kuwanyooshea vidole moja kwa moja.
Wanahofia pia kuwashutumu watu walio karibu na tajiri kwa sababu wanajua kwamba tajiri pia anaweza kususa. Hatimaye mtu ambaye inakuwa rahisi kumshutumu ni Mangungu. Hasira zinamaliziwa kwake na watu ambao ama wanafanya makusudi au hawajui kinachoendelea ndani ya timu.
Walio karibu na tajiri ndio ambao wanawajibika kutengeneza timu moja kwa moja pamoja na uendeshaji wa timu kila siku. Kwa miaka minne ambayo Yanga wanaburuza kuna watu ndio wanapewa pesa za kusajili wachezaji. Mangungu huwa hahusiki katika hilo zoezi. Wachezaji wanaoletwa huwa hawana hadhi ya kuvaa jezi ya Simba.
Kuna mengi huwa yanasemwa nyuma ya pazia. Kwamba tajiri anapigwa pesa zake. Hatujawahi kusikia tetesi za kwamba tajiri anapigwa pesa na Mangungu. Tunasikia tu kwamba tajiri anapigwa pesa na watu wengine. Hata hivyo, Simba ikiwa katika mwenendo mbaya jiwe linarushwa kwa Mangungu. Watu wanahofia kuwarushia mawe chawa wa tajiri kwa sababu wanahisi tajiri atachukia.

Wakati hayo yakiendelea kuna wanachama na mashabiki ambao wanafahamu wazi nguvu ndogo ya Mwenyekiti kwa mujibu wa katiba yao. Sidhani kama Mwenyekiti wa Simba ana nguvu kubwa ya uamuzi katika kuendesha timu. Hili nalo linafumbiwa macho kwa makusudi tu, ili Mangungu aendelee kutolewa kafara pindi mambo yanapokwenda kombo.
Nini kifanyike? Simba inapaswa kurudi katika ramani yake kiurahisi tu. Kama wanaamini kwamba mtani anafanikiwa basi wajikumbushe kwamba tatizo la kwanza la baadhi ya watu wanaodhani wao ndio wenye Simba yao ilianzia pale walipomdharau Hersi Said. Kuna watu wanajiona wao ndio Simba na mara nyingi badala ya kufanya mambo kisasa wao wamekuwa wakijivunia historia yao na klabu hii. Wengi wanatoka katika kundi la Friends of Simba.
Simba haijataka kuruhusu akili mpya kama ambavyo Yanga wamefanya. Hata utakaposema kwamba Simba imefanikiwa kufika fainali za Shirikisho wanajua kwamba wamefuata nyayo za watani wao ambao walishafanya hivyo miezi 24 kabla yao. Bado kuna akili mpya inahitajika Simba katika mambo mengi.

Kina Swedi Mkwabi waliingia katika timu kama vijana wenye nguvu mpya, lakini wakapigwa majungu kwa tajiri wakatimuliwa. Akawekwa rafiki yangu Mangungu kwa sababu waliamini wangemuweka mfukoni na pia kukubali kupokea mawe ambayo leo anapigwa na ameweza kukaa kimya. Mkwabi asingeweza kukubali haya mawe.
Usajili wa Simba umekuwa wa ovyo. Hapa tunazungumzia ukweli kwamba hata mida hii Simba itakuwa inahangaika kuvunja mikataba ya baadhi ya mastaa ambao wamekuja klabuni hapo miezi 10 tu iliyopita. Na hawa mastaa walikuja kuchukua nafasi za kina Papaa Jobe. Mangungu hajahusika lolote na jambo hilo. Mashabiki na wanachama wanajua, lakini wanakwepesha goli kwa sababu ya kuhofia huenda tajiri atanuna.

Simba irudi katika ramani tu. Mangungu sio tatizo la msingi. Kuna matatizo mengi ya msingi katika Simba, lakini sio Mangungu. Wanaoleta matatizo katika Simba wanafurahi kuona Mangungu anatolewa kafara, huku wao wakiwa wamejificha nyuma ya mbuyu. Mangungu hashirikishwi katika mambo mengi ya msingi ndani ya timu.
Uzuri ni kwamba Mangungu mwenyewe amekubali kuwa mbuzi wa kafara. Analaza shingo yake wanachama na mashabiki wamchinje kadri wanavyojisikia. Hata hivyo, yeye mwenyewe anajua kwamba hahuhusiki kwa lawama nyingi ambazo amekuwa akitupiwa kila uchao.

Kama Mangungu akiamua kufungua kifua chake nadhani nchi inaweza kusimama. Ana mengi ya kusema, lakini ameamua tu kuwa mnyonge ili mambo yaende. Naye pia inawezekana ana hofu ile ile ya wanachama. Hofu ya kumpoteza tajiri. Kitu kibaya zaidi ni kwamba akiamua kufungua mdomo yanaweza kumkuta yale yale ambayo yalimkuta Mkwabi.