Prime
Winga aliyesepa Yanga awataja mastaa wawili
OFFEN Chikola, winga aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha kubwa la majira ya kiangazi lililopita ameondoka ndani ya kikosi hicho.
Chikola, winga ambaye msimu juzi aliifunga Yanga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 ilioupata Tabora United (sasa TRA United) katika mchezo wa Ligi Kuu bara wakati huo, alionekana kuzivutia timu nyingi nchini kuitaka saini yake mara tu baada ya kumalizika kwa msimu huo.
Hata hivyo, ilikuwa ni Yanga iliyofanikisha dili kwa kumnyakua mchezaji huyo na kuanza naye maandalizi ya msimu (pre-season) mapema tu, ambapo katika mechi ilizocheza timu hiyo hapa nchini na nchini Rwanda ilikoalikwa katika michuano maalumu alikiwasha kwelikweli na kuwafanya mashabiki wa Jangwani kukoshwa na kiwango chake.
Hata hivyo, maisha yanakwenda kasi katika soka. Chikola alijikuta akikosa namba ya kuanza kikosini mara kwa mara na hii ni mara tu baada ya msimu wa mashindano wa 2025/26 kuanza, na ni hapo akaamua kukubali kutolewa kwa mkopo.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, winga huyo machachari amegusia safari yake mpya ya kutua Singida Black Stars (SBS) kwa mkopo akieleza kuwa uamuzi huo haukuwa wa bahati mbaya, bali ni mkakati maalumu wa kuboresha kiwango chake.
Anasema alipokea ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, aliyemweleza dhamira ya kumuona anapata dakika nyingi zaidi uwanjani ili aendelee kuwa bora zaidi.
Chikola anasema Goncalves anaamini uwezo, nidhamu na bidii aliyonayo, lakini ushindani mkubwa uliopo ndani ya kikosi cha Yanga umemfanya apate muda mchache wa kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.
ANACHOTAKA KOCHA
Chikola anamzungumzia Goncalves akisema: "Aliniambia anaona uwezo wangu, bidii na nidhamu ya juu niliyonayo. Anachotaka ni mimi kucheza mara kwa mara ili kiwango changu kiwe juu tofauti na Yanga kuna kikosi kipana cha wachezaji wazoefu na viwango bora.
"Natambua Singida kuna wachezaji wazuri wenye ushindani mkali. Kocha alisisitiza atakuwa ananifuatilia maendeleo yangu, hivyo sichukulii kama nimepunguziwa kazi, badala yake natakiwa nizidishe mazoezi na kujifunza."
Akiwa Yanga washindani wake wa namba walikuwa ni Pacome Zouzoua ambaye msimu uliopita alifunga mabao 12 na asisti 10 ilhali huu wa 2025/26 ana mabao matatu pamoja na asisti mbili, huku Maxi Nzengeli alifunga mabao sita na asisti 10 na huu ana mabao mawili na asisti mbili.
Wengine ni Clement Mzize ambaye msimu wa 2024/25 aliondoka na mabao 13 na asisti tano. Mastaa wengine waliopo Yanga ambao ana bato nao la namba ni Edmund John na Allan Okello.
Lakini, kwa upande wa Sigida Black Stars atakwenda kukutana na ushindani dhidi ya Ayub Lyanga, Lamine Jarjou, Mishamo Daudi na Deus Kaseke.
PACOME MWAMBA
Kwa Chikola, anasema kwa muda ambao amekuwapo Yanga amejifunza vitu vingi kutoka kwa Pacome kuanzia mazoezini, anavyoishi na wachezaji wenzake pamoja na ucheshi kwa kila mtu licha ya jina lake kuwa kubwa.
"Anachofanya Pacome katika mechi kinaanzia mazoezini ambako anajituma kwa bidii na kuonyesha nidhamu ya juu. Tofauti na ustaa wake anazingatia muda kufanya vitu vyake, kiukweli nimejifunza kitu kutoka kwake," anasema Chikola.
"Ni mtu wa vaibu na ucheshi kwa kila mtu. Anaheshimu kile kinachofanywa na wengine na kuona anapata ushindani halisi wa kuendelea kumfanya awe bora, pia anajishusha kwa kila mtu bila kujali jina lako kubwa au la".
WOSIA WA NZENGELI
Mchezaji huyo alipata muda wa kukaa kwa karibu na Nzengeli aliyemuelekeza nini afanye ili awe mchezaji mkubwa na kiwango chake kuwa juu.
"Kitu kikubwa aliniambia niwe naenda kanisani kumuomba Mungu anisaidie katika kazi zangu, na niwe mwaminifu wa kutoa sadaka na fungu la kumi kwa uaminifu na kusema hayo ndiyo yanamfanya upande wake awe na maendeleo mazuri," anasema Chikola.
"Nzengeli ana moyo wa kipekee na upendo, anapenda kumuona kila mtu akifanikiwa. Kwa ujumla wachezaji wa Yanga wanaishi kwa umoja na upendo wa hali ya juu. Ukiwa kambini unaiona ni familia iliyo pamoja. Kiukweli nitawakumbuka sana."
FUNZO YANGA
Ingawa Chikola amekaa muda mfupi Yanga hajaondoka bure, yapo mambo aliyojifunza hasa kutochukulia vitu kawaida mbele ya jamii.
"Mazingira ya Tabora United niliyokuwa nimetokea kabla haijaitwa TRA ni tofauti. Hilo limeniongezea kujua thamani yangu na kipi nikifanye. Kuhusu maisha, kama wachezaji hayana tofauti kubwa kwani hata Tabora ilikuwa na wa kigeni kama Heritier Makambo ambaye alikuwa ananishauri nikitaka kuwa mchezaji mkubwa nizidishe nidhamu na mazoezi.
"Ukiingia Yanga unapopita mtaani unakuwa umebeba brand (chapa) yao, lazima maisha yako yawe na nidhamu ya juu. Pia nimejifunza ushindani wa hali ya juu."
Anasema katika DM yake kwa sasa imejaa ujumbe wa mashabiki wanaomwambia mambo mengi mazuri ikiwamo "wanampenda" aende Singida kupambana ili kiwango chake kikipanda arejee Yanga kwa mara nyingine.
"Sikutegemea kama wangenipa moyo wa kunitaka nikapambane kwa bidii. Hilo limeniongezea ari na nguvu mpya ya kuona nina nafasi ya kufanya mambo makubwa katika mpira wa miguu," anasema.
MECHI YAKE YA KWANZA
Japokuwa mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Spors ya Rwanda aliyocheza dakika 45 akiwa Yanga na timu hiyo ikashinda mabao 3-1, alitoa asisti ya bao la tatu.
"Hiyo mechi nitaikumbuka kwa mambo mengi. Ilikuwa kwa mara ya kwanza kuvaa jezi ya Yanga na nilicheza kwa kiwango kizuri," anasema.
MAZOEZI BINAFSI
Kuna muda Chikola alionekana katika picha ya pamoja akiwa na mkufunzi wa mazoezi maarufu kama Denzel, na hilo analizungumzia akisema ilikuwa ni harakati za kujiongeza kwa zoezi la ufiti.
"Nilimtafuta na kumuonyesha video za mechi zangu za nyuma. Aliniambia unahitaji kuwa fiti zaidi. Nilikuwa nafanya hilo kabla ya kuja Yanga, ulichokiona ni kama mwendelezo," anasema Chikola.
"Kwa Yanga muda ambao tulikuwa tunapewa wa mapumziko nilikuwa nautumia kwenda kufanya mazoezi yangu binafsi na watalamu. Hilo lilinisaidia kujiamini na ndiyo maana sina wasiwasi kwenda Singida kwani najua nitakwenda kupambana.
"Kuna muda mwingine nikiwa kambini baada ya mazoezi ya timu nilikuwa namfuata kocha wa viungo anisaidie kunielekeza mazoezi nayotakiwa kuyafanya kwa muda mwingi."