Prime
Presha mashine tano mpya, kocha Yanga apigilia msumari
KIMAHESABU ni kama vile Yanga imeshamaliza usajili wa kikosi cha timu hiyo kupitia dirisha dogo na hadi sasa kuna wachezaji wapya watano wenye uhakika wa kuingia kukiongezea nguvu, ila kuna vita inawasubiri ndani ya timu hiy wanayotakiwa kukabiliana nayo fasta.
Yanga hadi sasa imeshatangaza kuwasajili mshambuliaji Emmanuel Mwanengo kutoka TRA United (zamani Tabora United), Mohamed Damaro kutoka Singida Black Stars na kiungo mshambuliaji Allan Okello (Vipers) aliyetua nchini.
Wengine ni mshambuliaji Laurindo Aurelio 'Depu' kutoka Radomial Radom ya Poland anayetarajiwa kutua wakati wowote na beki Yao Kouassi aliyerudishwa katika mfumo wa usajili baada ya kupona majeraha ya muda mrefu.
Mastaa hao watano wataingia Yanga, lakini wakitarajiwa kukabiliana na mambo mbalimbali ambayo yatawataka kuthibitisha ujio wao katika kikosi kilichopo chini ya kocha Pedro Goncalves ambaye ni usajili wake wa kwanza tangu apewe ajira hiyo.
Tuanze na Mwanengo, wakati Yanga ikisubiri kuona kama ilipatia kumsajili kiungo mshambuliaji Offen Chikola akitokea TRA United, anaungana na mshambuliaji huyo ambaye walikuwa wakicheza pamoja.
Ujio wa Mwanengo ni katika hesabu za Yanga kutafuta mshambuliaji mzawa anayekuja kuongeza nguvu iliyopungua kutokana na Clement Mzize ambaye hakuwapo kikosini kwa muda na ambaye anaendelea kujipanga kurejea uwanjani baada ya kuumia goti.
Mwanengo alikuwa staa muhimu ndani ya TRA, lakini hakuwa na takwimu bora ambapo kwenye mechi saba hadi anaachana na timu hiyo hakufanya makubwa sana, akicheza mechi sita akikosa moja dhidi ya Pamba Jiji, huku akiwa hana bao zaidi ya kutengeneza asisti moja kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars.
Mshambuliaji huyo anatakiwa kujipanga sawasawa kuonyesha thamani yake akijiunga na timu ambayo itampa kila huduma na kusalia kwake kuonyesha ubora ili kumshawishi kocha, huku akianza vyema kwenye mashindano ya Mapinduzi yaliyomalizika juzi alikofunga mabao mawili, akitakiwa kupigania namba mbele ya Prince Dube na Depu atakapofika.
DAMARO MFUPA MGUMU
Yanga inapambana na vita ya kufukia kivuli cha kiungo Khalid Aucho ambaye baada ya utumishi uliotukuka, akashushwa Moussa Conte, viatu vikaonekana kumshinda kuwasahaulisha mashabiki wa timu hiyo juu ya mazuri ya mtangulizi wake, na sasa ameshushwa Damaro.
Baada ya Aucho kwenda Singida Black Stars akitokea Yanga, alififisha nafasi ya Damaro na sasa ametua alikotoka 'mbaya wake', lakini watetezi hao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), wanataka injini itakayozima mbele ya mabeki wao wa kati.
Conte alishindwa kuonyesha kiwango cha juu cha kukaba kwa ipasavyo pale kati, na kusukuma mashambulizi mbele kazi ambazo Damaro sio mgeni nazo akikaba kwa nguvu na kupiga pasi kusogeza timu eneo la wapinzani.
Damaro mtihani wake unatakiwa kuendeleza ubora alioanza kuuonyesha katika Kombe la Mapinduzi, ambapo atatakiwa kupigania nafasi kwa watu bora aliowakuta kina Duke Abuya na Mudathir Yahya ambao wana mizizi yao kwenye nafasi hiyo.
DUPE KAZI ANAYO
Jina lingine kubwa ambalo mashabiki wa Yanga wanasubiri kuona ubora wake ni Dupe, raia wa Angola, ambaye Yanga inamshusha akitokea Poland barani Ulaya alikokuwa anaichezea Radomial Radom.
Dupe kabla ya kutimkia Ulaya alikuwa mtu hatari mbele ya uso wa goli, anajua sana kuweka mpira wavuni. Ubora huo ndio anaoukumbuka Pedro ambaye alikuwa anakutana naye timu ya taifa la Angola.
Huo ni usajili wa Pedro moja kwa moja akitaka mshambuliaji atakayempa chaguo tofauti, na ubora alionao Dupe ambapo kuna uwezekano wa kuja kuona pacha ya Dupe na Dube au Dupe na Mzize. Hata hivyo, Dupe anatakiwa kutambua Yanga ilikuwa na Andy Boyeli kwa mkopo, lakini amerudi alikotoka Sekhukhune United ya Afrika Kusini.
Dupe alifunga bao moja na asisti mbili akiwa Radomial Radom, takwimu ambazo zinawatia unyonge Yanga, lakini wakiamini akili ya kocha kumrejeshea ubora wake.
OKELLO NAYE
Timu kubwa zote nchini zilikuwa zinamtakai fundi huyo wa mguu wa kushoto, Simba ikimuwinda kwa msimu wa pili na kuishia kumkosa. Azam FC nayo ilikuwa inampigia hesabu nyingi ikashindwa, huku Singida ikigomewa. Lakini, Yanga imebahatika baada ya raia huyo wa Uganda kukubali kufanya nayo kazi.
Okello anatua Yanga kama kiungo mshambuliaji namba 10, lakini pia chaguo la pili la matumizi yake ni kushambulia akitokea pembeni kulia akicheza nusu eneo (half space).
Okello ana takwimu nzuri anakotokea Vipers akiwa na mabao matatu na asisti nne msimu huu na staa pekee ambaye anaichezea timu ya taifa ya Uganda kati ya wachezaji waliosajiliwa na Yanga katika dirisha hili.
Presha kubwa kwake ni kuziba pengo lililoachwa na Stephanie Aziz KI ambaye alikuwa akizalisha pasi za mwisho, akiwa na ubunifu mkubwa majukumu ambayo Okello anaweza kuyafanya hata kufunga kwa mipira ya adhabu ndogo.
Katika usajili wa dirisha kubwa lililopita Yanga ilimsajili Mamadou Doumbia, lakini ameshindwa kuwaka haraka na sasa anadaiwa kutolewa kwa mkopo.
YAO, JESHI LINARUDI KAZINI
Kati ya wachezaji ambao Yanga imewaingiza katika usajili dirisha hili hakuna mwenye uhakika mbele ya mashabiki wa timu hiyo kama Yao Kouassi maarufu kwa jina la Jeshi. Hata hivyo, tangu alipokuwa nje ya uwanja akijiuguza kutokana na jeraha la mguuu pengo lake halikuonekana sana, Yanga ilisajili beki wa kazi, Israel Mwenda.
Yao anajua kukaba kwa nguvu na kupandisha mashambulizi, maana yake Yanga imevikutanisha vyuma viwili bora upande wa beki wa kulia.
MSIKIE PEDRO
Akizungumzia usajili, Pedro alisema wanaufanya kuboresha maeneo ambayo waliona yanatakiwa kuongezewa nguvu ambapo hawataki kuwa na mchezaji anayetua kikosini na kuishia kukubali matokeo k wa urahisi, akimaanisha msugua benchi.
“Tulikuwa tumeangalia maeneo ambayo tunaona yanahitaji kuongezewa nguvu kwa kutafuta watu wapya. Tunaamini watakuwa wachezaji wenye nishati kubwa. Kitu muhimu tunalenga kuwa na wachezaji watakaoweza kushindana kwa kufanya makubwa kwa ajili ya malengo ya timu na sio kuja kukubali kushindwa kirahisi,” alisema Pedro.