WE ACHA TU! Penalti 10 zinazouma zaidi kwenye mchezo wa soka
Muktasari:
- Kwanza, inaweza kumjenga mchezaji kwa kumpatia sifa endapo kama atafunga penalti muhimu, lakini pili inaweza kumbomoa na kumfanya aonekane mchezaji wa hovyo ndani ya sekunde chache tu.
LONDON, ENGLAND: MIKWAJU ya penalti hutengeneza nyakati zisizo na huruma kabisa katika mchezo wa soka.
Mambo mawili, yanaweza kumkuta mchezaji anayehusika kwenye kupiga mkwaju huo wa penalti.
Kwanza, inaweza kumjenga mchezaji kwa kumpatia sifa endapo kama atafunga penalti muhimu, lakini pili inaweza kumbomoa na kumfanya aonekane mchezaji wa hovyo ndani ya sekunde chache tu.
Kukosa penalti moja kunaweza kuumiza kwa miaka mingi, ikiwa ni tukio litakalobaki kwenye kumbukumbu ya zaman a zama kwa mchezaji husika na mashabiki.
Mfano mkwaju wa penalti wa Brahim Diaz kwenye fainali ya Kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) 2025 dhidi ya Senegal, unadhani mashabiki wa Morocco itabaki kwenye kumbukumbu yao kwa miaka mingapi?
Unadhani itabaki kwenye kumbukumbu za Diaz kwa miaka mingapi baada ya kukosa na kuifanya Morocco kushindwa kumaliza ukame wa kubeba taji hilo ndani ya ardhi ya kwao huku mara ya mwisho ikiwa imelibeba mwaka 1976?
Unaweza kupata hisia jinsi penalti inavyoweza kukupandisha au kukushusha. Na maumivu yake hasa unapokosa penalti muhimu.
Kuanzia fainali za Kombe la Dunia hadi usiku wa kukumbukwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, historia ya soka imejaa maumivu ya mikwaju ya penalti.
Wachezaji wa kimataifa kutoka Ufaransa, England, Italia, Misri na hata Ghana, wanaweza kukuambia jinsi wanavyotamani kurudi nyuma na kubadilisha kilichotokea baada ya kukosa mikwaju yao ya penalti kwenye mechi muhimu kabisa.
Hii hapa orodha ya penalti 10 zilizoumiza zaidi katika historia ya soka.
10 & 9. Kingsley Coman & Aurélien Tchouaméni – Fainali ya Kombe la Dunia 2022
Hakuna tofauti kubwa kati ya Coman na Tchouaméni, wawili hao walipata bahati mbaya katika mikwaju yao ya penalti katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2022.
Wote hawakuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa mwaka 2018, hivyo hiyo ilikuwa nafasi yao ya kunasa taji kubwa. Lakini, bado liliwakwepa.
Ni vigumu kudhani Coman, ambaye sasa anacheza Saudi Arabia, atapata nafasi nyingine kama hiyo, lakini Tchouameni bado anaweza kupata nafasi kadhaa zaidi.
Angalau wanaweza kujifariji kwa mafanikio makubwa katika klabu zao. Na kwa ujumla, ushiriki wa Ufaransa katika simulizi ya Kombe la Dunia la Qatar ulifunikwa haraka. Lakini, walikosa penalti zao dhidi ya Argentina na kumruhusu Lionel Messi na wenzake kunyakua taji hilo lenye hadhi kubwa kabisa.
8. Mohamed Salah – Mchujo Kombe la Dunia 2022
Mo Salah alifanya kosa kama la Ronaldo kwenye fainali ya AFCON 2021. Mfungaji bora na wa kuaminika zaidi wa penalti wa Misri alipangwa kupiga penalti ya tano, ambayo haikuwahi kufika. Kosa la kimsingi.
Hilo likapita na hatimaye, hatima ilipanga Misri ikutane tena na Senegal kwenye mechi ya mchujo wa Kombe la Dunia 2022 mwezi uliofuata.
Mfalme wa Misri wa Liverpool hakuwa tayari kuangalia kwa huzuni tena. Senegal walikosa penalti zao mbili za kwanza, lakini Salah alikuwa miongoni mwa Wamisri watatu walioshindwa kufunga.
Haikuwa bahati mbaya Salah alipomulikwa machoni kwa mwanga wa leza za kijani zilizokuwa zikimulikwa kutoka kwa mashabiki, alikosa mkwaju wake na kuiangusha Misri.
7. Jadon Sancho – Fainali Euro 2020
Matusi ya kibaguzi yaliyowalenga wachezaji watatu vijana Weusi baada ya kupoteza mikwaju ya penalti yaliweka kivuli kizito na cha aibu juu ya fainali ya Euro 2020, moja ya nyakati mbaya zaidi katika historia ya soka la England.
Winga wa mpira, Jadon Sancho anachukuliwa kama mfano mbele ya Marcus Rashford na Bukayo Saka kwa sababu ya athari kubwa tukio hilo lilikuwa nalo katika maisha yake ya soka.
Rashford na Saka bila shaka watacheza Kombe la Dunia lijalo, lakini Sancho hakuwahi kurejea kwenye kiwango chake.
Alijiunga na Manchester United kwa Pauni 73 milioni, lakini hakuwahi kufikia kiwango kikubwa alichoonyesha Borussia Dortmund.
Tangu akose penalti dhidi ya Italia, Sancho amevaa jezi ya England mara moja tu dhidi ya Andorra. Hata Patrick Bamford anaweza kujivunia hilo.
Wachezaji kama Tyrick Mitchell, Kyle Walker-Peters na Emile Smith Rowe wamecheza mechi nyingi zaidi kwa England katika miaka mitano iliyopita.
6. David Trezeguet – Fainali Kombe la Dunia 2006
Kuwa mkweli hukumbuki mara moja ni nani aliyekosa penalti ya Ufaransa mwaka 2006, sivyo?
Kwa bahati ya Trezeguet, tukio hilo limesahaulika kwa kiasi kikubwa kutokana tukio maarufu lililofanywa na Zinedine Zidane la kumpiga kichwa sehemu ya kifuani beki wa Italia, Marco Materazzi, tukio lililokuwa maarufu kuliko waliokosa penalti katika fainali hiyo ya Kombe la Dunia huko Ujerumani.
Zidane tayari alikuwa amefunga penalti ya panenka mapema na kama nahodha, angepiga penalti ya mwisho katika maisha yake ya soka. Lakini haikuwa hivyo.
Trezeguet tayari alikuwa na taji la Kombe la Dunia 1998. Kupata jingine lingekuwa zuri, lakini hilo lilipunguza maumivu ya kugonga mwamba wa juu wa lango Berlin.
5. John Terry – Fainali Ligi ya Mabingwa 2008
“Sikutakiwa hata kupiga moja ya penalti tano za kwanza, lakini Didier Drogba alikuwa ametolewa,” Terry aliambia FourFourTwo akitafakari kuteleza kwake maarufu kwenye mvua ya Moscow.
“Bado nafikiria kosa langu hadi leo. Sio mara nyingi kama zamani, lakini bado naota nalo.
“Taji ulilokosa linaweza kukuandama maisha yote. Sidhani kama nitawahi kulisahau.”
Hii ingefaaa kuwa namba moja kwenye penalti zinazouma zaidi baada ya kukosa kama Terry asingepata nafasi nyingine ya kushinda taji hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Ilinivunja kabisa. Nashukuru sana tulishinda 2012, ilinisaidia sana.”
4. Stuart Pearce – Nusu fainali Kombe la Dunia 1990
Hisia kali usoni mwa Pearce alipofunga penalti Euro 96 dhidi ya Hispania zinaeleza mzigo aliokuwa nao tangu kukosa Turin 1990.
“Kushindwa kwangu kusingekuwa kukosa tena,” alisema.
“Kushindwa kungekuwa kutojaribu.”
Moyo wa chuma. Hata hivyo, tukio hilo linabaki kwenye kumbukumbu za kudumu za Pearce kutokana na mkwaju aliokosa na kuigharimu timu yake.
3. Gareth Southgate – Nusu fainali Euro 96
Mikwaju ya penalti ilikuwa bado mipya miaka ya 90. England bado hawakuwa na hofu ya kisaikolojia kuhusu penalti walipoandaa Euro 96.
Ndiyo, kulikuwa na Italia 1990, lakini England waliwashinda Hispania kwa penalti zote kwenye robo fainali na wakafunga penalti tano za kwanza dhidi ya Ujerumani. Tatizo? Wajerumani pia walifanya hivyo.
Chanzo cha janga la penalti la England kinaweza kufuatiliwa hadi pale Southgate alipokosa penalti ya ghafla Wembley.
England walipoteza mikwaju minne mfululizo ya mashindano makubwa kabla ya kuvunja laana hiyo dhidi ya Colombia mwaka 2018, Southgate akiwa kocha. Soka lina mashairi yake, sivyo?
2. Brahim Díaz – Fainali AFCON 2025
Pengine ni upendeleo wa ukaribu wa tukio, lakini hili linaingia moja kwa moja katika historia.
Fainali kubwa. Nyumbani. Taifa limesubiri zaidi ya miaka 50 kushinda taji hili.
Umecheza mashindano bora na una nafasi ya kufunga penalti ya ushindi dakika za mwisho za majeruhi.
Halafu unafanya hivi. Sio tu panenka iliyoshindikana, lakini iliyopigwa kwa udhaifu kiasi kwamba mitandao ya kijamii ilijaa tetesi kuwa alikosa makusudi. Maumivu makubwa. Ushindi wa Senegal katika muda wa nyongeza ulionekana hauepukiki baada ya hapo.
1. Roberto Baggio – Fainali Kombe la Dunia 1994
Hili ndilo kosa la penalti linalouma zaidi kuwahi kutokea. Jukwaa halikuwa kubwa zaidi ya hapo.
Hakuna anayeweza kuelezea maumivu hayo vizuri kuliko Baggio mwenyewe.
“Kama ningekuwa na kisu wakati huo, ningejidunga,” alisema katika mahojiano na The Athletic. “Kama ningekuwa na bunduki, ningejipiga risasi. Wakati huo nilitaka kufa. Ndivyo ilivyokuwa.”