Wazee wa mboga saba waliokinukisha dimbani

Muktasari:
- Hata hivyo, sio wachezaji wote ambao wametokea katika maisha duni na walipambana ili kubadilisha hali ya umaskini iliyokuwa inawaandama wao na familia yao, kuna mastaa wa soka ambao kabla ya kuwa wachezaji wakubwa tayari walishakuwa na maisha mazuri kutokana na familia zao walizotokea.
ROTTERDAM, UHOLANZI: WACHEZAJI wengi wa soka wamebadilisha maisha yao kupitia soka. Wengi wametokea katika maisha ya chini na walipambana kadri wanavyoweza kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.
Hata hivyo, sio wachezaji wote ambao wametokea katika maisha duni na walipambana ili kubadilisha hali ya umaskini iliyokuwa inawaandama wao na familia yao, kuna mastaa wa soka ambao kabla ya kuwa wachezaji wakubwa tayari walishakuwa na maisha mazuri kutokana na familia zao walizotokea.
Hapa kuna orodha ya wachezaji watano ambao bila hata ya mpira wa miguu bado walikuwa na maisha mazuri kutokana na utajiri wa familia walizotoka.
ROBIN VAN PERSIE
Van Persie alikulia Rotterdam, Uholanzi akitokea katika familia ya kitajiri na ya kisanii. Baba yake, Bob, ni msanii maarufu na mchora sanamu, huku mama yake, Jose Ras, akiwa mchora picha, mwalimu, na mbunifu wa vito vya thamani.
Licha ya malezi haya ya kifahari, Van Persie alikutana na upinzani kutoka kwa wazazi wake ambao walihitaji aendelee kusoma na kufanya kazi tofauti na mpira wa miguu, lakini yeye aliendelea kushikilia msimamo huo.
GERRARD PIQUE
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana, Kevin Prince Boateng, aliwahi kusema sio tu, kuwa na maisha mazuri, Pique hata alipokuwa akicheza Barcelona alikuwa akicheza kama mfanyabiashara, hakuwa anaweza kuingiza mguu sehemu ambayo aliona kama ni hatari kwa afya yake, alicheza kiungalifu sana.
Staa huyu ambaye alikulia Catalonia, baba yake alikuwa ni wakili na mjasiriamali maarufu, huku mama yake, Montserrat, akiwa mkurugenzi wa hospitali huko Barcelona.
Vilevile babu yake, Amador Bernabeu, aliwahi kuwa makamu wa rais wa Barcelona.
HUGO LlORIS
Kipa huyu wa zamani wa Tottenham na timu ya taifa ya Ufaransa, alizaliwa huko Nice, Ufaransa ba ni mmoja kati ya wachezaji ambao hawakuwa na maisha ya tabu hata kidogo katika ukuaji wao.
Baba wa kipa huyu mzee Luc alikuwa ni mfanyabiashara ambaye alijikita katika uwekezaji wa kununua hisa katika benki mbalimbali.
Vilevile mama yake Marie alikuwa ni mwanasheria mwenye kampuni maarufu.
Alipokuwa mtoto alikuwa akicheza sana mchezo wa tenisi kabla ya kuhamia katika soka.
RICARDO KAKA
Staa huyu wa zamani wa kimataifa wa Brazil ambaye alizaliwa huko Ricardo Izecson dos Santos, Brazil, aliishi maisha ya kifahari tangu akiwa na umri mdogo.
Baba mzazi wa fundi huyu Bosco Izecson alikuwa akifanya kazi kama injinia maarufu huko Brazil na mama yake alikuwa ni mwalimu wa shule.
Licha ya utajiri wa familia yake, Kaka amejikunjia kiasi kikubwa cha pesa kupitia soka akikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 50 milioni.
ANDREA PIRLO
Wakati Andrea Pirlo anakua, baba yake alikuwa ni mwanzilishi wa kampuni ya uchakataji wa madini ya chuma huko Brescia mwaka 1982 inayoitwa Elg Steel ambayo inaripotiwa kuingiza mauzo ya zaidi ya Pauni 60 milioni kwa mwaka na kwa sasa Pirlo mwenyewe anamiliki hisa katika kampuni hiyo.
Baba wa Pirlo alitarajia kwamba mtoto wake angejiingiza katika biashara ya familia na uamuzi wake wa kuamua kucheza soka haikumpendeza kwa wakati huo lakini kwa sababu aling’ang’ania kufanya hivyo alimwacha afuate ndoto zake.