Wawa: Morison na Luis walinisumbua sana

Friday October 22 2021
waawaa pic
By Saddam Sadick

MSIMU uliopita beki wa kulia wa Dodoma Jiji, George Wawa alikuwa miongoni mwa wachezaji walioweka rekodi tamu ya kucheza mechi nyingi zaidi (29) sawa na dakika 2,610 huku akimtaja winga machachari wa Simba, Benard Morison kumpa wakati mgumu.

Wawa ambaye alisajiliwa Dodoma Jiji misimu miwili iliyopita akitokea Singida United iliyoshuka daraja, amekuwa nguzo muhimu katika timu hiyo ya makao makuu ya nchi akiisaidia zaidi katika mafanikio iliyonayo uwanjani.

Beki huyo ambaye hadi sasa amecheza mechi tatu mfululizo za msimu huu, anaelezea ugumu alioupata, mchezaji aliyemsumbua uwanjani, mipango na mikakati ya msimu huu.

Wawa anasema pamoja na mafanikio ya kucheza mechi nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine kikosini, lakini haikuwa kazi rahisi kutokana na ushindani ulivyokuwa.

Anasema katika mechi hizo hawezi kuwasahau nyota wa Simba, Morison na Luis Miquissone ambao walimpa ugumu kwa nyakati tofauti lakini alipambana nao.

“Nilikosa mechi tano tu msimu uliopita, lakini haikuwa kazi nyepesi ilikuwa ni vita kali sana. Kuna wachezaji - Luis na Morison walinipa upinzani lakini walinikuta na mimi siyo wa mchezomchezo,” anasema Wawa.

Advertisement

Hata hivyo, nyota huyo anasema kuwa pamoja na vita aliyokutana nayo kwa wachezaji hao, amejipanga vyema msimu huu kuwadhibiti watukutu uwanjani.

Anasema siri ya kujihakikishia namba kikosini ni kujituma, lakini pia mipango ya benchi la ufundi kutegemeana na aina ya mchezo na kwamba hata msimu huu amejipanga kuendeleza alipoishia.

Anasema kuwa anafahamu msimu huu vita itakuwa kali zaidi, lakini kutokana na maandalizi waliyonayo hana wasiwasi na kazi yake na kwamba, matamanio yake ni kuona Dodoma Jiji ikimaliza katika nafasi nne za juu.

Anasema kinachompa matumaini na nguvu kutamba ni kutokana na muunganiko, umoja na ushirikiano kikosini kwa kila mmoja kuipigania timu na kwamba lazima msimu huu wafanye kweli.

“Kwa sasa mipango ni kuendeleza palepale nilipoishia. Natamani kuona timu yangu ikifika mbali hasa kumaliza nafasi nne za juu. Kinachonipa morari ni uwajibikaji wa kila mmoja kwa nafasi yake,” anasema beki huyo.

Mchambuzi wa soka jijini Mbeya, Deogratias Mwakyusa anasema kuwa kuaminiwa kwa mchezaji kupewa nafasi katika mechi zote za ligi inatokana na utayari wake kuonyesha kitu tofauti cha kumshawishi kocha.

Anasema kutokana na mafanikio kwa beki huyo, anapaswa kupambana msimu huu bila kulewa sifa au kubweteka na nafasi hiyo kwani upinzani ni mkali ambapo kila timu inahitaji matokeo mazuri.

Wawa anasema tangu aanze kumfuatilia mchezaji huyo amekubali ubora wake na kwamba, ni miongoni mwa mabeki wenye uwezo awapo uwanjani akifanya kazi yake kwa ufanisi.

“Wawa amekuwa mmoja wa mabeki wenye uwezo na pengine amekuwa na uhakika wa namba kutokana na kitu cha tofauti alichonacho. Kimsingi asilewe sifa bali apambane atafika mbali,” anasema Mwakyusa.

Advertisement