Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wapinzani wa timu nne Bara CAF katika namba

Muktasari:

  • Ni Simba na Yanga ambao watapeperusha bendera ya kimataifa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao wataanzia nyumbani wakati Mnyama akivaana na Petro Atletico de Luanda ya Angola kati ya Novemba 21-23 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa ilhali Wananchi watakuwa Zanzibar kukabiliana na AS FAR ya Morocco kwenye Uwanja wa Amaan.

BAADA ya kalenda ya Fifa, wachezaji wa Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars wanatarajiwa kurejea fasta kwenye klabu zao kwa ajili ya maandalizi ya wiki ya kwanza ngumu ya michuano ya kimataifa, lakini kuna ambao wataanzia nyumbani huku wengine wakiwa na kibarua cha kucheza ugenini.

Ni Simba na Yanga ambao watapeperusha bendera ya kimataifa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao wataanzia nyumbani wakati Mnyama akivaana na Petro Atletico de Luanda ya Angola kati ya Novemba 21-23 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa ilhali Wananchi watakuwa Zanzibar kukabiliana na AS FAR ya Morocco kwenye Uwanja wa Amaan.

Azam na Singida Black Stars upande wa Kombe la Shirikisho Afrika wao, mmoja atakuwa Kindu huko DR Congo kucheza dhidi ya AS Maniema Union huku mwingine akiwa Algiers, Algeria kucheza dhidi ya CR Belouizdad.

Itakuwa ni wikiendi ya moto kwa wawakilishi hao wa Tanzania ambao watakuwa wakisaka rekodi nyingine tamu katika michuano ya CAF ikiwa ni wiki chache tangu waweke rekodi ambapo ni kwa mara ya kwanza timu nne kutoka taifa moja la ukanda wa Afrika Mashariki kutinga hatua ya makundi.

Rekodi nyingine ambayo itakuwa ikisakwa katika hatua ya makundi ni timu zote nne kwa mpigo kufuzu robo fainali, na kabla ya hilo, makala hii inaletea undani mechi hizo za kwanza katika hatua ya makundi huku ikijikita katika rekodi.


SIMBA vs PETRO ATLETICO

Kati ya timu zenye rekodi nzuri nyumbani kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni pamoja na Simba, msimu uliopita katika Kombe la Shirikisho Afrika ilikuwa na asilimia 85.7 ya ushindi nyumbani hivyo wikiendi ijayo itakuwa na kibarua cha kuendeleza hilo katika michuano ya CAF.

Simba ikiwa nyumbani msimu uliopita ilishinda mechi sita kati ya saba (moja ilitoa sare ilikuwa ni fainali ya pili), katika sita ilizoshinda, moja ilikuwa katika hatua ya awali dhidi ya Al Ahli Tripoli (3-1), tatu hatua ya makundi dhidi ya Bravos do Maquis (1-0), CS Sfaxien (2-1), CS Constantine (2-0).

Huku upande wa mtoano, robo ikiichapa Al Masry kwa mabao 2-0, nusu iliichapa Stellenbosch (1-0) huku fainali ikitoa sare ya bao 1-1 RS Berkane, msimu huu Simba katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa imeshinda na kutoa suluhu.

Simba imeshinda bao 1-0 ikiwa nyumbani dhidi ya Gaborone United ya Botswana na kutoa suluhu dhidi ya Nsingizini Hotspurs baada ya kumaliza kazi Eswatini. Wakati Simba ikionekana kuwa moto wa kuotea mbali nyumbani hasa, kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, mpinzani wake, Petro de Luanda sio timu ya kubezwa.

Tofauti na Simba ambayo katika mechi za awali imeruhusu bao moja, Petro de Luanda yenyewe haijaruhusu bao na imeshinda mechi zote mbili ambazo ilicheza ugenini, iliitandika Cercle de Joachim huko  Mauritania mabao 3-0 kisha  Stade d’Abidjan huko Ivory Coast mabao 2-0.

Rekodi zao ugenini zinaonyesha katika msimu wa 2021–22 ambao walifika hadi nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, katika mechi zao mbili za awali ikiwa ugenini ilitoa sare ya mabao 2-2 kwenye kila mechi dhidi ya Fovu de Baham huko Cameroon na AS Otoho, Congo.

Katika hatua ya makundi ilitoa sare tena ikiwa ugenini ya mabao 2-2 dhidi ya Zamalek, iliwafunga Waangola wenzao, Sagrada Esperança kwa bao 1-0 na wakakumbana na kipigo kizito cha mabao 5-1 huko Morocco mbele ya Wydad Casablanca ambayo kwa sasa anaichezea Stephane Aziz KI.

Katika robo fainali, ilitoa sare ya 1-1 na Mamelodi Sundowns na kuwang’oa katika michuano hiyo lakini ilikiona cha moto tena mbele ya Wydad Casablanca katika hatua ya nusu fainali licha ya kutoa sare ugenini ya bao 1-1 ikiwa ni mechi ya marudiano, ilichapwa katika mechi ya kwanza kwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani Angola. Hivyo pamoja na ubora wao ni timu inayofungika.


YANGA vs AS FAR

Rekodi zinaonyesha katika mechi nane zilizopita, Yanga ikiwa nyumbani katika Ligi ya Mabingwa Afrika, imeshinda mechi sita, sare moja na kupoteza mara moja.

Msimu uliopita 2024/25, Yanga ikiwa nyumbani iliifunga Vital’O ya Burundi katika hatua ya awali kwa mabao 6-0, katika hatua iliyofuata timu hiyo ya Wananchi iliendeleza dozi hiyo kwa CBE ya Ethiopia mabao 6-0 na kutinga kibabe hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo.

Katika hatua ya makundi Yanga ilipoteza mechi moja nyumbani dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwa mabao 2-0, ikaichapa TP Mazembe kwa mabao 3-1 na kutoa suluhu dhidi ya MC Alger ya Algeria, hivyo msimu uliopita ambapo iliishia hatua ya makundi ikiwa nyumbani ilikuwa na rekodi ya ushindi kwa asilimia 66.6. 

Msimu huu, Yanga imeshinda mechi zote mbili za awali ikiwa nyumbani kwa mabao 2-0 kwenye kila mechi dhidi ya Wiliete na Silver Strikers. Wakati rekodi ya Yanga ikiwa hivyo, AS FAR ambayo msimu uliopita ilifika robo fainali ya michuano hiyo.

Katika mechi ya kwanza kwa AS FAR msimu uliopita ikiwa ugenini, ilichapwa dhidi ya Remo Stars ya Nigeria kwa mabao 2-1 pamoja na kwamba ilivuka hatua hiyo kwa jumla ya mabao 3-2, katika hatua ya pili, ilitoa sare ya mabao 2-2 huko Sudan dhidi ya Al Merrikh na kutinga hatua ya makundi.

Licha ya kumaliza kinara wa kundi B ikiwa na pointi 10, AS FAR ilishinda mechi moja tu ugenini katika hatua hiyo na ilikuwa dhidi ya ndugu zao wa nchini kwao, Morocco, Raja Casablanca kwa mabao 2-0, walitoa sare mbili ya bao 1-1 katika kila mechi dhidi ya AS Maniema Union na Mamelodi Sundowns.

Katika hatua ya robo fainali ambayo safari yao iliishia, ilichapwa mabao 4-1 na Pyramids anayoichezea Fiston Mayele. Kwa msimu huu wababe hao, walishinda mechi ya kwanza huko Gambia kwa mabao 2-0 dhidi ya Real de Banjul na hatua ya pili wakatoa sare ya bao 1-1 huko Guinea dhidi ya Horoya, hivyo Yanga inatakiwa kuwa macho na mechi hiyo.


CR BELOUIZDAD vs SINGIDA BS

Singida Black Stars ambayo hii ni mara yake ya kwanza kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, haina rekodi ya kupoteza ugenini, imecheza mechi mbili tu na ilikuwa katika hatua ya awali iliibuka na ushindi wa bao 1-0 Rwanda dhidi ya Rayon Sports kisha ikatoka sare ya bao 1-1 huko Burundi dhidi ya Flambeau du Centre.

Hiki ni kibarua kingine kabisa tofauti na mechi za awali imecheza. Unaweza kusema ni kama Singida BS ilikuwa fungate na sasa maisha ya ndoa ndio yanaanza hivyo wanatakiwa kuwa tayari kukabiliana na changamoto zake.

CR Belouizdad ni timu yenye uzoefu wa kutosha na michuano hii ya kimataifa, rekodi yao nyumbani inaonyesha katika mechi tano zilizopita nyumbani, imeshinda nne na kutoa sare moja.

Katika hatua ya awali yenyewe ilianzia raundi ya pili ikiwa nyumbani iliitandika Hafia ya Guinea mabao 2-0 baada ya kutoa sare kwenye mechi ya kwanza na kutinga hatua ya makundi.

Timu hiyo inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic msimu wa 2023–24 ilicheza Ligi ya Mabingwa Afrika na katika hatua ya awali ikiwa nyumbani iliichapa Bo Rangers ya Jamhuri ya Sierra Leone kwa mabao 3-1 na kutinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-2.

Katika hatua hiyo, ambayo ilipangwa kundi moja (D) na Yanga, licha ya kushinda mechi zao mbili nyumbani kwa mabao 3-0 katika kila mechi dhidi ya Yanga na Medeama ya Ghana, ikatoa suluhu moja dhidi ya Al Ahly, iliishia hatua ya makundi ikishika nafasi ya tatu kwa pointi nane huku Yanga ambayo nayo ilikuwa na pointi nane na Al Ahly iliyoongoza kundi ikiwa na pointi 12 zikitinga robo fainali za michuano hiyo. 


MANIEMA UNION vs AZAM

Azam ikiwa chini ya kocha Florent Ibenge, imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika bila ya kuruhusu bao, ikishinda mechi zote nyumbani na hata ugenini, iliichapa El Merreikh Bentiu huko Sudan Kusin mabao 2-0 na katika raundi ya pili ya hatua hiyo ya awali ikawanyuka tena maafande wa KMKM huko Zanzibar kwa mabao 2-0.

Hivyo Azam inaenda Kindu huko Kongo kujaribu kile ilichofanya katika hatua ya awali, mpinzani wao, AS Maniema Union yenyewe katika hatua ya awali ikiwa nyumbani iliichapa Pamplemousses ya Mauritania mabao 2-1 na katika hatua ya pili ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Royal Leopards ya Eswatini.

Tofauti na Azam ambayo haikuruhusu bao ikiwa ugenini, AS Maniema Union ambayo itakuwa nyumbani rekodi zake zinaonyesha imeruhusu mabao mawili licha ya kwamba hakuna mechi iliyopoteza katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi. Hii ni mara yao ya kwanza kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kama ilivyo kwa Azam tu.

Pamoja na kwamba hii ni mara yao ya kwanza upande wa Shirikisho, upande wa Ligi ya Mabingwa, ilicheza hatua ya makundi msimu uliopita wa 2024–25 na rekodi zao nyumbani zinaonyesha, ilishinda mechi moja, sare mbili na kupigwa mara moja.

Katika hatua ya awali ilitoa suluhu dhidi ya Ngezi Platinum ya Zimbabwe na kuichapa Petro de Luanda ya Angola mabao 2-1, ikiwa kundi B iliburuza mkia ilitoa sare mbili nyumbani kwa bao 1-1 na AS FAR na Raja Casablanca huku ikifungwa mabao 2-1 na Mamelodi Sundowns.