Hatma ya Prisons, Mbeya City kuondoka, kubaki Ligi Kuu leo
Muktasari:
- Hii ni baada ya timu hizo za jijini Mbeya kumaliza Ligi Kuu msimu wa 2025/26 ikiwa Prisons nafasi ya 13 kwa pointi 32, huku City wakiwa nafasi ya 14 kwa pointi 30 na sasa ni jasho na damu kukwepa kushuka daraja.
HESABU zinaanza leo. Ndivyo unaweza kusema kuelezea mtifuano wa Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa hatua ya kwanza ya mchujo (play off) kusaka nafasi ya kubaki salama Ligi Kuu.
Hii ni baada ya timu hizo za jijini Mbeya kumaliza Ligi Kuu msimu wa 2025/26 ikiwa Prisons nafasi ya 13 kwa pointi 32, huku City wakiwa nafasi ya 14 kwa pointi 30 na sasa ni jasho na damu kukwepa kushuka daraja.
Kutokana na matokeo hayo, wadau na mashabiki wa soka jijini Mbeya wamekuwa na mitazamo tofuati juu ya soka la mkoani humo wakitaja kiini cha tatizo na kushauri cha kufanya ili kuondokana na presha ndani ya uwanja.
Katika Ligi hiyo iliyomalizika Juni 30, Yanga ilitetea ubingwa wake wa tano mfululizo kwa pointi 77, huku Mtibwa Sugar na KMC zikishuka daraja moja kwa moja baada ya kukusanya pointi 27 kwa tisa.
Hata hivyo, timu hizo zinacheza mchujo kwa mara ya pili ambapo Mbeya City inakumbuka rekodi mbaya ilipokutana na Mashujaa iliyokuwa Championship na kuondoshwa kwa jumla ya mabao 3-1 na kushuka daraja msimu wa 2022/23.
Kwa Prisons walicheza mchujo msimu wa 2021/22 dhidi ya JKT Tanzania iliyokuwa Championship na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, na kukwepa aibu ya kushuka daraja na sasa inakwenda kujiuliza tena.
Kama haitoshi, utamu wa mchezo huo utakaopigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, unazikutanisha timu hizo kwa mara ya kwanza katika historia ya play off na mara ya tatu msimu huu kila timu ikiwa na hesabu zake.
Katika michezo miwili ya kwenye ligi kukutana timu hizo, kila upande umeshinda mchezo mmoja na sasa zinatkutana tena katika 180 kujua nani atabaki salama au kusubiri dakika nyingine 180 dhidi ya timu ya Championship.
Iko hivi, baada ya michezo miwili kwa timu hizo, yoyote itakayoshinda itabaki Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku itakayofungwa itakutana na mshindi kati ya Polisi Tanzania na Mbeya Kwanza za Championship na matokeo kuamua.
Rekodi ya timu hizo
Kwa takribani misimu mitano sasa timu hizo zimekuwa na matokeo yasiyoridhisha na kuweka presha kwa wadau na mashabiki wa soka jijini Mbeya kutokana na mwenendo mbovu wa matokeo.
Ikumbukwe kuwa Mbeya City iliyowahi kufanya vizuri na kumaliza nafasi tatu za juu msimu wa 2013/14 ikiwa ni mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu, ilijivunia nguvu ya mashabiki na kuweka heshima kwake na jiji la Mbeya kwa ujumla.
Hata hivyo baada ya kudumu zaidi ya miaka 10 Ligi Kuu, ilijikuta ikishuka daraja msimu wa 2022/23 kupitia mchujo na kucheza Championship misimu miwili kabla ya kurejea msimu huu na kujikuta kwenye presha.
Timu hizo zimekuwa katika presha kubwa ya matokeo na kujikuta zikisubiri miujiza na huruma ya michezo ya mwisho kuweza kubaki salama na msimu huu hali si shwari.
Timuatimua makocha
Wakati timu hizo zikikutana katika mchezo huo kila upande unakumbukwa kwa kutema makocha ambapo Mbeya City imeajiri watatu kuinoa hadi sasa, huku Prisons ikiajiri wawili.
City ilianza msimu na aliyekuwa Kocha Mkuu, Malale Hamsini kabla ya kumtema na kumvuta Mecky Maxime ambaye naye alikutana na mkono wa kwakheri na sasa ni Mayanga.
Mayanga aliyetua kikosini humo akiwa huru baada ya kuachana na Mahujaa, ameiongoza timu hiyo michezo 10 akishinda michezo mitatu, sare tatu na kupoteza minne na kumaliza ligi nafasi ya 14 kwa pointi 30.
Kwa upande wa Tanzania Prisons ilianza Ligi chini ya kocha raia wa Kenya, Zedekiah Otieno kabla ya mambo kumbadilikia na kumpiga chini na nafasi yake kuzibwa na Nsajigwa aliyepo hadi sasa.
Nsajigwa aliyetua kwa Maafande kutokea Transit Camp ya Championship, ameiongoza timu hiyo michezo 16, akishinda saba, sare mbili na kupoteza saba na kumaliza ligi nafasi ya 13 kwa pointi 32.
Tatizo liko hapa
Mabadiliko ya mara kwa mara kwa viongozi na baadhi yao kutokuwa na uwezo na uzoefu wa soka umetajwa kuliangusha soka la Mbeya, huku wadau wakitaka kila timu kufanya tathimini binafsi kama kila mmoja anatosha kwenye nafasi yake.
Mbeya City tangu ilipopanda Ligi Kuu ilikuwa chini ya Mtendaji Mkuu, Emanuel Kimbe aliyeiongoza kwa takribani miaka 10 kabla ya kung’atuka waliposhuka daraja na kuikabidhi kwa wengine.
Timu hiyo inayomilikiwa na Halamashauri ya Jiji la Mbeya, baadaye ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Mchumi wa Jiji, Ally Nnunduma ambaye aliipandisha Ligi Kuu na kusimamia michezo mitatu wakivuna pointi 10.
Baadaye Nnunduma aliyeonekana kuwa kipenzi cha mashabiki wengi wakimtaja kuwa kiongozi aliyeiwezea timu hiyo, alihamishwa kituo cha kazi na kupandishwa cheo kuwa Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu sehemu ya Sera, Utafiti na Ubunifu.
Kwa sasa timu hiyo inaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), John Kilua ambaye pia ni Afisa Uhusiano na Mawasiliano Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambaye ameiongoza kwa michezo takribani 27.
Tanzania Prisons ilianza msimu na Ofisa Mtendaji Mkuu, Godfrey Madegwa aliyeiongoza kwa zaidi ya mechi 15, kisha kumpisha Ajab Kifukwe aliyepo hadi sasa.
Wilbert Mwampamba anasema mabadiliko ya mara kwa mara kwa ya uongozi kwenye timu hizo ni sababu mojawapo ya anguko kwao akieleza kuwa lazima kuwepo tathimini binafsi kwa uongozi.
“Lakini lazima kuwepo muunganiko wa uongozi badala ya kila muda kupishana watendaji, haiwezi kuleta ufanisi kwa timu, lakini wapo baadhi uwezo wao kuongoza mpira bado, wangepewa muda kujifunza,” anasema Mwampamba.
Naye Dickson Mwampashe anasema mkoa huo umepata aibu kwa timu zake kuangukia mtoano akieleza kuwa wanachoshukuru ni kuwa na uhakika wa mmojawapo kubaki salama Ligi Kuu. “Pamoja na kwamba tuna uhakika wa timu Ligi Kuu msimu ujao, lakini iwe chama cha Soka, viongozi wa timu lazima wajitathimini haiwezakani tuzidiwe na mikoa yenye timu moja iwe salama, sisi twende play off,” anasema Mwampashe.
Kauli za makocha
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shedrack Nsajigwa anasema kwa matokeo waliyoanza nayo walijiandaa kwa lolote na kwamba ushindi wa mechi tano kati ya sita za ligi zimerejesha tumaini jipya.
Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga anasema mchezo huo una presha kubwa kwa kuwa wanahitaji kubaki salama Ligi Kuu, akieleza kuwa wamekuwa na siku tatu nzuri za maandalizi ya ushindi.
“Vijana wote wako fiti na tayari kwa mchezo huo,” anasema.