Wamekumbuka shuka tayari kumekucha

Thursday June 23 2022
shuka pic
By Daudi Elibahati

MSIMU wa Ligi Kuu Bara umekaribia mwisho kwa baadhi ya timu kubakisha michezo mitatu na nyingine miwili.

Ni msimu 2021/22 umeshuhudia baadhi ya mastaa wakikiwasha kinoma tangu mwanzo, huku wengine wakikata moto mapema na hadi unatamatika Juni 29, wapo wengine walioamka kuanzia mzunguko wa pili wa ligi na wanakiwasha sana.

Mwanaspoti linakuletea kwa kina nyota hao ambao kwa sasa viwango vyao vipo juu ingawa wamechelewa kuonyesha moto wao.


JEREMIAH JUMA (TANZANIA PRISONS)

Ndiye mchezaji pekee aliyefunga mabao matatu ‘Hat trick’ katika mchezo mmoja, alipoifunga Namungo Novemba 27, 2021 na kufikisha mabao matano.

Advertisement

Hata hivyo, baada ya hapo alichukua muda mrefu tena kufunga alipofanya hivyo dhidi ya Geita Gold Mei 26, 2022 kwenye sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sokoine na kuandika bao la sita.

Hakuishia hapo Juni 14 alifunga bao lake la saba dhidi ya KMC, kwenye sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru.


JOHN BOCCO (SIMBA)

Bocco ndiye mfungaji bora msimu uliopita akipachika mabao 16, lakini alianza vibaya kwa kutokufunga bao lolote hadi alipoanza kufungua ukurasa wa mabao dhidi ya Ruvu Shooting Mei 8, Kagera Sugar Mei 11 na Azam Mei 18 na kufikisha mabao matatu baada ya ukame uliomkuta tangu alipoifunga Namungo Julai 18, 2021.


MATHEO ANTHONY (KMC)

Nyota huyu aliibuka alipofunga mabao mawili kwenye ushindi wa 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar Mei 12, mwaka huu na kufikisha mabao sita baada ya kuandamwa na ukame tangu alipofunga mara ya mwisho dhidi ya Mbeya Kwanza, Januari 21, 2022.

Hakuishia hapo aliendeleza moto kwa kufunga tena bao lake la nane wakati KMC iliposhinda 3-0 dhidi ya Mbeya City Mei 19, 2022.

Aliendelea tena kufanya vizuri alipofunga bao lake la tisa msimu huu wakati timu yake ilipofungana bao 1-1 na Tanzania Prisons Juni 14.


YUSUPH MHILU (SIMBA)

Tangu ajiunge na Simba msimu huu akitoea Kagera Sugar alipofunga mabao tisa, mshambuliaji huyo bado hajafunga ingawa alitoa pasi ya bao la tatu kwa John Bocco kwenye ushindi wa timu hiyo wa 4-0, dhidi ya Ruvu Shooting Mei 8, 2021.


SHIZA KICHUYA (NAMUNGO)

Alianza msimu kwa kasi na mchezo wa kwanza mbele ya Geita Gold, Septemba 27, 2021 alifunga bao la kwanza kwenye ligi wakishinda 2-0, ila baada ya hapo alimaliza mzunguko wa kwanza kwa kusuasua.

Mzunguko wa pili alifunga bao kali dhidi ya Yanga Aprili 23, licha ya Namungo kufungwa mabao 2-1, kisha akafunga mawili dhidi ya Biashara United Mei 17 na kufikisha jumla ya matatu sambamba na nyota wenzake Obrey Chirwa.


HERITIER MAKAMBO (YANGA)

Mei 20, mwaka huu, alianza kufungua rasmi ukurasa wa mabao alipofunga bao la kwanza la msimu dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye ushindi wa timu hiyo wa 4-0, baada ya kupitia kipindi kigumu kilichozua maswali mengi.


PRINCE DUBE (AZAM FC)

Msimu huu haukuwa mzuri kwake tofauti na msimu uliopita alipofunga mabao 14, kwani hadi sasa ni bao moja alilofunga Machi 16, 2022, wakati timu yake ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Ilulu.


DICKSON AMBUNDO (YANGA)

Nyota huyu aliweza kutupia bao lake la kwanza mbele ya Polisi Tanzania Januari 23, 2022 kisha ikabidi asubiri hadi Mei 15, alipofunga dhidi ya Dodoma Jiji kwa shuti kali wakati Yanga ikishinda mabao 2-0.

Akaendeleza moto wake kwa kufunga tena Mei 20, mwaka huu Yanga ikishinda 4-0 mbele ya Mbeya Kwanza.


SALUM ABUBAKAR ‘SURE BOY’ (YANGA)

Mei 20, mwaka huu aliweza kutoa pasi ya bao la kwanza la Fiston Mayele wakati Yanga ikishinda mabao 4-0 dhidi ya Mbeya Kwanza na kiwango chake kikiimarika zaidi tofauti na alivyoanza msimu akitokea Azam.

Advertisement