Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WAMEDATISHWA: Kwa pisi za Kibongo, wamezama mazima!

Muktasari:

  • Mwanahawa alitoa kibao hicho miaka mingi iliyopita, lakini hadi wakati huu kinafanya vizuri kwa kuwa kilichoimbwa ndiyo sifa ya mapenzi yenyewe. Mtu anapopenda huwa haangalii rangi ya ampendae, dini, kabila wala nchi anayotokea ambaye moyo na nafsi yake kwa wakati huo vinakuwa vimeshapenda.

KATIKA moja ya utenzi wake gwiji wa kughani mashairi ya taarabu nchini, Mwanahawa Ally aliwahi kusifia mapenzi kwa kuyapa sifa ya majani, kwamba yenyewe hayachagui pa kuota.

Mwanahawa alitoa kibao hicho miaka mingi iliyopita, lakini hadi wakati huu kinafanya vizuri kwa kuwa kilichoimbwa ndiyo sifa ya mapenzi yenyewe. Mtu anapopenda huwa haangalii rangi ya ampendae, dini, kabila wala nchi anayotokea ambaye moyo na nafsi yake kwa wakati huo vinakuwa vimeshapenda.

Kwenye mapenzi sio ajabu watu wa makabila, lafudhi au hadhi tofauti kupendana na hatimaye kuoana. Yenyewe hayana kitu ambacho mtu anaweza kusema hiki ni maalumu kwa ajili ya mtu kupenda. Pia sio ajabu kuona kijana wa Kibongo akiwa na mpenzi raia wa kigeni kutoka mataifa ya Ulaya au raia wa kigeni kuja Bongo kisha kuanzisha mahusiano na mwanamke wa Kitanzania.

Kuna wageni wengi ambao wamewahi kufika Tanzania kisha wakaanzisha mahusiano na mabinti wa hapa. Kuna wale ambao hawajulikani, lakini pia kuna mastaa wa mbalimbali wa soka ambao wameiteka jamii ya Kitanzania kutokana na 'couple' zao baada ya kuanza safari moja ya mpira wakajikuta wameanza nyingine ya mapenzi.

Mwanaspoti linakuletea nyota sita waliokuja Tanzania kusakata kabumbu kwa nyakati tofauti, lakini wakajikuta wakiingia kwenye mahusiano na wanawake wa Kitanzania na baadae kuwaoa kabisa.


STEPHANE AZIZ KI

Supastaa huyu wa Yanga ndiyo kwanza ndoa yake bado ni mbichi na binti wa Kibongo, Hamisa Mobetto ambaye walifunga pingu za maisha Februari 16, mwaka huu, baada ya kukaa katika mahusiano kwa miezi kadhaa.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ndoa ya wawili hao ilifungwa katika Msikiti wa Nuur, Mbweni, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na nyota wengine wa Yanga ambao walijitokeza kumpa kampani mwenzao kukiwa pia na mastaa wa tasnia nyingine kama muziki, filamu na mitindo.

Aziz Ki alifunga ndoa na Hamisa ambaye ni mmoja ya wasanii wenye majina makubwa nchini baada ya raia huyo wa Burkina Faso kukamilisha taratibu zote za ndoa na kwa sasa wanaishi kama mume na mke.


FELIX SUNZU

Unamkumbuka Felix Sunzu? Yule straika ambaye alisajiliwa na Simba msimu wa 2011/12 na kufunga katika Dabi ya Kariakoo ambayo Yanga walifungwa mabao 5-0? Basi raia huyo wa Zambia kwa sasa ni kama Mtanzania tu kwa kuwa utamuona muda wote anatembea mitaa mbalimbali ya Jiji la Mwanza.

Unajua ni kwa sababu gani? Sunzu amehamishia makazi yake Tanzania kutoka kwao Zambia na katika kuonyesha kunogewa na maisha ya Bongo amemuoa mwanamama Juliana Enock ambaye ni Msukuma wa Mwanza.

Mzambia huyo aliweka wazi kwamba anapenda kuishi Tanzania kwa kuwa Watanzania ni wakarimu na wasiofuatilia mambo ya watu jambo ambalo linamfanya kuishi atakavyo na amefungua duka lake la kuuza jezi jijini Mwanza. Sunzu na Juliana kwa pamoja wana watoto watatu ambao ni Enock, Catherine na Mo Fernandez.


AMISSI TAMBWE

Kwa mara ya kwanza raia huyu wa Burundi aliikanyaga ardhi ya Tanzania 2013 baada ya kusajiliwa na Simba akitokea Vital'O ya nchini kwao. Uwezo wa Tambwe katika kufunga akiwa ametoka kuibuka mfungaji bora wa Kombe la Kagame mwaka huo ndiyo uliowalazimisha mabosi wa Simba fasta kumpigia simu kisha kumalizana naye na kumpa mkataba wa miaka miwili.

Baada ya kutua na kucheza msimu mmoja na nusu Msimbazi, Tambwe aliibukia Yanga ambao walimnyakua muda mfupi tu baada ya straika huyo kutemwa Msimbazi.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kilichotokea baada ya hapo, Tambwe alijitengenezea jina kubwa Yanga akiwa mmoja wa mastraika ambao wanajua kucheka na nyavu. Lakini, tukiachana na huko, nyota huyu pia ni mmoja wa wachezaji ambao walipagawishwa na pisi za Bongo kisha wakazama mazima kwa kuoa.

Tambwe alimuoa bibie Raiyan Mohammed aliyezaliwa Mbeya lakini akiwa na asili ya Uarabuni, na stori ya mahaba ya wawili hao ilianzia baada ya kukutana Ilala Boma, Dar es Salaam ambapo Raiyan alikuwa anakwenda mjini kisha Tambwe akampa lifti na kubadilishana namba za simu.

Tambwe na Raiyan walifunga ndoa Novemba 10, 2018 na walibarikiwa kupata watoto wawili wa kike na kiume anayeitwa Ayman. Staa huyo mwenye mafanikio anatarajia kurudi tena Tanzania hivi karibuni baada ya kutajwa kuwa meneja wa Singida Black Stars.


MUKOKO TONOMBE

Uwezo wa kulisaka soka, kuwaongoza wenzake vizuri uwanjani pamoja na staili ya kushangilia kama anawafundisha nyota wenzake ndivyo vilizaa jina la Ticha ambalo alijulikana nalo kirahisi kokote alikopita.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Huyu ni Mukoko Tonombe, kiungo mkabaji ambaye alitua nchini 2020 kuitumikia Yanga baada ya kusajiliwa akitokea AS Vita ya kwao DR Congo, ambapo ujio wake ulikuja kuongeza kitu katika eneo la kiungo cha timu hiyo.

Ubora wa Mukoko kukaba na kupiga pasi havikuishia uwanjani tu kwani alimuona binti mrembo wa Kitanzania, Trisha Maxis ambaye walianzisha mahusiano ambayo baadaye yakazaa ndoa ambayo ilifungwa Mei 26, 2023 na wawili hao kwa sasa wanaishi  DR Congo ambako kiungo huyo anaichezea TP Mazembe.


HARUNA NIYONZIMA

Huyu kiungo ambaye amecheza kwa mafanikio makubwa akiwa Yanga, lakini pia aliitumikia Simba, akianza kucheza Ligi Kuu Bara 2011-2017 ndani ya Yanga. Niyonzima aliondoka Yanga na kujiunga na Simba ambako alidumu kwa miaka miwili kuanzia 2017 hadi 2019.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kiungo huyo ambaye ametwaa mataji na timu zote mbili, ukiondoa ubora aliokuwa nao aliamua kuopoa pisi ya Kitanzania ambayo ilikuwa ni ndoa yake ya pili akimuoa Cassandra Rayan wa Bagamoyo mkoani Pwani.

Ukiachana na ndoa hiyo halali aliyofunga kiungo huyo, pia ameacha mtoto wa kiume Tanzania ambaye alizaa na staa anayefanya vizuri kwenye tamthilia ya Huba, Marry Blizzy maarufu kama Doris.


ABASILIM CHIDIEBELE

Mchezaji huyu wa Kinaijeria alitua nchini 2013, akazitumikia timu za Stand United, Coastal Union na Mbeya City.

Ingawa kuna wakati alitimkia Caps United ya Zimbambwe, lakini alirejea nchini na amemuoa Tabitha James wa Mwanza na kufanikiwa kupata naye watoto wawili wa kiume na kike, huku wa kwanza ana miaka 10 ilhali wa pili anatimiza miaka minne.