Prime
Hili la kupeleka mechi Amaan litufumbue macho

Muktasari:
- Kabla ya kutoa maagizo hayo Mei 14, CAF ilitangaza kuufungia uwanja huo mara baada ya mechi ya robo fainali ya michuano hiyo baina ya Simba na Al Masry uliofanyika kwenye uwanja huo mkubwa kuliko yote nchini; na yaliyotokea yalikuwa ya kufikirisha.
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeelekeza mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Simba na RS Berkane ya Morocco ifanyike kwenye Uwanja wa New Amaan, uliopo Unguja Zanzibar kutokana na tatizo la Uwanja wa Benjamin Mkapa kujaa maji wakati wa mvua.
Kabla ya kutoa maagizo hayo Mei 14, CAF ilitangaza kuufungia uwanja huo mara baada ya mechi ya robo fainali ya michuano hiyo baina ya Simba na Al Masry uliofanyika kwenye uwanja huo mkubwa kuliko yote nchini; na yaliyotokea yalikuwa ya kufikirisha.
Kabla ya mchezo huo uliofanyika Aprili 9, mvua kubwa zinazoendelea jijini Dar es Salaam, zilinyesha na hivyo maji kutanda sehemu kubwa, hali iliyolazimisha wafanyakazi wa uwanja kufanya kazi ya ziada ya kuyasukuma kwa mifagio kuyaondoa sehemu ya kuchezea.

Juhudi hizo hazikuweza kurekebisha sehemu hiyo muhimu ya kuchezea ya uwanja huo ulioanza kutumika mwaka 2007 na kusababisha utelezi au mpira kukwama nyakati fulani, hivyo kuondoa ladha ya mechi ya hatua hiyo muhimu.
Hii ilikuwa baada ya serikali kutoa tamko la kuishangaa CAF kwa kuufungia uwanja wakati marekebisho muhimu yalishafanyika. Bila shaka hilo la mfumo wa kutoa maji uwanjani lilikuwa muhimu zaidi kati ya marekebisho yaliyotakiwa kufanywa.
Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alisema mamlaka zilishafanya marekebisho muhimu na kwamba uwanja ulikuwa tayari kwa mechi yoyote, akitaka maofisa wa chombo hicho kinachosimamia uendeshaji mpira wa miguu Afrika, wafike tena kukagua ili uanze kutumika kwa mechi za kimataifa.

Lakini matokeo yake yakawa ile sinema ya Simba v Al Masry iliyosababisha uwanja kufungiwa tena.
Yote hayo yalitokea baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao unaweza kuchukua watu 60,000 waliokaa na ambao uligharimu kwa wakati huo Sh56 bilioni kufanyiwa marekebisho kwa muda mrefu yanayotakiwa kugharimu Sh31 bilioni, kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Husna Saliboko.
Mbali na marekebisho ya Benjamin Mkapa, serikali ilitenga jumla ya Sh50 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa viwanja mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuwa mwenyeji wa fainali za mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zitakazofanyika Agosti, na za Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2027. Mashindano hayo yote yataandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.

Barua ya CAF kutangaza mechi hiyo itafanyika Uwanja wa Amaan imeibua malalamiko mengi, hasa kutoka klabu ya Simba ambayo ilidai, RS Berkane walipewa taarifa Mei 14, hivyo kuandaa hoteli siku hiyo, lakini barua hiyo inaonyesha kuwa hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitumiwa barua hiyo siku moja na wenzao wa Morocco.
Barua hiyo ilimuinua kitini Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye Jumamosi alifanya ziara kwenye uwanja huo na kuhakikishiwa kuwa marekebisho yote yameshafanyika na uko tayari kutumika kwa mechi ya aina yoyote ile.
Natumaini kauli ya safari hii ya Waziri Mkuu itakuwa na uzito zaidi ya ile ya Msigwa na kama haitakuwa sahihi, basi itakuwa ni kosa kubwa kumdanganya Mtendaji Mkuu wa serikali kwa jambo muhimu ambalo linaweza kulitia aibu taifa mbele ya Afrika.

Ni muhimu sana kuwa wazalendo na kutetea rasilimali na mali zetu, lakini pale tunapokuwa na uhakika wa ubora wake. Kama hatuna uhakika na ubora wake ni muhimu kutoona aibu na kueleza kuwa utayari wetu bado haujafikia asilimia mia ili tujiwajibishe na kujituma zaidi kufikia malengo yanayokusudiwa.
Tunajua kabisa kazi ya kurekebisha miundombinu ya kuondoa maji uwanjani kwa haraka, hasa wakati wa mvua si kitu cha mchezo na kinachukua muda mrefu. Na kwa kuwa ni kazi kubwa, uhai wake huchukua muda mrefu kabla ya kufanya marekebisho mengine.
Hivyo ni lazima masuala haya yazingatiwe wakati wa kushughulikia na kutoa matamko kuhusu mali zetu na miundombinu yake ili kujiepusha na dosari na fedheha kama iliyotokea wakati wa mchezo wa Simba na Al Masry.
Tumeona viongozi wa Simba wakitoa kauli kali hadi za kuishutumu CAF kuwa iliitaarifu RS Berkane kuhusu uwanja hata kabla ya kuwataarifu wenyeji na kwamba wana wasiwasi kuwa huenda huo ukawa ni mpango wa kuiyumbisha Simba ili isifanye vizuri.
Na kuna barua inayosambaa mitandaoni kuwa Simba imeandika barua ya kutaka mchezo huo wa marudiano uchezwe Algeria, jambo ambalo linaweza kuwa ni kuingilia tatizo la kidiplomasia kati ya Algeria na Morocco ambalo limedumu kwa muda mrefu na limesababisha mechi kadhaa baina ya timu za nchi hizo mbili zisichezwe.

Lakini ukweli umedhihirika kuwa tuhuma hizo hazina mashiko kwa kuwa Uwanja wa Mkapa haukuwa umeondolewa adhabu na pande zote zilitaarifiwa siku moja kuhusu uwanja utakaotumika kwa mechi ya marudiano ya fainali.
Kwa hiyo ni muhimu sana kuwa thabiti wakati wa kushughulikia masuala ya kitaifa kama la kukamilika kwa marekebisho ya uwanja na taratibu za kufuata ili zuio hilo la CAF kuutumia Uwanja wa Mkapa liondolewe na mechi ichezwe sehemu ambayo klabu inaona ina mazingira mazuri kushinda.
Wakati huu tunaelekea kuandaa fainali za CHAN miezi miwili ijayo ni muhimu masuala ya ukaguzi yafanyike mara kwa mara kubaini kama kuna kasoro zimejitokeza kutokana sababu mbalimbali na hata kufuatilia mwenendo wa uwanja nyakati za mvua. Kuna kiongozi wa Simba alienda uwanjani hapo na kupiga picha kuonyesha sehemu ya kuchezea ni nzuri, lakini picha hiyo ilipigwa wakati mvua haijanyesha!
Mali kubwa kama Uwanja wa Mkapa inatakiwa iangaliwe kama mboni ya jicho kwa kuwa fedha nyingi za walipa kodi zimetumika kuujenga kwa lengo la kuiwezesha nchi kuandaa mashindano makubwa kama ya mpira wa miguu, riadha na michezo mingine.
Itakuwa ni fedheha kama doa kama la Simba v Al Masry litajirudia wakati tukijiandaa kwa fainali za CHAN miezi miwili ijayo. Wakati huu serikali inajenga uwanja mwingine mkubwa mkoani Arusha na bado ina mpango wa kujenga uwanja wa kisasa mkoani Dodoma, uwezo wetu wa kutunza na kusimamia viwanja ni lazima uwe thabiti na wenye weledi.