Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RS Berkane walivyonusa kombe ardhi ya Unguja au Temeke

JICHO Pict

Muktasari:

  • Tulisikia mengi kuelekea fainali hii. Mbwembwe nyingi kutoka kwa watu walioambatana na timu katika ndege binafsi kuanzia safari ya Dar es Salaam hadi Casablanca kisha Oujda kabla ya kwenda Berkane.

TOFAUTI katika mpira ilikuwapo jana kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane. Rafiki zetu walituonyesha wazi kwamba wametuacha mbali kisoka. Mengine ambayo tunajaribu kufanya kwa sasa ni kufarijiana. Simba alikuwa katika tanuri la moto katika fainali ya kwanza dhidi ya Berkane jana.

Tulisikia mengi kuelekea fainali hii. Mbwembwe nyingi kutoka kwa watu walioambatana na timu katika ndege binafsi kuanzia safari ya Dar es Salaam hadi Casablanca kisha Oujda kabla ya kwenda Berkane. Ilionekana kama vile ingekuwa mechi ngumu kwa mwenyeji. Haikuwa ngumu na kumbe wangeweza kumaliza fainali pale pale nyumbani na kisha kuja Tanzania kutalii.

Kilichoonekana ni kwamba Berkane waliiunda timu yao kimya kimya kwa ajili ya kuwashangaza Wamorocco kwa kutwaa ubingwa wa Ligi hiyo maarufu kama Botola. Halafu wakaja kutushangaza katika michuano hii ya shirikisho kwamba sio hadhi yao. Wanastahili kule kwa wakubwa wengine.

Na hata msimu ujao wakati watakapokuwa wanashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa ni wazi kwamba Berkane watafika zao mbali. Hiki kilikuwa kiwango tosha cha kufika hata fainali za Ligi ya Mabingwa kama wangeandaa timu yao mapema.

JICH 01

Wametuonyesha kwamba kuna njia ambayo Simba walipita kufika fainali na inawezekana haikuwa sahihi sana. Hawakuwahi kukutana na changamoto ngumu mpaka walipoangukia katika mikono ya kina Mamadou Camara, ustaadhi Yassine Lebhiri na wengineo. Ni ndoto inayotisha.

Safari ya ugumu wa Simba kutwaa taji lenyewe ilianza ndani ya dakika kumi tu. Camara aliruka peke yake katika mpira wa kona na kufunga. Kumbe tulitakiwa kuwa makini kwa kila kitu. Pale Simba hawakuwa makini na mchezaji mrefu kuliko wote uwanjani. Hakuna hata aliyemghasi.

Tuna hili tatizo. Kama Camara asingefunga basi asingefunga tena kwa kona. Kwa sababu wachezaji wa Simba wangegundua uhatari wake. Tatizo hatupimi uhatari wa tatizo kabla halijatokea. Huwa tunagundua tatizo baada ya kutokea.

JICH 02

Baadaye Oussama Lamlaoui akafunga tena baada ya Camara wetu ambaye ni kipa kujaribu kuanzisha mpira kwa nyuma huku mchezaji wake, Yusuf Kagoma akiwa hayupo tayari. Katika mpira wa kisasa makocha wamekuwa wakisisitiza mchezaji aendelee na kanuni zile zile alizofundishwa lakini Camara alipaswa kupima joto la mechi yenyewe. Angepiga mbele tu.

Kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa mechi Berkane walituonyesha uwezo wa kila kitu. kwanza kabisa walikuwa bora wakiwa na mpira. Kila mchezaji alijua aufanyie nini mpira. Pili walikuwa bora pindi walipokuwa hawana mpira. Walikaba kuanzia juu, katikati na chini kabisa.

Haikushangaza kwamba hadi wakati pambano linamalizika Simba ilikuwa haijapiga shuti hata moja lililolenga lango la Berkane. Takwimu nzuri za mechi ni kwamba Simba walipiga kona mbili. Na kona pia ni sifa ya ukabaji kwa anayeshambuliwa.

JICH 03

RS Berkane walitulia na mpira mguuni. Walipiga pasi sahihi. Walifungua uwanja sahihi. Waliwahi kuingilia mipira isiyowahusu. Waliwahi kucheza 'first balls' kama Simba wangepiga mipira mirefu. Walikuwa wepesi katika kuonana kuelekea katika lango la Simba.

Katikati ya uwanja Camara wao alinikumbusha Patrick Vieira wa Arsenal. Ndio wote ni Wasenegali kwa sababu hata Vieira alitoroka Senegal kwenda Ufaransa. Camara ana futi 6'4 na bado alikuwa na mnyumbuliko wa ajabu uwanjani.

Camara alipora mipira yote, alipiga pasi zote kwa usahihi sana na mwisho wa kila kitu alikuwa injini ya timu katika kukaba, lakini pia katika kupiga pasi ndefu kwa mastaa wenzake wa eneo la mbele ya uwanja. Nitaandika kitu kuhusu yeye kesho.

JICH 04

Kipindi cha pili Berkane walipunguza kasi na VAR pia iliwapunguza kasi ilipokataa bao lao. Pengine ni bao ambalo limeiweka Simba katika uhai hadi sasa kiasi kwamba kipa Camara alianza kupoteza muda akiamini kwamba mabao mawili yalikuwa yanatosha kuweza kujaribu kupindua meza watakaporudi kucheza Tanganyika au Zanzibar wiki ijayo.

Simba ina nafasi? Nadhani kazi ifanyike. Kwa taswira ya mechi ya jana, shabiki ambaye hazifahamu timu zote mbili anajua wazi kwamba shughuli itakuwa imeishia pale. Zilikuwa timu mbili tofauti. Lakini kwa mpira wa Kiafrika Simba walishangilia kwa sababu wanaamini kuna mambo yanaweza kufanyika na wakarudisha mabao mawili.

Swali linakuja namna gani wanaweza kupata mabao hayo mawili hadi la tatu. Kwa mchezo ambao tuliutazama nadhani Berkane inabidi iwe na siku mbovu uwanjani ili isipate bao lolote Unguja au Dar es Salaam au katika uwanja wowote wa soka duniani.

Kunaweza kuwa na mambo yale mengine nje ya uwanja lakini kwa maana ya kuwapigia kelele Berkane nadhani haina msaada mkubwa. Mechi ya kwanza dhidi ya Wydad walisafiri mpaka katika uwanja wa mauti na chuki lakini wakashinda bao 1-0 huku wakiwa pungufu.

JICH 05

Na mechi nyingine dhidi ya watemi wengine wa jiji hilo Raja walisafiri hadi Casablanca na bado wakashinda 1-0. Sidhani kama sisi tuna kelele na vurugu nyingi kushinda mashabiki wa Wydad na Raja. Labda kuwe na mambo mengine nje ya uwanja.

Itakuwa shida kama Berkane watapata bao lolote kwa sababu Simba wameshindwa kufanya hivyo au hata kukaribia kufanya hivyo pale Morocco. Utakuwa mtihani mkubwa kwa Simba kujaribu kuleta uwiano wa kushambulia na kujilinda kwa wakati mmoja.

Itakuwa kazi ngumu kusaka mabao mawili na hapo hapo kuhakikisha Berkane hawaleti madhara yoyote katika lango lao. Imani kwamba Simba inafanya vizuri katika mechi za nyumbani ni jambo zuri lakini kuna wakati wa kupima aina ya timu ambayo wanacheza nayo. Berkane wanaonekana kuwa wa moto.