Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliondoka Simba wanakiwasha Yanga

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Hili lilikuwa linashuhudiwa kwenye Ligi Kuu Bara wachezaji pendwa wa vigogo hao baadhi walisajiliwa kwenda kwa wapinzani wao wakiwa kwenye kiwango bora na walipojiunga nao walishuka na wengine waliendeleza ubora wao.

LIGI Kuu ya Wanawake imekua kiasi cha timu pinzani kutunishiana misuli kwenye usajili wa wachezaji mfano msimu uliopita wachezaji watatu wa Yanga Princess walijiunga na Simba Queens baada ya kuwekewa mkwanja mrefu wakasepa.

Hili lilikuwa linashuhudiwa kwenye Ligi Kuu Bara wachezaji pendwa wa vigogo hao baadhi walisajiliwa kwenda kwa wapinzani wao wakiwa kwenye kiwango bora na walipojiunga nao walishuka na wengine waliendeleza ubora wao.

Sasa tambo za kusajili zimehamia katika soka la wanawake, wachezaji waliowahi kuvalia jezi nyekundu ya Msimbazi sasa wamegeuka silaha hatari ndani ya kikosi cha Wananchi wa kike.

Msimu huu, Yanga Princess wameonekana kunufaika zaidi na wimbi la mastaa waliowahi kuachwa Simba Queens na kuwa tegemeo kwenye maeneo tofauti hasa ya ulinzi.

Mwanaspoti linakuchambulia mastaa waliowahi kutamba na Simba na walipoachwa wakageuka mhimili mkubwa ndani ya kikosi cha wananchi.


ASHA DJAFAR

Winga huyo alikuwa mmoja ya wachezaji 13 waliopewa mkono wa kwaheri na Simba Queens msimu uliopita hasa kwa wale ambao waliamini hawataendelea nao msimu huu.

Baada ya kuachana na Simba Queens, Yanga Princess ikamsajili katika dirisha dogo na kufikisha idadi ya wachezaji watatu kutoka Msimbazi kujiunga na Wananchi.

Tangu alipojiunga na Yanga alichangia mabao matano katika mechi nne akifunga mabao matatu na asisti mbili na kuwa mmoja ya wachezaji muhimu na wenye mchango mkubwa kwenye kikosi cha kocha Edna Lema 'Mourinho'.

Djafar ni kati ya wachezaji wawili pekee wa kigeni waliowahi kuchukua kiatu cha ufungaji bora wa ligi akinyakua msimu wa 2021/22 baada ya kuweka kambani mabao 27 na mwingine Jentrix Shikangwa aliyebeba kiatu msimu 2022/23 baada ya kutupia mabao 17.


PRECIOUS CHRISTOPHER

Hii ni mara ya pili kwa nyota huyo anayetumia mguu wa kushoto kuitumikia timu hiyo ya wananchi. Msimu wake wa kwanza ulikuwa mwaka 2022 alipojiunga na Yanga Princess akitokea Rivers United ya nchini kwao Nigeria.

Baada ya kucheza misimu miwili Yanga bila mafanikio msimu wa 2024/25 alijiunga na watani wao Simba Queens lakini nako hakufanikiwa kunyakua taji akacheza msimu mmoja akarejea tena Jangwani.

Wakati anaondoka Yanga ndani ya misimu yote miwili alifunga mabao matatu na asisti moja idadi ambayo ni sawa na aliyofunga akiwa Simba.

Fundi huyo wa kupiga mipira ya frii-kiki baada ya kurejea kwenye mechi 11 tayari amefunga mabao manne akivunja rekodi ya misimu mitatu aliyocheza ligi ya wanawake (WPL).

Tangu alipoondoka, Yanga ilikuwa na uhaba wa kiungo mshambuliaji mwenye sifa zake na kurejea kwake kumeisadia Yanga msimu huu hasa kwenye kuichezesha timu na kusambaza pasi.


WINCATE KAARI

Ni beki wa kushoto ambaye alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2020 akitokea Thika Queens ya nchini kwao Kenya ambako alikuwa na kiwango bora kiasi cha kuwashawishi mabosi wa wananchi.

Aliitumikia Yanga misimu minne akifunga mabao mawili na kutoa asisti 13, lakini ndani ya misimu yote hakufanikiwa kuchukua ubingwa hivyo akaamua kujiunga na watani wao msimu wa 2024/25.

Simba hakucheza muda mrefu akiitumikia msimu mmoja kisha akarejea tena kwa wananchi na sasa ni moja ya mabeki wanaotegemewa ndani ya kikosi hicho.


RITTICIA NABBOSA

Huyu ni nyota mwingine ambaye raia wa Uganda ambaye amezitumikia timu zote mbili, ni kiungo muhimu kwenye kikosi cha Yanga kwa sasa ambaye ameituliza timu kwa kiasi kikubwa msimu huu.

Kabla ya kuitumikia Simba misimu miwili mfululizo kuanzia 2023/24 na kuchukua ubingwa mara moja, alikipiga Fountain Gate Princess alipokuwa na misimu bora.

Msimu wa kwanza Simba alipata nafasi ya kuanza na kuwa mmoja ya wachezaji tegemeo, lakini uliofuata ni kama hakuwa na nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kocha Juma Mgunda ndipo baadaye akajiunga na wananchi.


DIANA MNALLY

Ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kupata nafasi kwenye kikosi cha wekundu wa Msimbazi, aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao kwenye mashindano ya Kombe la Dunia U-17 mwaka 2022.

Alijiunga na Yanga msimu uliopita akitokea Gets Program ambako hakucheza muda mrefu akatimka kutokana na changamoto ya maslahi na kutolipwa mishahara.

Aliondolewa Simba baada ya kukutana na ushindani kwenye eneo hilo lililokuwa chini ya Mzimbabwe Danai Bhobho na nyota wengine wazawa akiwamo Doto Evarist.

Sasa hivi ndiye mchezaji tegemeo eneo la beki wa kushoto na amekuwa na muendelezo mzuri kiasi cha kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana U-20, Tanzanite Queens cha kufuzu Kombe la Dunia.