Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vyuma vitatu vinaondoka na utamu wake England

VYUMA Pict

Muktasari:

  • Kwa pamoja, majina hayo yamekuwa ni mihimili katika vikosi vya timu husika na siyo wachezaji wa kawaida, bali ni alama ya ubora, uthabiti na mafanikio yaliyoifanya EPL kubaki kuwa ligi yenye ushindani mkubwa zaidi duniani.

LONDON, ENGLAND: MWISHO wa msimu wa Ligi Kuu England (EPL) unatarajiwa kuwa wa kihistoria, ukibeba simulizi tamu na chungu.

Miongoni mwa zile simulizi chungu ni ile ya kuaga kwa nyota watatu waliolitawala soka la ligi hiyo kwa nyakati tofauti na hao ni pamoja na Mohamed Salah, Casemiro na Bernardo Silva.

Kwa pamoja, majina hayo yamekuwa ni mihimili katika vikosi vya timu husika na siyo wachezaji wa kawaida, bali ni alama ya ubora, uthabiti na mafanikio yaliyoifanya EPL kubaki kuwa ligi yenye ushindani mkubwa zaidi duniani.

Kuondoka kwao kunafunga ukurasa mpya huku kukifungua milango kwa kizazi kipya kinachotakiwa kuiga au hata kuzidi viwango walivyoviweka.

VYUM 05

MO SALAH

Tangu alipotua katika kikosi cha Liverpool 2017 akitokea AS Roma ya Italia, Mohamed Salah amefanikiwa kujenga hadhi ya kubwa akiwa mmoja wa wafungaji hatari zaidi kuwahi kutokea katika Ligi Kuu England.

Ndani ya zaidi ya misimu saba aliyocheza, Salah amefaniki kufunga zaidi ya mabao 150 akitoa pasi za mabao 60 katika ligi hiyo, takwimu zinazomuweka katika kundi la magwiji wa ligi hiyo.

Ingawa kwa ujumla anatajwa kufunga mabao 255 katika mashindano yote akiichezea timu hiyo kwenye michezo 435, akiwa mchezaji wa tatu wa Liverpool aliyefunga mabao mengi zaidi tangu ilipoanzishwa miaka 133 iliyopita akiwa na wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 138.

Wanaomtangulia ni Ian Rush (mabao 346) na Roger Hunt (285) huku akiwa juu ya Gordon Hodgson aliyetupia nyavuni mara 234 na Billy Liddell (215).

Katika msimu wake wa kwanza pekee ulimshuhudia akifunga mabao 32, rekodi iliyovunja historia kwa msimu wa mechi 38. Kwenye mafanikio ya pamoja, aliisaidia Liverpool kushinda ubingwa wa EPL msimu wa 2019/20, Ligi ya Mabingwa Ulaya 2018/19 pamoja na FA na Carabao.

Upande wa tuzo binafsi Mo Salah ameshinda Kiatu cha Dhahabu mara tatu na tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa England (PFA) mara mbili, akionyesha ubora wa kiwango cha juu kwa muda mrefu.

VYUM 06

Kutokana na mafanikio hayo thamani ya Salah ilipanda kwa kasi kutoka Pauni 36 milioni hadi zaidi ya Pauni 150 milioni katika kilele cha ubora wake ikionyesha namna alivyokuwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya uwanja.

Kwa sasa mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea, Fiorentina, Basel na Al-Mokawloon ya kwao Misri anatarajiwa kuondoka akiwa na thamani inayokadiriwa kuwa kat ya Pauni 60 hadi 70 milioni ikionyesha athari ya umri (miaka 33), lakini siyo kushuka kwa ubora wake kwa kiasi kikubwa.

Kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp aliwahi kumuelezea Sala kuwa mchezaji “anayebadilisha mchezo ndani ya sekunde chache,” kauli inayodhihirisha namna alivyokuwa silaha muhimu kwa Liverpool.

Kuondoka kwake kunaacha pengo, si tu kwa mabao, bali pia uongozi uwanjani na uzoefu. Inatarajiwa kwamba Salah atakwenda katika moja ya timu za Ligi Kuu Saudi Arabia (Saudi Pro League), ambako atakutana na maisha mapya yenye ushindani mdogo wa kila wiki, lakini yakiwa na mvuto mkubwa wa kifedha na hadhi ya kuwa balozi wa soka katika eneo hilo.

VYUM 04

CASEMIRO

Kwa upande wake Casemiro ambaye jina lake kamili ni Carlos Henrique Casimiro, ujio wake Manchester United 2022 kutoka Real Madrid aliyoitumikia kwa miaka tisa (2013- 2022) ulikuwa ni suluhisho la haraka kwa matatizo ya kiungo cha ulinzi ya klabu hiyo.

Ingawa alipotua tu kikosini alianza kwa kusuasua pengine kutokana na mazingira ya soka la England, lakini baadaye alifanikiwa kusimama imara na kufanikiwa kujimilikisha namba sita, akiwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza.

Ndani ya misimu yake minne EPL, ameleta utulivu Man United unaoambatana na nidhamu na uzoefu mkubwa kikosini uliotokana na mafanikio yake Ulaya, kwani akiwa Real Madrid alifanikiwa kubeba zaidi ya tuzo binafsi na mataji 20 ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano, La Liga mara tatu na Kombe la Dunia la Klabu mara tatu.

Alipotua Man United 2022, wengi waliona kama ni hatua ya mwisho ya soka lake, lakini aliendelea kuonyesha thamani yake kwa kuisaidia timu hiyo kushinda Kombe la Ligi 2023 na FA 2024. Hii inaonyesha kuwa hata katika hatua za mwisho za ubora wake, bado amekuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya ndani ya timu.

VYUM 03

Ndani ya Man United, Casemiro amecheza mechi nyingi za ushindani, akifunga mabao zaidi ya 10, mengi yakiwa  muhimu katika mechi kubwa. Ingawa hajabeba ubingwa wa EPL mchango wake umeisaidia Manchester United katika kipindi kigumu inachopitia cha zaidi ya misimu ya 10.

Casemiro alifika England akiwa na thamani ya takriban Pauni 70 milioni, lakini sasa imeshuka hadi kati ya Pauni 35 milioni na 40 milioni kutokana na umri wake. Hata hivyo, mchango wake haupimwi kwa thamani ya soko pekee bali ushawishi wake uwanjani.

Wakati fulani, kocha wa zamani wa Manchester United, Erik ten Hag aliwahi kusema kuwa Casemiro ni “moyo wa timu,” akisisitiza umuhimu wake katika kusawazisha makosa na kuweka mambo sawa katika eneo la kiungo.

Anatarajiwa kuondoka EPL akiacha urithi bora wa kiungo wa ulinzi mwenye akili kubwa ya mchezo na uwezo wa kuongoza. Maisha yanayomsubiri yanaweza kuwa Saudi Arabia au kurejea Amerika Kusini, ambako ushindani utakuwa tofauti, lakini nafasi ya kuendelea kuwa na mchango kikosini itabaki kuwa wazi. Kabla ya kutua Real Madrid na kisha Man United, Casemiro aliichezea Sao Paolo ya kwao Brazil.

VYUM 02

BERNADO SILVA

Naye Bernardo Silva amekuwa mfano halisi wa wachezaji wenye ubunifu wa hali ya juu ndani ya Manchester City tangu alipojiunga 2017 akitokea AS Monaco, ambapo ndani ya misimu yake tisa EPL ametoa mchango mkubwa.

Kiungo huyo si tu ametoa mchango wa mabao 45 na asisti zaidi ya 50, pia kwa kudhibiti mchezo, kucheza nafasi nyingi akifanya kazi kubwa uwanjani.

Vilevile ameisaidia Manchester City kushinda EPL mara sita katika misimu ya 2017/18, 2018/19, 2020/21, 2021/22, 2022/23, 2023/24; FA 2018/19 na 2022/23, Carabao 2017/18, 2018/19, 2019/20, 2020/21 na 2025–26, Ngao ya Jamii 2018, 2019 na 2024, Ligi ya Mabingwa Ulaya 2022/23, UEFA Super Cup 2023 na Kombe la Dunia la Klabu 2023. Thamani ya Bernardo ilipanda hadi zaidi ya Pauni 90 milioni kabla ya kushuka kidogo hadi takribani Pauni 70 milioni.

Kocha Pep Guardiola anamwelezea mchezaji huyo kuwa mmoja wa nyota wenye akili kubwa zaidi ya soka, akisisitiza uwezo wake wa kuwasoma wapinzani na kuelewa mifumo ya uchezaji ni jambo la kipekee katika kikosi hicho. Bernardo anapoondoka anaiacha EPL akiwa mfano wa mastaa wenye ubunifu na nidhamu mchezo.

VYUM 01

Guardiola anasema: “Bernardo ni mmoja wa wachezaji wenye akili kubwa zaidi niliowahi kuwafundisha, na wabunifu kwelikweli akiwa na uwezo wa kuizawadia timu vitu vingi ikiwamo ubora katika kila eneo unalompangia majukumu uwanjani.”

Kwa sasa akiondoka Man City, Silva anaweza kwenda Barcelona au kujaribu changamoto mpya katika timu za ligi zingine Ulaya, ambako atakutana na mazingira tofauti ya ushindani lakini yenye hadhi sawa na England. Pia anaweza kurudi Benfica, klabu iliyoibua kipaji chake utotoni, huku ikielezwa ana ofa kibao mezani kwake kutoka Saudi Arabia.


WARITHI WAO

Kwa pamoja, Salah, Casemiro na Bernardo wanaiacha EPL ikiwa imejaa kumbukumbu za mafanikio yao. Huo unaweza kuwa mtihani mkubwa kwa kwa warithi wao ambao wanapaswa kuwa na uwezo wa juu zaidi unaombatana na  takwimu bora na uwezo wa kubeba presha ya ligi hiyo.

Ndani ya Liverpool, Florian Wiltz anaonekana kuwa mmoja wa wachezaji wanaoweza kuvaa vyema viatu vya Salah akiwa na kasi pamoja na uwezo mzuri wa kufunga mabao.

Hata hivyo, nje ya klabu hiyo, Liverpool inaweza kuvuta mashine ya Nottingham Forest, Dan Ndoye. Kwa upande wa Casemiro, ndani ya Manchester United, Kobbie Mainoo anaonekana kuwa na dalili za kuwa mrithi wake, huku nje ya klabu hiyo kukiwa na mastaa kibao wakiwamo Sandro Tonali wa Newcastle United na Carlos Baleba wa Brighton wanaotajwa kuanza kufukuziwa na kikosi hicho.

Nyota hao ni mfano wa viungo bora wa kisasa wenye uwezo wa kukaba na kushambulia, wakiwa na thamani kubwa na mafanikio kadhaa viwanjani.

Kwa upande wa Bernardo Silva, Phil Foden wa Manchester City tayari ameanza taratibu kuandaliwa akicheza japo mara moja moja katika eneo la kati la ushambuliaji akichezesha timu.

Kwa ujumla kuondoka kwa wachezaji hao watatu ni tukio litakaloacha simulizi fulani ya kipekee na pia kutoa nafasi ya mabadiliko kwenye vikosi vya timu hizo.

EPL itaendelea kuwa na ushindani mkali, lakini urithi wa Mohamed Salah, Casemiro na Bernardo Silva utaendelea kuishi kupitia kumbukumbu, rekodi na viwango walivyoweka ambavyo vitakuwa kipimo kwa vizazi vipya vya wachezaji wanaokuja.