VPL SPESHO: Kikosi cha msimu 2020-21

MSIMU wa 2020-21, umemalizika leohuku Simba ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya nne mfululizo huku wakiweka rekodi mbalimbali.

Hawa ni mastaa waliokiwasha zaidi msimu huu.


AISHI MANULA

Manula amekuwa mhimili wa Simba langoni mwao, huku mechi 17 kati ya alizocheza msimu huu akivimba bila ya kuruhusu bao. Hakuna kipa anayeweza kumfikia katika hili.

Manula amekuwa na kiwango bora kwa misimu mitano mfululizo akishinda tuzo ya kipa bora wa msimu mara nne na hata msimu huu anaweza kuichukua tena.


SHOMARY KAPOMBE

Beki wa kulia wa Simba, Kapombe amekuwa akitimiza vyema majukumu yake ya ulinzi na amekuwa tishio akipanda mbele kusaidia mashambulizi.

Washambuliaji wa Simba msimu huu wamefunga mabao kadhaa ambayo yametokana na mchango wake.

Amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza muda wote msimu huu kama ilivyokuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.


MOHAMMED HUSSEIN

Katika eneo la beki wa kushoto Tshabalala anaweza kupata nafasi ya kuanza kutokana na umahiri wake Simba wanapokuwa wanashambulia kwani mbali ya kuhusika katika mabao muda mwingine hufunga mwenyewe.

Tshabalala ameipa Simba pointi tatu muhimu katika mechi ya ugenini dhidi ya Gwambina kwa kufunga bao pekee la mechi hiyo waliyoshinda 1-0.


JOASH ONYANGO

Onyango amekuwa nguzo muhimu ya Simba msimu mzima, aking’aa katika michuano ya ndani na nje.

Alipotua akitokea Gor Mahia ya Kenya, wengi hasa wa mahasimu wao Yanga, walimkebehi kwamba ni mzee, lakini amethibitisha kuwa mmoja wa mabeki bora zaidi katika Ligi Kuu ya Bara.


PASCAL WAWA

Safu ya ulinzi ya Simba ndio imeruhusu mabao machache (14 tu), kutokana na ubora wa safu yao ya ulinzi msimu huu.

Wawa amekuwa nguzo imara katika kikosi cha Simba kwa kuwazuia washambuliaji wa timu pinzani, amehusika kuanzisha mashambulizi kwa kupiga pasi za maana na muda mwingine hufunga mwenyewe.

Msimu huu Wawa amekuwa bora zaidi na maelewano makubwa pindi anapocheza na Onyango, lakini beki mwingine ambaye anaweza kuingia katika nafasi hiyo ni Lamine Moro wa Yanga ambaye amefunga mabao manne ila masuala yake ya kinidhamu ndio shida.


MUKOKO TONOMBE

Kiungo mkabaji wa Yanga, anaingia katika kikosi bora cha msimu kutokana na umahiri wake wa kutimiza majukumu ya nafasi hiyo huku katika timu nyingi za ligi msimu huu wengi hawana sifa kama zake.

Tonombe mbali ya kutimiza majukumu yake ya kiukabaji ameifungia Yanga mabao matatu katika mechi muhimu dhidi ya Polisi Tanzania, Kagera Sugar (mechi mbili ya nyumbani na ugenini).

Mukoko licha ya kwamba huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya Yanga amethibitisha kuwa ni bora na hahitaji muda mwingi wa kuonyesha utawala wake.


LUIS MIQUISONNE

Winga wa kulia katika kikosi bora cha msimu atakuwepo, Miquissone ambaye ameifungia timu yake mabao tisa na kutoa asisti 11, tatu nyuma ya Clatous Chama ambaye ndio kinara wa pasi za mwisho.

Katika kikosi cha Simba na ligi nzima msimu huu moja ya wachezaji hatari katika kushambulia ni Miquissone ambaye ni bora kwenye kufunga, kutoa pasi za mwisho, kushuka chini kukaba na kuwasumbua wachezaji wa timu pinzani.

Katika eneo hili anaweza kuwepo mshambuliaji wa Gwambina, Mashack Abraham ambaye kwenye ligi msimu huu amefunga mabao tisa na kutoa pasi za mwisho mbili.


FEISAL SALUM

Katika eneo la kiungo mshambuliaji ataanza, Fei Toto ambaye amekuwa bora kwenye kutoa pasi za mwisho, kuanzisha mashambulizi na muda mwingine kufunga mwenyewe ndio maana hadi sasa ana mabao matano kwenye ligi.

Katika kikosi cha Yanga, Fei ni miongoni mwa wachezaji wazawa ambaye amekuwa na uhakika wa kucheza katika mechi zote msimu huu licha ya mabadiliko ya walimu yaliyofanyika.

Salum ni bora hata pale anapokutana na viungo wa timu pinzani walio imara, naye huonyesha makali yake, Katika eneo hili anaweza kuanza Yacouba Sogne ambaye amefunga mabao nane na kutoa pasi za mwisho nne.


JOHN BOCCO

Hakuna ubishi kuwa katika eneo la straika ataanza Bocco ambaye ndio kinara wa ufungaji mpaka wakati huu akiwa na mabao 15, ambayo yanamfanya kufikisha jumla ya mabao 141, tangu alipoanza kucheza ligi msimu wa 2008-09.

Straika huyo wa Simba mbali ya majeraha ya mara kwa mara ambayo yanamkumba lakini ushindani wa nafasi ya kucheza dhidi yake mbele ya Chriss Mugalu na Meddie Kagere amekuwa akifunga kila akipata nafasi ya kucheza.

Bocco ameifungia Simba mabao muhimu hata katika viwanja vya ugenini ambavyo washambuliaji wengi hushindwa kuonyesha makali yao lakini kama haitoshi hakuna beki ambaye anapenda kumkataba kutokana na usumbufu wake.


PRINCE DUBE

Straika wa Azam ndio msimu wake wa kwanza alianza vizuri kwenye ligi kwa kufunga mabao lakini alikutana na majeraha ambayo yalimuweka nje si chini ya miezi miwili lakini bado yupo katika chati ya wafungaji.

Dube anashika nafasi ya pili kwa wafungaji kwenye ligi mpaka sasa akiwa na mabao 14 na pengine kama si majeraha aliyoyapata angeweza kufunga idadi zaidi ya hiyo,

Licha ya kucheza mechi chache ameonyesha makali ya kufunga na anaingia katika kikosi cha kwanza cha wachezaji bora wa msimu huu akiwa ni mmoja wa wachezaji wa kigeni waliofanya vyema.


CLATOUS CHAMA

Huenda akatetea tuzo ya mchezaji bora ambayo alichukua msimu uliopita kwani katika ligi kufikia wakati huu ametoa mchango mkubwa katika mabao ya Simba.

Rekodi zinaonyesha Chama ndio kinara wa kutoa pasi za mwisho akifikisha 14, huku akifunga mabao nane kwa maana hiyo amechangia mabao 22, kati ya 73, ambayo Simba wamefunga kufikia sasa wakibakisha mechi moja tu na Namungo.

Hakuna ubishi Simba inapokwenda kushambulia Chama ni moja ya wachezaji hatari ambaye huwasumbua wachezaji wa timu pinzani, si rahisi kukabika anafunga na kutoa pasi za mwisho.