Vita ya MVP Ligi Kuu ya Wanawake iko kwao

Muktasari:
- Msimu uliopita tuzo hiyo ilikwenda kwa Aisha Mnunka wa Simba Queens ambaye pia aliibuka mfungaji bora akiweka kambani mabao 21 na kuiwezesha timu yake kuchukua ubingwa na kushiriki mashindano ya CECAFA.
WAKATI Ligi ya Wanawake (WPL) ikielekea ukingoni kuna nyota walioonyesha kiwango bora na huenda wakawania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka (MVP).
Msimu uliopita tuzo hiyo ilikwenda kwa Aisha Mnunka wa Simba Queens ambaye pia aliibuka mfungaji bora akiweka kambani mabao 21 na kuiwezesha timu yake kuchukua ubingwa na kushiriki mashindano ya CECAFA.
Nyota huyo hadi sasa amefunga mabao mawili kwenye mechi tano alizocheza akirejea kikosini hapo dirisha dogo baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne.
Msimu huu sasa kuna wakali wamekuja kivingine na kwa jinsi wanavyoonyesha viwango bora, ni wazi vita iko kwao na huenda tuzo ya MVP ikaenda kwa mmoja wao.
NEEMA PAUL (YANGA PRINCESS)
Winga huyu ndiye kinara wa ufungaji kwa Yanga Princess kwenye mechi 12 alizocheza amefunga mabao 12, wastani wa kufunga bao moja kwa kila mechi.
Mshamuliaji huyo amewahi kuzichezea Simba Queens, Fountain Gate Princess na Baobab Queens kabla ya kujiunga na Yanga, lakini huu unakuwa msimu wake bora wa kufunga mabao.
Kumbukumbu nzuri kwa nyota huyo alikuwa kwenye kikosi cha Serengeti Girls kilichofuzu Kombe la Dunia (W) U17 mwaka 2022 akiifunga Cameroon bao moja kwenye ushindi wa mabao 5-1 wakati huo timu hiyo ya taifa ilikuwa moto wa kuotea mbali.
STUMAI ABDALLAH (JKT QUEENS)
Kama kuna msimu bora kwa Mtanzania huyu basi ni huu akiweka rekodi mbalimbali ikiwamo kufunga mabao saba kwenye mchezo mmoja dhidi ya Mlandizi yaani alifunga double hat-trick.
Ndiye kinara hadi sasa wa Ligi hiyo akiweka kambani mabao 26 ambayo yamekuwa na msaada mkubwa kwa timu hiyo inayowania nafasi ya kuchukua ubingwa unaotetewa na Simba.
Stumai hadi sasa anaongoza kwa kufunga hat-trick akiwa nazo tano zinazomfanya kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka.
Nyota huyo wa Twiga Stars amevunja rekodi ya misimu mitano ya kufunga mabao mengi baada ya ule 2019/20 kuweka kambani mabao 22 kwenye mechi 18.
Msimu wa 2020/21 alicheza mechi tatu na kufunga mabao saba, msimu uliofuata alikaa msimu mzima akiuguza jeraha la goti.
Wakati Shikangwa anachukua kiatu cha dhahabu msimu 2022/23, Stumai alimaliza na mabao 14 kwenye mechi tisa ikiwa siku chache tangu atoke kuuguza majeraha yake, msimu jana alicheza mechi 18 na kuweka kambani mabao 19.
JENTRIX SHIKANGWA (SIMBA QUEENS)
Ni msimu wa tatu kwa nyota huyu Mkenya kuitumikia Simba Queens akisajiliwa kutokea Vihiga Queens ya nchini kwao alikokuwa na msimu bora.
Msimu wake wa kwanza 2022/23 alifunga mabao 17 kwenye mechi 18 licha ya timu yake kutobeba ubingwa lakini alifanikiwa kuchukua kiatu cha ufungaji.
Msimu uliofuata alimaliza na mabao manane akicheza mechi tisa baada ya kurudishwa Simba dirisha dogo aliposajiliwa kutokea Beijing ya China kwa mkataba wa miezi sita.
Wakati ligi haijamalizika msimu huu tayari amefunga mabao 19 akivunja rekodi yake binafsi ya misimu miwili akiingia kwenye vita ya ufungaji nyuma ya Stumai mwenye 26.
WINIFRIDA GERALD (JKT QUEENS)
Miongoni mwa makinda wanaofanya vizuri katika Ligi Kuu ya wanawake ukiwa msimu wake wa tatu sasa akizitumikia Fountain Gate ambako ndiko walikomkuza na sasa JKT.
Kinda huyo aliwahi kuwania tuzo za CAF kwenye kipengele cha mchezaji bora chipukizi, pia ana medali ya mashindano ya CECAFA kwa wasichana U-18 akiwa na kikosi cha timu ya taifa ‘Tanzanite Queens’ kilichobeba ubingwa huo mwaka 2023 mbele ya Uganda.
Msimu huu tayari ameifungia JKT mabao 10 akivunja rekodi yake ya msimu uliopita aliofunga mabao manane kwenye mechi 18 alizocheza.
Kutokana na muendelezo mzuri wa kufunga mabao akiwa na umri mdogo ni wazi atakuwa miongoni mwa nyota wanaotazamwa kuwania tuzo ya MVP. Mbali na kinyang’anyiro hicho huenda akachukua tuzo ya mchezaji bora chipukizi kwa kile alichokifanya na muendelezo wa kiwango chake akiisaidia JKT.
IGWE UZOAMAKA (YANGA PRINCESS)
Ni kitasa haswa ukitaja mabeki wa kati bora msimu huu basi jina la Mnigeria huyo lipo miongoni mwao kutokana na kile alichokinyesha kwenye msimu wake wa kwanza kuitumikia Ligi ya Tanzania.
Kama kuna usajili ambao Yanga imelamba jike basi ni mwanadada huyo ambaye ana uwezo mzuri wa kukaba kuanzia mipira ya chini na mipira mirefu lakini kubwa zaidi ni utulivu wake na nidhamu ya ukabaji.
Kabla ya kujiunga na Yanga msimu huu alipita klabu mbalimbali ikiwamo Bayelsa Queens ya nchini kwao na Malabo Kings FC ya Equatorial Guinea.
Amecheza mechi zote 15 na kuruhusu mabao 10 na kiwango alichoonyesha huenda akaingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka.
NAIJAT ABBAS (JKT QUEENS)
Ndiye kipa aliyeruhusu mabao machache zaidi akifungwa matatu tu WPL hadi sasa ikiwa ni idadi ndogo ya mabao kwenye mechi 14 alizocheza akiongoza kwa cleansheet 13.Nidhamu nzuri ya kuzuia mashambulizi ya timu pinzani huenda ikambeba msimu huu akachukua tuzo ya MVP kwa kile anachoendelea kukionyesha. Mbali na MVP lakini pia anaweza kuwania na kubeba tuzo ya golikipa bora mbele ya Janet Shija wa Simba Queens na Rita Akarekor wa Yanga.