Vichaka anavyoweza kuibukia Neymar Januari
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, klabu zinazohitaji huduma ya Mbrazili huyo zimeanza kutuma maombi ya kutaka saini ya mchezaji huyo.
RIO DE JANEIRO, BRAZIL: SUPASTAA wa boli, Neymar atakuwa mchezaji huru kwenye dirisha la Januari, hivyo ataondoka Santos huku jambo hilo likivutia timu nyingi zinazosaka mchezaji huyo mnyumbulifu uwanjani.
Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, klabu zinazohitaji huduma ya Mbrazili huyo zimeanza kutuma maombi ya kutaka saini ya mchezaji huyo.
Neymar, 33, amekuwa akitaabika juu ya ufiti wake tangu aliporejea Brazil, ambako kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Santos, lakini bado anasumbuliwa na ufiti na kiwango. Santos ipo kwenye hatari ya kushuka daraja huko kwenye Ligi Kuu Brazil, Serie A.
Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Palmeiras, Jumapili iliyopita uliifanya Santos kuwa na pointi moja juu ya shimo la kushuka daraja huku mechi zimebaki tano msimu kufika mwisho.
Lakini, swali linaloulizwa kwa sasa, Neymar atakwenda wapi? Je, muda umeshamtupa mkono kwenda kukipiga kwenye Ligi Kuu England? Hizi hapa timu tano zinazoweza kumnasa Neymar.
Chelsea
The Blues kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na Neymar na ilijaribu kunasa saini yake mwaka 2010 kabla ya Barcelona kufanikiwa kunasa huduma yake.
Kisha ilikuja kuelezwa kuwa Chelsea baada ya kuwa chini ya Todd Boehly ilijaribu pia kunasa saini yake kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2022.
Lakini, kwa sasa, Neymar umri wake upo juu kwa miaka 10 kutoka kwenye sera ya usajili wa Chelsea wa kutaka kunasa wachezaji vijana.
Hata hivyo, kutokana na kiungo mbunifu Cole Palmer kusumbuliwa na maumivu ya mara kwa mara, Chelsea inaweza kumnasa Neymar ili kuleta mbunifu mwingine kwenye kikosi chao.
Man United
Kama ilivyo kwa Chelsea, Manchester United imekuwa na kawaida ya kunasa mastaa wa Kibrazili, ambapo kwenye kikosi chao kwa sasa wapo Matheus Cunha na Casemiro.
Kuhusu Neymar, Man United ilihusishwa na mchezaji huyo mara kadhaa, hata katika kipindi ambacho alikuwa akicheza soka huko Saudi Arabia. Matajiri wa Man United bado wanatoa pesa ya usajili kwenye kikosi hicho, hivyo jambo hilo linafungua milango ya Neymar kwenda kukipiga kwenye kikosi cha Old Trafford, licha ya kwamba dili lake halitakuwa la pesa nyingi.
Man City
Ufundi wa Neymar ulikuwa gumzo huko Barcelona na jambo hili lilimvutia sana kocha Pep Guadiola, ambaye kuna wakati alihusishwa na mpango wa kwenda kunasa saini yake ili akakipige katika kikosi cha Manchester City.
Soka la kutumia nguvu nyingi kwenye Ligi Kuu England ndicho kitu ambacho kilimfanya Guardiola atie shaka juu ya kwenda kumsajili Neymar, lakini kwa sasa, wakati timu hiyo ikiwa inajaribu kutafuta wachezaji wabunifu wa kutosha kwenye kikosi chao, wanaweza kufanya usajili wa mkali huyo wa Kibrazili ili akacheze Etihad.
Liverpool
Katika kuungana na kundi la Wabrazili, Neymar endapo kama atakwenda kujiunga na Liverpool huku atakutana na kipa Alisson, wakati kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Anfield kuna Mbrazili mwingine aliyetengenezea sifa kubwa kabla ya kuondoka, Roberto Firmino.
Kocha Arne Slot anaweza kushawishika kwenda kumsajili Neymar, lakini saini yake inaweza kwenda kuleta ushindani mkubwa wa namba dhidi ya kiungo Florian Wirtz kwenye eneo la Namba 10 au kiungo wa pembeni kushoto.
Ufundi wa Neymar, kama hatosumbuliwa na majeraha ni hatari kwelikweli ndani ya uwanja ukimlinganisha na Mjerumani, Wirtz.
Newcastle United
Kutokana na kikosi cha Newcastle United kuwa na mastaa wa Kibrazili, Bruno Guimaraes na Joelinton, Neymar atakwenda kutua hapo St James’ Park na kujihisi kama yupo nyumbani tu.
Ukiweka kando suala la mazingira, kuwapo kwa kiungo hiyo ya Kibrazili, itamfanya Neymar kuwa na wakati mzuri wa kucheza soka lake kwa kiwango cha juu endapo kama hatakuwa anasumbuliwa na maumivu.
Newcastle kama ilivyo kwa Liverpool, inakosa mchezaji muhimu kwenye idara ya ubunifu na hilo linaweza kufanywa vizuri kabisa na staa huyo wa Kibrazili.