Hadithi ya Neymar huko Santos haivutii
Muktasari:
- Mechi sita zimebaki kwenye ligi ya Brazill, miamba hiyo ya Amerika Kusini, Santos ipo pointi mbili tu juu ya shimo la kushuka daraja, licha ya kwamba bado ina mechi mmoja mkononi.
SANTOS, BRAZIL: HADITHI ya supastaa Neymar kurudi Santos inaelekea kwenye mwisho mbaya tofauti na ndoto zake baada ya timu hiyo kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.
Mechi sita zimebaki kwenye ligi ya Brazill, miamba hiyo ya Amerika Kusini, Santos ipo pointi mbili tu juu ya shimo la kushuka daraja, licha ya kwamba bado ina mechi mmoja mkononi.
Na hilo limetokea baada ya kupoteza mechi ya pili ndani ya wiki moja ilipocheza ugenini.
Miamba inayofukuzia ubingwa Flamengo ilishinda 3-2 dhidi ya Santos, mechi ambayo ilimshuhudia Neymar akianzishwa kwa mara ya kwanza tangu Septemba.
Hata hivyo, kurejea uwanjani kwa Neymar kuliishia kwenye dakika ya 81, wakati huo Santos ilikuwa nyuma kwa mabao 3-0. Wakati anatoka uwanjani, Neymar alikumbana na kelele za kuzomewa na mashabiki wa Flamengo na maneno ya kumkashifu mchezaji huyo.
Santos ilifunga mabao mawili dakika za mwisho, lakini ilishindwa kusawazisha. Kwa Neymar, majanga yake yamekuwa hayafiki mwisho kutokana na kuwa na majeruhi mfululizo tangu alipotoka Saudi Arabia.
Katika mechi hiyo, Neymar alionyeshwa kadi ya njano baada ya kutibuana na mwamuzi, Savio Pereira Sampaio. Na Neymar, amesema: “Mwamuzi mbaya sana. Ukiweka kando kuwa mbaya, alikuwa mjinga. Wakiwa kwenye vyumba vyao wanasema manahodha ndio wanaoruhusiwa kuzungumza uwanjani. Tunapowafuata kuzungumza, wanatugeukia.”
Neymar aliongeza: “Nilipozungumza naye, alinitishia. Ni utata. Nilionyeshwa kadi ya njano kwa sababu alinitishia. Aliniambia: “Ukinisogelea, nakuonyesha kadi ya njano.Nilisema: Siwezi kuzungumza na wewe?”
Kuhusu bao la kwanza walilofungwa Santos, Neymar amesema: “Kwa maoni yangu, ile ilikuwa faulo, ambayo haijapaswa kuwa kona, ambayo walitumia kufunga bao lao. Waamuzi Brazil wanafanya makosa makubwa sana. Hili linapaswa kumalizwa.”
Neymar anaripotiwa alimhoji kocha wake pia, Juan Pablo Vojvoda kabla ya kumtoa uwanjani, ambapo staa huyo wa zamani wa Barcelona na PSG aliripotiwa kuuliza “Unanitoa?” kabla ya kutoka na kuelekea vyumbani.
Santos iliwahi kushuka daraja mara moja tu kabla ya miaka yao 113 ya historia na hili lilitokea 2023 baada ya kuwa na msimu mbaya kabisa. Ilipambana na kupanda daraja msimu uliopita, lakini sasa wamejikuta kwenye mashaka makubwa ya kushuka tena.