Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Van basten mburudishaji anayeangaliwa kwa jicho tofauti AC Milan

Muktasari:

  • Kila kocha na viongozi wamekuwa wanatafuta njia ya kujikwamua wakijikuta mzigo unazidi kuwa mzito na safari kuwa ngumu, na sasa AC Milan inajipapatua imalize msimu ikiwa sio miongoni mwa timu zitazoponea chupuchupu kushuka daraja. Hivi sasa inakamata nafasi za katikati kwenye msimamo wa ligi hiyo.

KWA mara ya kwanza katika kipindi cha miongo minne timu ya AC Milan ambayo ilitawala na kuwa miongoni mwa zilizokuwa kileleni katika Ligi Kuu Italia (Serie A), inafanya vibaya na imewashangaza mashabiki wengi.

Kila kocha na viongozi wamekuwa wanatafuta njia ya kujikwamua wakijikuta mzigo unazidi kuwa mzito na safari kuwa ngumu, na sasa AC Milan inajipapatua imalize msimu ikiwa sio miongoni mwa timu zitazoponea chupuchupu kushuka daraja. Hivi sasa inakamata nafasi za katikati kwenye msimamo wa ligi hiyo.

AC Milan ilipata mafanikio makubwa Ulaya kwa kuwa bingwa wa Italia mara 19 na kushinda makombe mengi, ikivuna ubingwa wa Ulaya mara saba na mara tatu ule wa mabara.

Katika kutafuta ufumbuzi ilimtimua kocha Paulo Fonsesca miezi miwili iliyopita na kumuajiri Sergeo Conceicao ambaye naye yupo hatarini kutimuliwa baada ya matokeo mabaya katika ligi na Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki mbili zilizopita. Milan inafikiria kumuajiri mchezaji wake wa zamani, Marco Van Basten wa Uholanzi aliyestaafu kucheza soka 1995 akiwa na miaka 30 na kuwa kocha wa Uholanzi 2004 hadi 2016.

Basten wiki iliyopita alisema alikuwa anaumia kuIona klabu yake ya zamani ya AC Milan ikiboronga, lakini ana matumaini itarejea katika hali yake ya zamani. Alisema hayo alipoitembelea klabu hiyo na kupokewa kwa shangwe na mashabiki kukumbuka mchango wake.

Nyota huyo ni mchezaji na kocha mwenye rekodi za kuvutia na mawazo ya kipekee katika kuuendeleza mchezo wa kandanda. Miaka mitano iliyopita alipendekeza kufanyika mabadiliko ambayo yangeufanya mchezo wa kandanda kuwa tofauti na sasa.

Katika mapendekezo aliyoyatoa alipokuwa mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (Fifa), Basten  alitaka pasiwepo kuotea wala dakika za nyongeza timu zikiwa sare muda wa mchezo ukimalizika.

Vilevile badala ya mchezo kuwa na dakika 30 za nyongeza mshindi atafutwe kwa penalti tano tofauti na ilivyo sasa. Alishauri wachezaji watano wa kila upande, mmoja baada ya mwingine wapewe mpira mita 25 kutoka golini na kufunga bao ndani ya sekunde nane. Kipa awe huru kukaa atakapo katika eneo la hatari na mchezaji lazima atingishe wavu ndani ya muda huo na ataposhindwa ipulizwe filimbi ya kutofaulu.

Mchezaji awe huru kupiga mpira moja kwa moja au aende golini kukabiliana na kipa, iwe atamlamba chenga na kufunga au atasukuma kombora golini. Basten aliamini hii itamwezesha mchezaji kuonyesha umahiri wa kudhibiti mpira na kupiga chenga, kipa kuonyesha alivyo makini na italeta msisimko kwa watazamaji.

Mapendekezo mengine ni kwa anayecheza rafu asipewe kadi, bali apumzishwe kwa dakika 10 na arejee uwanjani au mchezaji mwingine achukue nafasi yake. Vilevile sheria ya kuongeza muda wa majeruhi itumike kuanzia dakika 10 za mwisho za mchezo.

Mapendekezo mengine ni mchezaji asikae na mpira kama mali yake kwa zaidi ya sekunde 10 na anayefanya hivyo timu yake ipigiwe mpira wa adhabu hapo alipo, mchezo uwe na sehemu nne kama netiboli badala ya mbili za sasa ili wachezaji wasichoke na waweze kucheza kwa ustadi zaidi muda wote.

Mapendekezo ya Basten, mcheaji bora duniani 1992 yalijadiwa na wachezaji, waandishi wa habari, makocha na mashabiki.

Viongozi wa Fifa walisema yangejadiliwa, lakini tangu yalipotolewa haijasema jingine na hii ilitafsiriwa kwamba yalitupwa kapuni.

Wataalamu wa kandanda wanaoheshimika wameyakataa mapendekezo na wengine kusema ni ya kitoto, na yakitumika msisimko wa mchezo utatoweka. Kocha wa Rennes ya Ufaransa, Christian Gourcuff alisema anamheshimu Basten, lakini anayadharau mapendekezo yake kwa vile ni ya kijinga.

“Kuondoa sheria ya kuotea ni kualika vurugu golini na badala ya watu kucheza mpira watapigana vikumbo," alisema.

Kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp alimtaka Basten atafaute mchezo mwingine kuuchezea na si kandanda, na vizuri aanzishe mchezo atakaouita ‘Basten soccer’ yaani kandanda la Basten.

Aliyewahi kuwa kocha wa Chelsea na sasa Juventus, Antonio Conte alisema kandanda ni mchezo wa watu wenye akili na hautaki vurugu kama zinazoonekana katika michezo ya kupigana misuli, ndondi au rage. Basten alivuma miaka ya 1980 na 1990 kwa mabao maridadi, moja likisifiwa kama la pili kwa ubora nusu karne iliyopita.

Alikuwa mwanamichezo bora wa Ulaya 1988, 1989 na 1992 na Fifa ilimtangaza kuwa mchezaji bora wa dunia 1992 na kushika nafasi ya 10 ya wachezaji bora duniani wa karne iliyopita. Basten alifunga mabao 276 katika michezo ya kimataifa hadi alipostaafu kwa maumivu.

Alitumia miguu yote miwili kupiga mashuti makali na alikuwa mjanja wa kutafuta mabao sekunde chache kabla mchezo

kumalizika. Kila timu yake ilipobanwa ndipo alipofanya maajabu na alifunga zaidi ya mabao 20 muhimu sekunde chache kabla ya mchezo kumalizika.

Alizaliwa Oktoba 31, 1964 katika mji wa Utrech, Uholanzi na alipokuwa mdogo alipenda mchezo wa gimnastiki na kutumia ustadi wa mchezo huo kujipinda kubabaisha wachezaji alipokuwa na mpira. Alianza kuchezea Edilwijik ya Utrech na kuchukuliwa na Ajax Amsterdam.

Mchezaji huyo alikuwa mfungaji bora wa Ulaya 1986 akiiwezesha Ajax kuwa bingwa wa Uholanzi mara mbili na kunyakua Kombe la Washindi Ulaya. Akiwa amefunga mabao 128 katika michezo 143 ya ligi na mfungaji bora wa Uholanzi kwa miaka minne,  Silvio Berlusconi aliyekuwa anahaha kuijenga AC Milan iliyoteremshwa daraja mara mbili katika kipindi cha

miaka mitatu alimnunua Basten kuimarisha kikosi chake.

Mchezo wake mmoja unaozungumzwa sana ni wa AC Milan ilipokutana na Cagliari ambayo iliongoza bao 1-0 hadi mapumziko. Filimbi ya kipindi cha pili ilipopulizwa Basten aliingia uwanjani akitabasamu na kuwaonyesha mashabiki vidole vitatu.

Wakati watazamaji wakimzomea Basten alizunguka uwanjani na kupiga kelele "mtayaona". Alijituma ile mbaya katika kipindi cha dakika 18 akitingisha nyavu mara tatu na baadaye kutoa burdani. Mchezo ulipomalizika na matokeo kuwa 3-1, Basten alichukua watoto wawili na kuzunguka nao uwanjani kuashiria mabao matatu aliyofunga.

Mchezaji huyo alistaafu kucheza kama alivyoanza. Alifunga bao lake la kwanza katika ligi ya Italia kipa akiwa Nista Ferron na katika mchezo wake wa mwisho alifunga Nista akiwa analinda nyavu. Alipostaafu 1995 alikataa kufundisha kandanda, lakini baadaye alijiunga na chuo cha makocha wa kandanda cha Uholanzi.

Alichaguliwa kuwa kocha msaidizi wa timu ya daraja la pili ya Ajax 2003 na 2005 akawa timu ya taifa Uholanzi na kuwaondoa wachezaji nyota waliokuwa wanaringa. Miongoni mwa aliowaweka pembeni kwa sababu ya majivuno ni Clarence Seedorf, Patrick Kluivert, Edgar Davids na Roy Makaay.

Basten aliwategemea vijana wa klabu ndogo badala ya wazoefu wa wa Ajax, PSV na Feyenoord. Chini ya uongozi wake Uholanzi hawakufungwa hata mchezo mmoja katika kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia 2006. Hata hivyo, walitolewa na Ureno katika mchujo baada ya kufungwa bao 1-0. Kinachosubiriwa sasa ni je atachukua jukumu la kuifundisha AC Milan na atakuja na maajabu gani? Tusubiri.