Prime
Utata kadi nyekundu Namungo, nahodha asimulia

Muktasari:
- Katika tukio hilo hakuna aliyeelewa kitu gani kilitokea hata mwamuzi Japhet Smarti kutoka Katavi kumpa kadi beki huyo raia wa Burundi, huku baadhi wakihisi labda alitoa lugha chafu, lakini umbali baina ya wawili hao uliondoa dhana hiyo.
WAKATI utata ukiendelea kuzunguka juu ya kadi aliyopewa beki wa Namungo, Erick Mukombozi dhidi ya Simba, nahodha wa timu hiyo, mkongwe Japhet Massawe amefunguka majibu aliyojibiwa na mwamuzi wa mchezo huo mara mwenzake alipoonyeshwa kadi hiyo iliyokuwa gumzo.
Katika tukio hilo hakuna aliyeelewa kitu gani kilitokea hata mwamuzi Japhet Smarti kutoka Katavi kumpa kadi beki huyo raia wa Burundi, huku baadhi wakihisi labda alitoa lugha chafu, lakini umbali baina ya wawili hao uliondoa dhana hiyo.
Mwamuzi huyo alimpa kadi nyekundu ya moja kwa moja Mukombozi baada ya tukio la beki huyo akimdhibiti mshambuliaji wa Simba, Lionel Ateba huku picha za mikanda ya video zikishindwa kuonyesha kosa lolote wakati wawili hao wakipambana uwanjani.
Hata hivyo, mara baada ya mchezo huo Massawe ameliambia Mwanaspoti, mara baada ya Smarti kumtoa kwa kadi hiyo, Mukombozi alimfuata na kumhoji sababu ya maamuzi yake kisha kujibiwa beki huyo Mrundi alimpiga Ateba.
"Nilimfuata mwamuzi nikiwa kama nahodha na kumuuliza imekuwaje amempa kadi nyekundu beki wetu, akanijibu ni kutokana na kumpiga mchezaji wa Simba lakini majibu yake yalizidi kutuchanganya zaidi," alisema Massawe.
"Unajua hatukuona kabisa kama kuna kitu kama hicho kimefanyika, kumbuka Derrick alikuwa eneo la lango letu, lakini hata penalti haikutolewa kama kuna tukio hilo. Hata baada ya mchezo tukajiridhisha hakukuwa na tukio lolote la namna ile basi tumebaki hatujielewi tu na ukiangalia kadi ile iliharibu kila kitu kwetu na kuwapa faida kubwa ya kushinda wapinzani wetu."

MSIKIE MUKOMBOZI
Akizungumzia kitendo cha kadi hiyo, Mukombozi mwenyewe alisema alishangazwa na uamuzi wa mwamuzi huyo kumwonyesha kadi nyekundu, huku akikiri hakuna kosa lolote alilofanya ambalo lingesababisha yeye kutolewa nje.
"Mimi nilishangaa kwa sababu niliona kama maajabu, binafsi naweza kusema haikuwa sahihi na sikustahili kutolewa nje kwa kosa nisilolijua, imeniharibia sana rekodi yangu kwani tangu nimeanza kucheza soka sijawahi kuonyeshwa kadi nyekundu."
Mukombozi aliyerejea tena ndani ya kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari mwaka huu baada ya kukitumikia msimu wa 2023-2024 kisha kuondoka, alisema kupoteza mchezo kulisababishwa pia na kutolewa kwake kwani kuliwavunja moyo wenzake.

SHIDA YA MAAMUZI
Kilio cha maamuzi au waamuzi hazihusishi klabu kubwa peke yake lakini saa karibu ligi nzima mambo yanazidi kuendelea kuharibika.
SIMBA, YANGA NA MAREFA
Wakubwa wawili pale juu ya msimamo wa ligi wao wamejichagulia orodha ya waamuzi watakaochezesha mechi zao peke yao na mabadiliko kwao ni machache sana tena yamekuja hivi karibuni baada ya wadau kuanza kupiga kelele.
Yanga imekuwa ikitembea na waamuzi wake kwenye mechi zao wakiongozwa na Ahmed Arajiga kutoka Manyara aliyechezesha jumla ya mechi tano za timu hiyo msimu huu akiwa ndio mwamuzi aliyechezesha michezo mingi yao.
Nyuma ya Arajiga yumo Abdallah Miwyimkuu na Saad Mrope kila mmoja akipewa mechi tatu,huku Nassoro Mwinchui, Abel William wao wakicheza mechi mbilimbili na wengine waliosalia wakipata mechi moja moja.
Simba nako hali iko hivyo hivyo wakiwa na waamuzi wao ingawa kwao mwamuzi mwenye mechi nyingi ni Shomari Lawi kutoka Kigoma akisimamia mechi tatu akifuatiwa na Hussein Athuman, Omar Mdoe, Japhet Smarti na Kefa Kayombo wote wakichezesha mechi mbilimbili kila mmoja na wengine waliosalia wakipewa mechi moja.
Ni waamuzi watatu pekee ambao wameamua mechi za timu zote mbili msimu huu mpaka sasa ambao ni Nassor Mwinchui, William na Kayoko ambaye aliamua mechi baina ya timu hizo kwenye mzunguko wa kwanza, wengine waliosalia wakibaki kila mmoja na mechi za timu yake.

MAKOSA YA WAAMUZI
Makosa ya waamuzi yameendelea kuwa mengi kwenye mechui mbalimbali za ligi ukiacha hizi za timu kubwa na maeneo makubwa yakiwa kwenye mabao ya kufunga, pia utoaji wa maamuzi ya adhabu kubwa penalti.
TIMU NDOGO ZINALIA
Uliangalia mechi ya Pamba ilipokuwa ugenini dhidi ya Mashujaa makosa ya mwamuzi yalikuwa makubwa akitoa maamuzi yenye utata lakini pia akishindwa kuutunza muda wa mchezo kutokana na watoto waokota mipira kuchelewesha mchezo kwa kukusudia.
BAO LA MKONO LIPO
Beki wa Yanga Ibrahim Hamad 'Bacca' ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga bao safi kwa mkono wake lakini hakuna mwamuzi alikuwa makini kuliona hilo wala adhabu kutolewa baadaye na kuonekana kama kitu cha kawaida.

KADI NYEKUNDU YA UTATA
Mchezo wa Namungo dhidi ya Simba kuna maamuzi ya Smarti mpaka sasa anazidi kuwachanganya hata mashabiki wa wekundu hao kwa hatua ya kumtoa kwa kadi nyekundu beki wa wenyeji Erick Mukombozi akisema beki huyo alimpiga mshambuliaji wa wageni Lionel Atteba lakini kiuhalisia hata yeye akirudia tukio hilo anaweza kujishangaa.
Haya ni matukio ambayo yanaonyesha wazi kwamba endapo akili ya viongozi na wasimamizi wa ligi ambao ni bodi ya ligi wasiposimama imara ligi inaweza kuzalisha bingwa na hata kuzishusha timu pasipo halali.
ADHABU NYEPESI
Adhabu nyingi za waamuzi zimekuwa ni kufungiwa mizunguko kadhaa kisha wanarudi, hizi zimeshakuwa ni kitu ambacho hakiwapi presha waamuzi kwa kuwa wanajua wanaweza kufanya makosa na bado wakarudi baadaye.
Adhabu hizi ni hatari kwa kuwa endapo makosa ya waamuzi yanaweza kuwa yanahusisha ushawishi wa fedha, mwamuzi anaweza kufanya yake kisha akijua hataathirika na lolote kwa kuwa tayari ana motisha kubwa ambayo itamfuta jasho wakati anatumikia adhabu hiyo.
NAULI YA BASI, WANAPANDA NDEGE
Shirikisho la Soka linatoa nauli kwa waamuzi kupanda basi lakini uhalisia waamuzi wengi wanaochezesha mechi za klabu kubwa hizi mbili hawatumii usafiri huo wanatumia ndege kufika maeneo ambayo yanasafari za ndege.
Swali rahisi ni inawezekanaje mwamuzi akasafiri kwa ndege kwa fedha yake alafu akubali kurudishiwa nauli ya bei ya basi? Nani anafidia hiyo tofauti ya bei ya huo usafiri wa ndege ambao ni gharama kubwa?
MABOSI WA MAAMUZI
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Nassoro Hamduni, alisema ikiwa beki huyo wa kati wa Namungo, Derrick Mukombozi itagundulika hakuwa na kosa lolote kadi yake nyekundu itafutwa, kama zilivyokuwa pia kwa wengine.
"Waamuzi ni binadamu kama ilivyokuwa mimi na wewe pia, shida inayokuja ni presha iliyopo kwa mashabiki wa Yanga na Simba ambao kiuhalisia hakuna anayependa kuona timu anayoshabikia ikipoteza, tunapaswa tuheshimu mpira wetu hapa ulipofikia."
Hamduni alisema licha ya matatizo mbalimbali ya waamuzi kujirudia ila wanapaswa pia kupewa pongezi, kwani hawawezi kuwa timilifu siku zote, huku akieleza tukio linalotokea uwanjani ni la mara moja na hana uwezo wa kuangalia marudio tena.

"Watu wanashindwa kuelewa unapokuwa uwanjani ni tukio la mara moja na hupati nafasi ya kurudia tena, sasa ikitokea kwa mwamuzi anabeba lawama lakini ukiangalia kiuhalisia ni ngumu, tulipofika leo tunahitaji kuwatia moyo kuliko kuwakatisha tamaa."
Kagera vs Yanga -Abel William Arusha
Kengold vs Yanga -Abdallah Mwinyimkuu
Yanga vs KMC -Ahmed Arajiga
Yanga vs Pamba-Saady Mrope-Dodoma
Simba vs Yanga-Ramadhan Kayoko
Yanga vs JKT -Ahmed Arajiga
Coastal Union vs Yanga- Abel William
Singida Black Stars vs Yanga -Ally Mnyupe-Moro
Yanga vs Azam-Ahmed Arajiga
Yanga vs Tabora- Nassoro Mwinchui
Namungo vs Yanga -Abdallah Mwinyimkuu
Yanga vs Mashujaa-Saady Mrope-Dodoma
Yanga vs Prisons-Abdallah Mwinyimkuu
Dodoma vs Yanga -Ahmed Arajiga
Yanga vs Fountain Gate -Thabit Maniamba
Yanga vs Kagera -Nassoro Mwinchui
Yanga vs KenGold -Wilson Masea Mwanza
Yanga vs JKT Tanzania-Ahmed Arajiga -Manyara
KMC vs Yanga-Isihaka Mwalile -DSM
Yanga vs Singida-Saad Mrope-Dodoma
Simba
Simba vs Tabora -Nassoro Mwinchui
Simba vs Fountain Gate-Shomari Lawi
Azam vs Simba-Heri Sasii
Dodoma vs Simba -Omar Mdoe
Simba vs Coastal union-Japhet Smart-Katavi
Simba vs Yanga -Ramadhan Kayoko
Prisons vs Simba -Amina Kyando
Simba vs Namungo-Hussein Athuman-Katavi
Mashujaa vs Simba-omar Mdoe
Simba vs KMC -Shomari Lawi
Simba vs Kengold-Ester Adalbert -Singida
Kagera vs Simba-Tatu Malogo
Simba vs JKT Tanzania- Kefa Kayombo
Pamba vs Simba-Hussein Katanga-Tabora
Singida vs Simba-Shomari Lawi
Tabora vs Simba-Kefa Kayombo-Mbeya
Fountain Gate vs Simba- Abel William
Simba vs Prisons-Hussein Athuman -Katavi
Namungo vs Simba- Japhet Smart -Katavi