Usicheke! Hata Man Utd inaweza kubeba EPL msimu huu
Muktasari:
- Hata kipindi hicho, Arsenal ndiyo iliyokuwa ikiongoza msimamo wa ligi, kama ilivyo kwa sasa. Kama hilo ndilo linalotazamwa na wacheza kamari, basi kocha Amorim anaweza kuduwaza wengi msimu huu. Usicheke!
LONDON, ENGLAND: NENO la onyo. Kinachosemwa ni kwamba kwenye soka namba zinaweza kutumika kutoa taswira ya kitu kinachoweza kwenda kutokea au ambacho hakiwezi kwenda kutokea.
Wanasema namba hazidanganyi. Lakini, wakati huu wakati Ligi Kuu England ikiwa imesimama, ni wakati wa kutazama kilichopo nyuma ya namba hizo, wakati kwenye ligi kila timu ikiwa imecheza mechi 11.
Sambamba na hilo, umetazamwa pia msimamo wa ligi unavyosoma na kilichobebwa kwenye historia kutokana na msimamo ulivyo. Majibu ni haya.
Msimu 16 kati ya 33 iliyopita, timu iliyokuwa ikiongoza ligi baada ya mechi 11, ilikwenda kushinda ubingwa. Hiyo ina maana, kwa misimu 17, timu ambayo ilikuwa kileleni kwenye msimamo wa ligi baada ya mechi 11, ilishindwa kuwa bingwa wa Ligi Kuu England.
Na timu iliyohusika mara tano kati ya hizo 17, ni Arsenal.
Timu ya mwisho iliyoshindwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kuwa kileleni katika mechi 11 za kwanza ni Arsenal.
Kipindi kama hiki msimu wa 2022/23, Arsenal ilikuwa ikiongoza ligi kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya timu inayoshika namba mbili, Manchester City, ambao ndiyo waliokwenda kubeba ubingwa. Na msimu huu, Arsenal inaongoza ligi kwa tofauti na pointi nne dhidi ya Man City.
Kwa maana hiyo, je takwimu zitumike kubashiri bingwa wa msimu huu? Ukweli unabaika wazi, kuongoza ligi baada ya mechi 11 za kwanza kwenye ligi, hiyo halina maana utashinda ubingwa.
Kwa hesabu za pointi, nafasi ya chini zaidi ya timu inayoweza kuchukua ubingwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu ni hadi ile inayoshika namba nane.
Na hilo kwenye historia ya Ligi Ku England, limewahi kutokea mara mbili, timu inayoshika namba nane baada ya mechi 11 za kwanza, ilikwenda kunyakua ubingwa wa ligi.
Na ndio maana, timu tano zenye pointi 18 kwenye msimamo kwa sasa, hazijawekwa kando kwenye mbio za ubingwa. Na ndio maana, Manchester United haiwezi kuwekwa kando kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Man United haiko kwenye Kombe la Ligi na michuano ya Ulaya, hivyo kocha Ruben Amorim kazi yake itakuwa kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England pekee na itakuwa na mechi 10 za ligi tu ndani ya wiki saba zijazo.
Man United kwenye mechi 10 zijazo kwenye ligi, itacheza na timu zinashika nafasi ya 13, 10, 18, 20, 9, 6, 14, 20, 16 na 17.
Man United itacheza na Wolves mara mbili ndani ya wiki tatu za Desemba. Mechi zao tano zijazo za ugenini, moja tu ndiyo itakuwa ya umbali mkubwa. Mechi yao ya ugenini dhidi ya Crystal Palace itafuatiwa na Wolves, Aston Villa, Leeds na Burnley.
Kwenye namba, mechi hizo za Man United zinaipa faida kubwa dhidi ya timu zile zinazocheza michuano ya Ulaya na zilizopo bado kwenye Kombe la Ligi.
Sawa, timu hizo zina vikosi imara kuliko alichonacho Amorim, lakini viwango vya Bryan Mbeumo na Matheus Cunha pamoja na kipa Senne Lammens, vinaipa Man United nguvu ya ziada ya kuwapo kwenye vita.
Mechi zao mbili za mwisho kwenye mechi tano ilizocheza bila ya kupoteza zilimalizika kwa sare ya 2-2 dhidi ya Tottenham na Nottingham Forest.
Man United sasa inaonekana kuwa kwenye kiwango kizuri na wachezaji wameshaanza kuzoea na kufurahia mfumo wa kocha.
Na hilo ni jambo zuri kwenye vita ya ubingwa. Wacheza kamari hawataki kuifuta Man United kwenye mbio za ubingwa, huku wakiamini kutokuwa na presha ya mechi nyingi na kuwekeza tu kwenye Ligi Kuu England kinaipa nafasi ya timu hiyo kunyakua taji hilo kwa msimu huu.
Na kitu usichokijua, timu hizo mbili ambazo zilizidiwa pointi nane na timu vinara kwenye Ligi Kuu England baada ya mechi 11 zilizokwenda kunyakua ubingwa wa ligi hiyo mwisho wa msimu, ya hivi karibuni ilikuwa katika msimu wa 2002/3, Man United.
Hata kipindi hicho, Arsenal ndiyo iliyokuwa ikiongoza msimamo wa ligi, kama ilivyo kwa sasa. Kama hilo ndilo linalotazamwa na wacheza kamari, basi kocha Amorim anaweza kuduwaza wengi msimu huu. Usicheke!