Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unaukumbuka ule mkoko wa Kiduku? Sikia anachosema -1

KIDUKU Pict

Muktasari:

  • Kiduku aliyeanza kupigana Mei 25, 2013 katika uzito wa Super Middle, anashika nafasi ya 159 duniani kati ya mabondia 1,801 wa uzito huo, huku kwa hapa nchini akishika namba mbili kati ya mabondia 42.

“SIPIGANI ili watu au mashabiki wangu waone napigana napigana, (ila) kwa maslahi hivyo ndivyo watu wanatakiwa kufahamu. Binadamu saizi wanatamani kuona napigana halafu baadaye wakiona sina kitu hao wao watazungumza pia

“Ukiondoa hilo la kuhitaji maslahi ili nipigane pia kuna tatizo la waandaaji akitokea akiniambia kiasi kilichopo nitapambana na mtaniona, lakini siyo kila mwandaaji akija na kiasi chochote napanda ulingoni, hapana. Naangalia maslahi yangu pia hilo hata nikipigana najua nini nutaambulia ...baada ya hapo na nitaacha alama gani,” ni sehemu ya maneno ya bondia Twaha Kassim 'Twaha Kiduku'.

Mwanaspoti limebahatika kupiga stori mbili tatu na na bondia huyo baada ya kumfungia safari kutoka Dar es Salaam hadi mji kasoro bahari, Morogoro, ambako Kiduku anaishi, na amezungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzitaja chips mayai kama sehemu ya mafanikio makubwa kwenye ushindi wa mapambano yake.

Kiduku aliyeanza kupigana Mei 25, 2013 katika uzito wa Super Middle, anashika nafasi ya 159 duniani kati ya mabondia 1,801 wa uzito huo, huku kwa hapa nchini akishika namba mbili kati ya mabondia 42.

Mwamba huyo kutoka mji kasoro bahari amepigana katika mapambano 37 sawa na raundi 263, akishinda 26 huku 10 ikiwa ni knockout ilhali amepegwa mara 10 na ni mara moja tu amedundwa kwa KO, akiwa na sare 1.

Bondia huyo ambaye mara ya mwisho alizipiga na bondia wa Malawi, Alick Mwenda, Julai 26, 2025 na kumchapa, itakumbukwa vyema pambano lake dhidi ya Dullah Mbambe ambalo alimtwanga Mbabe kwa pointi na kuzawadiwa gari aina ya Toyota Crown lilifanyika Agosti 20, 2021, jijini Dar es Salaam, ushindi ambao ulimfanya mashabiki wake 'wajimwaye' vilivyo kuanzia Dar hadi Moro kumsindikiza nyumbani akiwa na mkoko wake huo.

Kama hukumbuki vizuri ni kwamba, kabla ya pambano hilo mabondia hao walitambiana kwa muda mrefu, huku kila mmoja akidai kuwa zaidi ya mwenzake katika masumbwi na hilo likaja na majibu siku ya siku walipokutana katika ukumbi wa Ubungo Plaza na kukata mzizi wa fitina wana Moro wakiondoka wakishangilia.

Na baada ya Kiduku kuondoka na mkoko wake, aliendelea kutamba nao huko Moro ukimtambulisha kuwa mbambe wa Mbabe - ukiwa kama alama ya namna alivyojipanga kuzimisha tambo za mpinzani wake huyo.

KIDU 01

ZAWADI YA GARI

Ingawa kuna mengi yalizungumzwa baada ya Kiduku kuibuka mshindi dhidi ya Mbabe na kukabidhiwa zawadi ya gari hilo, lakini akijibu swali la Mwanaspoti la kulikoni makubaliano yalikuwa mshindi azawadiwe gari badala ya fedha, na mwenyewe ana kitu cha kusema.

“Kwanza swali zuri sana kwa sababu nataka kuwafahamisha Watanzania hata mabondia wengine ambao walikuwa wanahoji yaani bondia anapigania gari... hauwezi mtu ukapanda ulingoni kushindania gari ipo hivi kilichotokea pale sawasawa kama unavyowekwa mkanda yaani promota akiongea na Dullah hili pambano unacheza kwa bei gani - elfu mbili mia tano na Twaha shilingi ngapi? Elfu moja, hivyo mshindi pale anapata kile alichokiomba kabla ya pambano,” anasema bondia huyo.

Twaha Kiduku anasema lile gari lilikuwa kama zawadi kwa ajili ya mshindi huku akibainisha kuwa gari hata lisingekuwepo bado mshindi angepatikana na kupata alichostahili hivyo wasingeweza kukataa.

Baada ya ushindi na kupata zawadi ya gari aina, Kiduku anasema aliliuza na kununua nyumba kwa ajili ya wapangaji na anafurahia mambo mengine yanavyomwendwa vizuri kimaisha.

“Mimi sio muumini wa kuwa na magari mengi sasa natembelea IST hiyo Crown niliiuza, niliamini itaweza kuniletea mabalaa kwa sababu itahitaji matengenezo. Nilichofanya nilifanya biashara (kuiuza) na kuongeza nyumba ya wapangaji,” anasema

“Naamini katika uwekezaji, kuna maisha baada ya mapambano, hivyo naamini asset (rasilimali) ya nyumba itanipa pesa ya kula na kuishi nje ya kupigana.”

KIDU 02

PAMBANO BORA, YEYOTE AJE

Kiduku amefanikiwa kupambana na mabondia wengi wa ndani na nje ya nchi, lakini analitaja pambano lake dhidi ya Dullah Mbabe kuwa ndilo bora na lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuupaisha mchezo huo kwa wadau kuanza kuupenda na kuufuatilia.

Pambano hilo lilikuwa ni moja kati ya mapambano ya kisasa yenye upinzani mkubwa ambalo lilishuhudiwa na kizazi kilichozaliwa miaka ya 2000 tofauti na wakati wa upinzani wake na kina Francis Cheka, Rashid Mtamla au Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo'.

“Nimepigana mapambano mengi, lakini kwangu pambano bora ni dhidi ya Mbabe, lilikuwa bora na kuibua hisia za wadau kupenda kufuatilia ngumi... ni lile pambano la Toyota Crown. Hadi sasa hakuna dabi iliyowahi kutokea na kusisimia kama dabi yangu na Mbabe, japo kuna fight (mapambano) zinajaribu, lakini hazijafikia. Nakiri kuwa hili ni pambano bora,” anasema.

Licha ya kukutana na mabondia wengi huku wengine wakimshinda, lakini Kiduku anasema yupo tayari kupambana na bondia yeyote ila kikubwa ni maslahi kwani hakuna anayemhofia.

“Kweli nimekutana na mabondia wengi, kuhusu ninayetamani kurudiana naye siwezi kumtaja hapa yeyote freshi kitatokea kama kilichomkuta Mbabe kwani baada ya sare kwenye pambano lililokuwa limeteka hisia za mashabiki tulirudiana nikampiga,” anasema na kuongeza:

“Sichagui silaha kama nilivyosema, mtu ambaye niliamua kurudiana naye baada ya sare ni Mbabe ambaye baada ya marudiano nikampiga, hivyo nipo tayari kupambana na bondia mwingine yeyote.”

KIDU 06

NGUMI YA KUVUNJA MKONO

Kila kilicho na mafanikio hakikosi changamoto, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mengi kutokea kwa binadamu kwenye majukumu ya utafutaji kama anavyodai Kiduku anayesema alishawahi kuvunjika mkono akiwa jukwaani.

“Nakumbuka ni miaka mingi imepita, lakini kabla ya Azam kuanza kuonyesha ngumi nilicheza pambano na Mkongomani nimemsahau jina, kitu kama raundi ya tatu au ya nne nilimpiga ngumi mkono wangu ukavunjika,” anasema bondia huyo.

“Mfupa ulivunjika kabisa, hivyo ikaniwia vigumu kutumia mkono wangu wa kulia ikanilazimu nitumie wa kushoto... nashukuru Mungu niliibuka na ushindi kwenye hilo pambano.”

KIDU 03

SINDANO HAPANA, DAWA KISADO

Kiduku amekwepa mishale mingi awapo ulingoni, lakini aliwahi kukutana na ngumi zenye uzito mkubwa na kupambana nazo. Hata hivyo anadai kuwa ni mwoga wa kuchomwa sindano bora katika matibabu na ni bora apewe kisado cha dawa anaweza  kuzimeza, ila sio sindano.

Anasema haogopi ngumi za mabondia wenzake anaokutana nao, lakini linapokuja suala la kuchomwa sindano akienda hospitali ni mwoga.

“Kuchoma sindano daaah! Ni mtihani sana, yaani kivumbi dawa hata ukiniletea kisado nitameza zote, ila kitu kinaitwa sindano nakiogopa sana,” anasema Twaha Kiduku ambaye licha ya kuwa na familia anasema hana mtoto ambaye ni bondia na haoni atakayefuata nyayo zake.

KIDU 04 (1)

CHIPS YAI FRESH TU

Wakati chips mayai hasa kwa mtoto wa kiume huko mitaani kuna utani unaodai kuwa wanaokula ni 'watoto wa mama', kwa upande wa Kiduku anaikana kauli hiyo akisema anashangazwa na watu wanaodharau chakula hicho.

“Wanazidharau chips mayai, hazipigani wanapigana watu na watu wakitaka kujua ni chakula kizuri wafanye mazoezi yake wakute yanayotajwa kwenye chips ya uzuri wake,” anasema na kuongeza:

“Ukiondoa (kupenda kula) chips siku ya pambano naamka mapema nakunywa supu asubuhi, nalala mchana, ndio nakula chips yai licha ya watu kudharau eti wanakula wanaume wa Dar... kuleni na mfanye mazoezi. Siku moja kabla ya pambano ratiba yangu huwa ni kupumzika sana ili kuuweka mwili katika hali nzuri ya kiushindani, hivyo nikula na kulala nakuwa sina ratiba yoyote."

Inaelezwa kwamba ili kumuepusha bondia kupatwa na shida ya akili anatakiwa kupata muda mwingi wa kupumzika baada ya kumaliza pambano, lakini Kiduku anatolea ufafanuzi suala hilo akisema, “bondia anatakiwa kupumzika wiki mbili tu siku chache baada ya kutoka kupambana. Hapaswi kupumzika sana, anatakiwa kurudi kambini na kuendelea na maandalizi kwa ajili ya pambano lingine."

KIDU 07

KUIGIZA HADI NGUMI

Sio kila binadamu amefanikiwa kupitia kile ambacho alitamani kukifanya awali, japokuwa kuna wengine wamepata bahati hiyo. Kwa upande wa Kiduku anasema licha ya kuanza na sanaa nyingine tofauti, lakini ngumi ndizo zimemtambulisha.

“Mimi nilianza kuigiza kabla ya kuanza kupigana. Mbali na kuigiza pia nilikuwa mpiga ngoma za asili, Dj, msanii wa muziki wa singeli kipindi cha Msagasumu. Wakitokea waandaaji wakitaka nishiriki nipo tayari na naendelea kufanya hivyo. Hivi karibuni kuna msanii alinifuata nifanye naye kazi, nilifanya hivyo (ngoma) ipo YouTube inaonyeshwa huko,” anasema.

Akizungumzia suala la U-dj, Kiduku anasema hajawahi kufikiria kurudi kwenye fani hiyo kwani anaamini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa tofauti na miaka ya nyuma. Ili aweze kuendana na waliopo sasa itampasa arudi darasani kusoma.

“U-dj nimeshamalizana nao kwa sababu kipindi hicho vifaa tulivyokuwa tunatumia na sasa kuna utofauti kabisa. Kwa mfano saizi wanatumia laptop, mimi sina ufundi huo, itanilazimu nirudi darasani siwezi kufanya hivyo.

“Kuhusu kuimba nimefanya hivyo kweli na nilishawahi kutoa wimbo na video yake kabisa unaitwa Marhaba upo, nakumbuka kuna kipindi (studio za) Wasafi waliupiga sana kwenye media yao.”

Anasema watu wengi baada ya kuusikia huo wimbo ukipigwa walimfuata na kumwambia kuwa wameandaa tamasha wakimuomba akatumbuize, lakini aliwakatalia kwa sababu sasa haoni kama anaweza kuimba tena, labda kuigiza.

KIDU 04

KUMZIMISHA BONDIA ULINGONI

Kwenye majukumu ya kawaida ya binadamu huwa anakutana na mafanikiko na changamoto kama anavyothibitisha Kiduku kuwa alipata pambano nchini Zambia na licha ya kushinda aliingiwa na huzuni kutokana na kumpiga mpinzani hadi kuzimia.

“Zambia nilishawahi kupigana na bondia nikamzimisha ulingoni, na alizimia vibaya. Nilijisikia vibaya sana na baada ya kufanikiwa kuzinduka alilia sana, sijui alisajiliwa lini lakini alilia nikamwambia (ni) kawaida kuna kushinda na kushindwa,” anasema na kuongeza:

“Kwenye pambano hilo nilikuwa napoteza mimi, raundi ya tatu lilikuwa la raundi sita, lakini mambo yalibadilika nilimpiga akazimia. Baada ya kutoka pale alilia. Wakati analia mimi niliumia sana. Nilivyopata rekodi yake niliambiwa kuwa kwenye mapambano yake yote amekuwa akishinda kwa KO na yeye kapigwa mapambano matatu yote kapigwa KO.”


KO HAIPANGWI, INATOKEA

Pale mabondia wanapopanda ulingoni ama katika pambano la kuwania ubingwa au hata kumaliza ubishi, mashabiki wengi hupenda kuona mmoja akipigwa KO au TKO, ingawa baadhi hupenda kushuhudia pambano likimalizika kwa raundi zote ili waendelee kuona ngumi zikipigwa, lakini Kiduku anasema sio rahisi.

“Mimi napenda kumpiga (mtu) KO, lakini kwa mchezo wenyewe kushinda TKO inatokea tu kwa juhudi na maandalizi yaliyofanywa na bondia husika ambaye ameibuka na ushindi, lakini KO haipangwi,” anasema na kuongeza:

“Kila bondia, sio mashabiki tu kuona tunashinda kwa KO, lakini mambo yanatokea tofauti uwanjani. Tukiacha tamaa au kubishana na ndondi ni mchezo wa kujitapa kwa aina yake, lakini ukweli ni kwamba KO haipangwi.”


MIKANDA TISA NDANI

Ili kupima mafanikio kwenye kila jambo kinachoangaliwa ni mikanda na kwa upande wa mabondia wakati kwa wanasoka ni medali na mataji, Kiduku anazungumzia mafanikio yake kwa kutaja idadi ya mikanda aliyo nayo ndani.

“Nina mikanda tisa ndani, yote ni yangu. Lakini mtu akitaka kuupambania naongea na promota ambaye atatangaza pambano tutaupambania tena. Sina mkanda ambao natakiwa kuutafutia pambano ili nisije nikaupoteza baada ya kukaa nao muda mrefu.

“Nina mkanda wa WBO, WBC, WBA, ABU, WBF, IBF, PST, TPBRC na kuna mikanda mingine mingi ya Tanzania,” anasema Kiduku ambaye pia alifanya kuwepo kwa msemo wa "mlingoti chuma na bendera chuma" kutokana na morali na kuungumza mpaka maneno hayo yamekuwa gumzo hadi sasa.