Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfaume, Class hapana! Mixer ya majaji fresh

NGUMI Pict

Muktasari:

  • Ajabu ni kwamba yote yalifanyika katika Wilaya ya Kinondoni, ambapo Knockout ya Mama Season 5 ambayo iliandaliwa na promosheni ya Mafia Boxing Promotion ilifanyika kwenye Viwanja vya Posta Kijitonyama.

WIKIENDI iliyopita Jiji la Dar es Salaam lilipambwa na matukio mawili makubwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa.

Ajabu ni kwamba yote yalifanyika katika Wilaya ya Kinondoni, ambapo Knockout ya Mama Season 5 ambayo iliandaliwa na promosheni ya Mafia Boxing Promotion ilifanyika kwenye Viwanja vya Posta Kijitonyama.

Wakati huo kwenye Viwanja vya Leaders Club nako kulikuwa kunawaka moto wa ngumi ambazo ziliandaliwa na Promosheni ya Peak Time Media. Pamoja na utamu ulioambatana na mapambano hayo, lakini kulikuwa na sintifahamu flani zilizowaacha mashabiki vinywa wazi.

NGU 01

MFAUME, CLASS WATEMBELEA MBELEKO

Licha kuonekana kwa ukubwa na mashabiki wa mchezo wa ngumi nchini hasa kupitia runinga, lakini dosari iliyojitokeza imehusisha kundi la waamuzi waliosimamia pambano hilo kwa kutoa uamuzi ulioonekana kuwa mbovu katika baadhi ya matukio muhimu.

Katika mitandao ya kijamii pambano la Ibrahim Class dhidi ya Nasibu Ramadhani ambalo lilikuwa la marudiano limechukuliwa tofauti na matarajio ya wengi kutokana na matokeo yaliyotolewa na majaji. Haijulikani nini kilichokuwa nyuma ya pazia kulifanya kuwa sare badala ya ushindi kwa Nasibu.

Pambano hilo liliamuliwa kwa matokeo ya sare ya ajabu kwani kila aliyeangalia pambano hilo, anakiri kuwa Class alikutana na kipigo isipokuwa waamuzi wa pambano waliamua kutoa sare. Nasibu, hakuficha hisia zake juu ya matokeo hayo kwa kuwa alitamka kuwa majaji na waamuzi wa pambano lake hilo wote watakwenda motoni kwa matokeo yaliyotolewa.

Lakini, upande wa Class kukubali kuomba kurudiana na Nasibu inaonyesha kutotosheleza ikionyesha hakupaswa kupewa matokeo ya sare na mwenyewe akasisitiza hakuwa na siku nzuri kazini.

NGU 03

Ukiondoa maajabu ya pambano hilo, kituko kingine kilichotokea ni upande wa bondia Mfaume Mfaume wa Naccoz ya Mabibo aliyepewa ushindi ilhali ilionekana wazi kwamba alipigwa. Kabla ya pambano hilo mara ya mwisho Mfaume kupanda ulingoni ilikuwa Juni 26, 2023 ambapo imepita miaka miwili bila kupigana, lakini mara zote amekuwa akizungumzia kuwa ni bondia hatari.

Katika pambano lake la raundi 10 dhidi ya Kudakwache Banda wa Malawi ambalo alipigana kwenye uzani wa middle badala ya walter aliouzoea miaka mingi, Mfaume alionekana kuchapwa katika raundi nyingi kiasi kwamba muda mwingi mashabiki ukumbini hawakuwa wakimshangilia na mwishoni mwishoni walianza kumshangilia Banda kutokana na namna alivyokuwa akimshushia vipigo Mtanzania huyo.

Awali, mashabiki wengi walikuwa na hamu kumuona Mfaume kutokana kukaa muda mrefu nje ya mchezo huo, lakini matokeo yake ya ‘kubebwa’ yalionekana kuwakatisha tamaa  na miongoni mwao kujawa na hasira kutokana na kuamini kwamba alipigwa, badala yake akapewa ushindi ambao bado umekuwa na maswali.

NGU 04

Katika raundi 10 walizopigana kwenye pambano hilo, Mfaume ni kama aliambulia raundi mbili pekee za ushindi, lakini zilizobaki zote alikuwa amepigwa.

Mdau wa ngumi, Bwanausi Rajab anasema ni aibu kwa mabondia kubebwa katika nchi yao kwa sababu mchezo wa ngumi unaonyeshwa hadharani, hivyo kama Taifa hususan katika pambano dhidi ya Banda limedharirika.

“Tumeaibisha nchi yetu kwa kumbeba mtu ambaye ni wazi kabisa alipigwa. Sikia, kila mtu aliyeangalia pale ukumbini aliona kwani yule bondia wetu hakuna aliyekuwa anamshangilia utadhani yupo ugenini, lakini mwisho wa gemu eti akapewa ushindi. Ile ni aibu kubwa,” anasema Rajab.

Alisema kwamba inapaswa majaji walioamua pambano hilo waangaliwe kwa jicho tofauti kwa sababu ndiyo waliosababisha matokeo yaliyoaibisha nchi katika uso wa kimataifa.

“Mchezo huo ulikuwa unarushwa laivu kila kona duniani, fikiria huko nje ya nchi waliotazama wanatufikiriaje Watanzania? Je kuna bondia mwenye akili zake anayeweza kuja akiamini kwamba anakuja kupigana hapa Tanzania ana haki akapata? Hakika tumeaibika.”

Mwajabu Rashid, bondia chipukizi alisema inawezekana kilichofanyika ni uzalendo kuonyesha kwamba Tanzania imejaliwa mabondia bora, huku akisisitiza kwamba katika ngumi mtu anapokuwa nyumbani ni nadra sana kupoteza pambano labda majaji watoke nje ya taifa lake.

“Mimi ndiyo nimeanza tu mazoezi na kujifunza funza kuhusu ngumi, lakini ukisikiliza simulizi utasikia kwamba hata wale wakongwe ambao wengine wameshastaafu walipokuwa ulingoni huko (nje) walikokuwa wanaenda kupigana ni nadra sana walirudi na ushindi,” anasema Mwajabu.

NGU 02

MIXER YA MAJAJI HAINA LONGOLONGO

Wakati wadau wa ngumi wakilalamikia kubebwa kwa mabondia hao, lakini katika Viwanja vya Posta Kijitonyama mapambano yalimalizika na utamu wake.

Ibrahim Mafia alifanikiwa kushinda kwa Knockout ya raundi ya 10 dhidi ya Aliu Lasisi kutoka Nigeria katika pambano la kutetea ubingwa wa WBC Africa ambalo lilisimamiwa na waamuzi kutoka Uganda, Nigeria, Afrika Kusini na Tanzania.

Twaha Kiduku alishinda kwa TKO ya raundi ya tatu dhidi ya Alick Mwenda wa Malawi na kutetea ubingwa wa PST, lakini Idd Pialali akafanikiwa kushinda kwa pointi dhidi ya Limbani Masamba, huku Salmin Kassim hakutaka mambo mengi kwani raundi ya tatu ilitosha kumpa ubingwa wa WBO Africa kwa kumchapa Knockout mpinzani wake Damien Zannou kutoka Benin katika pambano ambalo lilisimamiwa na waamuzi na majaji kutoka Ghana, Namibia na Tanzania.

Ni Kalolo Amir peke yake aliyepoteza pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa WBO Youth kwa pointi mbele ya Jonathan Kasheeta kutoka Namibia, huku Yusuph Changarawe akimchapa kwa Knockout ya raundi ya tatu William Chedy ilhali Asemahle Wellem akashinda kwa TKO ya raundi ya nane Rasheed Idowu wa Nigeria.

Mwingine alikuwa Abdurhaman Magoma ambaye alimchapa kwa Knockout ya raundi tatu Aubrey Masamba wa Zambia wakati Said Hakim akimchapa kwa pointi Bakari Bakari huku Kato Machemba akishinda kwa pointi mbele ya Kamal Singh wa India.