IBRAHIM MAFIA: Kutoka kuuza chipsi hadi bingwa wa WBC Afrika
Muktasari:
- Mafia ambaye ni bingwa wa WBC Afrika akiwa ni bondia wa pili wa Tanzania kushikilia ubingwa huo baada ya Fadhili Majiha, amekuwa ni Mtanzania pekee aliyetetea mkanda huo.
ANGA la mchezo wa ngumi za kulipwa duniani limeanza kulitaja jina la kijana wa Kitanga, Mtanzania, Ibrahim Mafia 'Knockout Master' baada ya kuweka rekodi mpya ya kupanda viwango vya Baraza la Ngumi duniani hadi kwenye 10 bora.
Mafia ambaye ni bingwa wa WBC Afrika akiwa ni bondia wa pili wa Tanzania kushikilia ubingwa huo baada ya Fadhili Majiha, amekuwa ni Mtanzania pekee aliyetetea mkanda huo.
Bondia huyo kutajwa kupanda kwake kwenye viwango vya WBC hadi kufika nafasi ya 10 siyo jambo jepesi, kwani alianza kwenye nafasi ya 17 kati ya mabondia 40 na kisha akapanda hadi nafasi ya 13 na sasa ni wa 10.
Kupanda kwake kumetokana na ushindi wake wa mwisho wa Julai 26, mwaka huu dhidi ya Alliu Bamidele Lasisi wa Nigeria aliyemchapa kwa Knockout ya raundi ya tisa katika pambano la raundi 10.
Mafia ambaye kwa sasa anajiandaa kupanda ulingoni Septemba 27, mwaka huu katika pambano lingine la 'Knockout ya Mama' ambalo atawania mkanda wa ubingwa wa WBC International ikiwa ni mara ya kwanza kuchezwa tangu nchi ipate uhuru.
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 14, akishinda 13, tisa kwa Knockout na sare moja.
Rekodi inaonyesha Mafia anashika nafasi ya pili katika uzani wa bantam nchini ambao una jumla ya 65 wakati Afrika akiwa bondia wa tatu kati ya 155 huku duniani akiwa wa 22 kati ya 1170.
Bondia huyo anasimulia safari yake ya kuwa Ibrahim Mafia illipitia vikwazo kutokana na familia aliyotokea akiwa mtoto pekee wa kiume kati ya wanne.
Anasema baba yake ni mtu mwenye kipato cha kawaida na alikuwa akijishughulisha na kazi ya uzaji wa chips ambayo alikuwa akimsaidia.
"Unajua wakati huo ndiyo nilikuwa naenda kumsaidia baba katika biashara ambayo kwa pale Tanga, Makorora kuanzia saa 10 jioni hadi saa sita usiku.
"Wakati nafanya kazi ya kumsaidia baba, nilikuwa nasoma sekondari hivyo nikitoka shule ndiyo naenda kwenye biashara ya baba kumsaidia, pia nilikuwa na muda wa kwenda madrasa kusoma dini.
"Muda ulivyokuwa unaenda, kuna rafiki yangu ndiye alinishawishi kwa sababu alikuwa ameanza kujifunza kwa kocha Hamis Mwakinyo kwenye gym yake.
"Kiukweli nilianza kufanya mazoezi kwa kuijiba na muda wa kwenda kumsaidia baba ukawa umepungua, baba alivyoona siendi mara kwa mara ilibidi anichunguze na alivyogundua akanizuia lakini sikuweza kuacha.
"Nakumbuka wakati naenda kucheza pambano la kwanza nilikuwa kidato cha nne, shule nilitoroka ili jioni niende kupigana na baada ya hapo baba yangu ndiyo alijua nimekuwa bondia kwa sababu watu walimpelekea video zangu, mwisho wa siku aliniruhusu."
Nani alikupeleka Mafia Boxing?
"Mafia sikupelekwa na mtu yeyote ila kilichotokea wakati nafanya mazoezi kwa kocha Hamisi Mwakinyo, mkurugenzi wa Mafia alikuwa anakuja sana kuangalia mazoezi mara kwa mara akavutiwa na uwezo wangu.
"Nakumbuka akaniambia anataka kunisaidia, nikaenda kuongea na mzee nimepata menejimenti inataka kunisaidia, mzee akaomba kumfaham kama familia, baada ya kila kitu kukaa sawa ndiyo nikaenda Marekani na Afrika Kusini kujifunza ngumi."
Ulikutana na mpinzani wa aina gani katika pambano mwezi uliopita?
"Kwanza alikuwa ni mpinzani mvumilivu kwa sababu tangu raundi ya kwanza alikuwa akipokea vigongo kwa maana ya ngumi kali lakini aliamua kuvumilia, lakini hadi ilipofika raundi ya 10 mwenyewe akapiga goti kuashiria amekubali kama mambo magumu.
"Lakini binafsi nimpongeze mpinzani wangu kwa kuweza kufika hadi raundi ya kumi maana kuna wenzake hawakuweza kabisa kufika hadi huko wamekuwa wakiishia raundi tano wengine ya tatu kwa sababu wanajua kuna maisha baada ya ngumi."
Unaamini alikuwa mpinzani mgumu?
"Sahihi kabisa kwa sababu ni bondia mwenye mapambano mengi kuliko mimi na mzoefu kutokana na ameshacheza na watu tofauti, ni bondia mwenye uzoefu mkubwa."
Umeshatetea mara ngapi WBC Afrika mpaka sasa?
"Unajua mara ya kwanza nilipigania mkanda huu dhidi ya Sabelo Ngebiyana wa Afrika Kusini lakini hakupatikana mshindi, mkanda ukarejea WBC.
"Nikapigana tena na Enoch Tetteh wa Ghana nikampiga kwa Technical Knockout ya raundi tisa katika pambano la raundi 10 ndiyo nikashinda huu mkanda wa WBC kwa mara ya kwanza, nikautetea dhidi ya Lusizo Manzana wa Afrika Kusini Desemba mwaka jana, nikashinda kwa pointi.
"Hili pambano la juzi kwangu lilikuwa pambano la mwisho kutetea ambayo ni mara ya pili na kwa sasa najipanga kupigania mkanda mpya wa ubingwa wa WBC International ambalo ndiyo nitaweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupigania mkanda huo ndani ya ardhi ya Afrika."
Ipi siri ya kuweka kambi Afrika Kusini maana mara nyingi mmekuwa mkifanya hivyo?
"Unajua menejimenti ya Mafia ina watu, nikisema hivyo nafikiri naeleweka kwa sababu tunapenda kusema wenzetu nje kuna maeneo wametuzidi na ndiyo maana mara kadhaa tumekuwa tukienda kuongeza vitu."
Hapa Tanzania bondia gani unaweza kujifunza kutoka kwake?
"Wapo kama watano, wa kwanza, Fadhili Majiha ambaye katika uzito wangu yeye ni namba moja, mimi namba mbili, nina vingi vya kujifunza kutoka kwake kwa sababu ukiangalia uzito wetu ni sawa kimo pia hatujaachana hivyo pale ndiyo nina vitu vingi vya kujifunza.
"Bondia mwengine ni Salim Mtango 'Messi wa Ngumi' bondia ambaye mjanja sana anapokuwa kwenye ringi, halafu mwengine ni Ibrahim Class napenda uchezaji wake anavyocheza ni mtu ambaye anatumia sana jab."
Sijasikia ukimtaja Hassan Mwakinyo, Mfaume Mfaume wala Twaha Kiduku ambao ndiyo mabondia maarufu na wakubwa huko mitandaoni?
"Sikuwataja kwa sababu kila mtu anauchezaji wake, mimi kilo zangu siwezi kupigana kama Twaha Kiduku anavyopigana, uzito ni tofauti kabisa kwa sababu nikisema nicheze kama Twaha Kiduku mashabiki watasema nachezaje kama Twaha Kiduku ambaye ni uzito mkubwa.
"Uchezaji wa uzito mkubwa na mdogo ni tofauti, mimi natakiwa nicheze nichangamke sana kwenye uzito wangu ambao ni mdogo, unamuona Fadhili Majiha anavyocheza anakuwa amechangamka na ndiyo napaswa kucheza vile."
Katika mabondia wa ndani bila ya kuangalia uzito unajiweka namba ngapi?
"Najiweka namba tatu, nimejiweka namba tatu kama orodha ya viwango vya mabondia wa Tanzania inavyoonesha, ukiingia kwenye orodha unaona namba moja ni Fadhili Majiha, anapaswa kuwa namba moja, yeye ana nyota nne mimi nina tatu na nusu.
"Siwezi kusema mimi namba moja wakati uliangalia namba mbili kuna Salmin Kasim lakini nipo katika kupambana ili niwe namba moja."
Pambano gani kali ambalo huwezi kulisahau?
"Pambano la kwanza naweza kusema lile na yule bondia wa Afrika Kusini, Lusinzo Manzana, pambano ambalo lilinipa changamoto kwa sababu raundi ya kwanza nilipasuka juu ya jicho baada ya kunipiga kichwa.
"Sasa damu zikawa zinatiririkia kwenye jicho, nikawa napigana halafu nifute damu hata mama yangu ambaye alikuwa akiangalia alikuwa na hali mbaya sana kwa sababu alikimbizwa hospitali baada ya kuona mtoto wake nimepasuka juu ya jicho na damu inavuja, nashukuru nilishinda kwa pointi."