Unapowaza vita ya Miquissone vs Pitso Mosimane

Unapowaza vita ya Miquissone vs Pitso Mosimane

IONDOE Soura ya Algeria halafu iweke Al Marreikh ya Sudan jibu lake unapata kundi lilelile ambalo Simba walipewa miezi 36 iliyopita wakati walipofuzu katika hatua ya makundi kama hii waliyotinga hivi majuzi.

Na sasa wamepewa tena Al Ahly, halafu AS Vita ya Congo. Al Marreikh ndiye mgeni mpya katika kundi hili la A. Tayari mashabiki wa Simba wameanza kupiga kelele kuhusu uwezekano wa timu yao kusonga mbele. Wengi wana imani. Kisa? Waliwahi kuzifunga Al Ahly na AS Vita hapa nchini.

Vita walichapwa 2-1. Al Ahly walichapwa 1-0. Hata hivyo kufikiria kwamba Simba inaweza kusonga mbele kwa kutumia matokeo yaliyopita sio sahihi. Hizi ni mechi nyingine mpya ambazo Simba wanapaswa kuzikabili upya na katika tabia tofauti. Ukiamini kwamba Simba watazifunga Al Ahly na Vita pale Temeke ni sawa na kufikiria kwamba Simba itafungwa tena mabao matano kila mechi katika mechi ambazo zitachezwa Kinshasa na pale Cairo. Sio kweli.

Ndani ya miezi 36 maisha yamekwenda kasi. Tayari Al Ahly amechukua ubingwa wa Afrika. Wameimarisha kikosi chao kwa kumchukua kocha mchawi wa Afrika, Pitso Mosimane. Mchezaji wa karibu zaidi waliyemchukua ni Walter Bwalya. Mshambuliaji aliyewahi kuifunga Simba pale Temeke akiwa na Nkana Red Devils.

Pitso atakubali kufungwa Dar es salaam akiwa bingwa wa Afrika? Haiingii kichwani moja kwa moja. Mabingwa wa Afrika watakubali kufungwa Dar es salaam kwa mara nyingine? Hili ni swali la kutafakari kabla ya kujipa imani.

Halafu hawa Vita kuna mastaa wameachana nao. Kina Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Jean Makusu, Fabrice Ngoma na wengineo. Unajua ni kina nani wamechukua nafasi zao? Wana ubora gani? Ni ngumu kujua kwa sababu hatutazami ligi ya DR Congo. Hata hivyo inatosha kusoma alama za nyakati kwa kugundua kwamba AS Vita na TP Mazembe wanaongoza Ligi Kuu wakiwa wamefungana pointi pale DR Congo. TP Mazembe wapo juu kwa tofauti ya mabao. Ndani ya miezi 36 maisha yamebadilika katika timu hizi. Sio lazima matokeo ya Dar es Salaam yarudiwe. Hata wakati Simba akizifunga timu hizi bado hakuwa bora uwanjani kuliko wapinzani. Kuna uhakika gani wa matokeo ya Dar es salaam kujirudia?

Lakini kwanini tunaisahau Al Marreikh? Wameitoa Enyimba ya Nigeria. Huo ni ushahidi wa pili wa mazingira kwamba wapo vizuri. Lakini kitu kikubwa ni kwamba Wasudan wanajua mpira. Wale wa upande wa Juba kule Sudan Kusini sio mafundi, lakini hawa wa hii Sudan halisi huwa wanajua mpira. Hawa si ndio kina Shiboub?

Lakini kwanini naegemea zaidi kutazama ugumu unaoikabili Simba? Siitendei haki. Miezi 36 nayo imeibadilisha pia Simba ingawa kinachonitia wasiwasi ni kwamba mmoja kati ya watu waliosaidia kuibadilisha Simba ameondoka. Sven Vandenbroeck.

Naamini Simba wamebadilika kuanzia pale. Huyu kocha aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco ameifanya Simba itawale zaidi mpira uwanjani. Lakini zaidi ni kwamba kuanzia pale Simba imewaongeza wachezaji watatu ambao wamekuwa muhimu katika timu. Larry ‘soft touch’ Bwalya, Luis Miquissone na Josh Onyango. Wameondoka kina Emmanuel Okwi na wachache wengine.

Wageni wamekuja kufanya vyema zaidi hasa Mmakonde Miquissone. Wataongeza nguvu. Mwishoni mwa michuano hii nabashiri huenda Simba wakapokea ofa nono kutoka mahala kama ataendelea kuonyesha kiwango hikihiki, huku ukikumbuka kwamba umri wake unamruhusu.

Kocha mpya wa Simba hatujui ataichezeshaje timu yake. Wala hatukufahamu huyu kocha aliyepita angeichezeshaje timu yake katika mechi za ugenini. Tuna kumbukumbu mbaya kutoka kwa Patrick Aussems ambaye alikuwa anaichezesha ovyo Simba katika mechi za ugenini.

Ukweli ni kwamba Simba walikuwa hawajihami vyema wakiwa ugenini katika mechi zao za mwisho za makundi. Haikushangaza walipopokea vipigo vikubwa kutoka kwa AS Vita na Al Ahly. Nadhani Simba watamwambia kocha wao mpya matokeo haya.

Kitakachofuata nadhani Simba wataweka azimio la walau kutoka sare katika moja ya mechi zao za ugenini. Watailenga zaidi Al Marreikh lakini sio kazi rahisi kucheza na Al Marreikh wakiwa kwao kutokana na sapoti kubwa wanayoipata kutoka kwa mashabiki. Hata hivyo wakipambana inawezekana.

Simba lazima wasake sare moja au mbili ugenini na kisha kujaribu kushinda mechi zote za nyumbani. Haiwi kazi rahisi lakini katika maisha ya makundi haya ni lazima ufanye kazi chafu ili usonge mbele. Hakuna timu nyepesi. Sio katika kundi la Simba tu, hata katika makundi mengine.

Baada ya hili la ndani ya uwanja kuna jingine ambalo linanipa moyo. Simba wana imani. Wana imani kwamba Dar es salaam hatoki mtu. Wana imani na uwanja wao wa nyumbani. Imani njema huzaa mambo mema. Imani humfanya mwanadamu atembee juu ya maji. Simba wana imani ambayo wameiingiza kwa wachezaji na mashabiki. Hiki ndicho kilichowatokea Platinum wakati Simba walipotangaza vita dhidi yao wiki iliyopita. Walishinda mechi kwa ushindi mnono kwa sababu hii. Hata walipofungwa mechi ya kwanza walikuwa na imani kwamba watapita na kweli wakapita.

Hata hivyo imani yao kwa sasa ipo katika wakati mgumu kuliko wakati wowote ule. Unawaza jinsi ambavyo maisha yameendelea kuanzia pale waliposhika nafasi ya tatu katika kundi lao mara ya mwisho. Wakati wao wana mtu kama Mmakonde aliyekuja kuongeza kasi, Al Ahly wana mtu kama Pitso Mosimane ambaye anajulikana kwa ubora wake katika soka la Afrika kiasi kwamba Waarabu wamelazimika kulipa mabilioni kupata huduma zake wakimtoa kwa tajiri wa Mamelodi Sundowns, Patrice Motsepe.

Usisahau kwamba Pitso amewahi kumfundisha Miquissone pale Mamelodi kabla ya kumuona mchezaji wa kawaida na kumruhusu arudi UD Songo. Wote wameimarika kuanzia pale. Miquissone amekuwa mchezaji bora zaidi huku Pitso akiwa kocha tishio zaidi.