UKWELI NDIVYO ULIVYO: Yanga wakiamua wanaweza

MAMBO yanaenda kasi sana. Jambo lililokuwa juzi jana, leo limebadilika kiasi cha kushangaza.

Utabisha nini? Nani aliyekuwa anajua kama Chelsea ingebeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya?

Ndio, Chelsea ilianza vibaya Ligi Kuu ya England chini ya Kocha Frank Lampard. Mwenendo wao mwanzoni mwa msimu haukutofautiana sana na ule wa Arsenal ama Man United.

Achana na Chelsea. Pale Ufaransa, PSG ambao ni kama walijimilikisha taji la Ligi Kuu nchini humo (Ligue 1), ilijikuta ikitoka kapa, licha ya kuwa na mastaa kibao wanaotamba duniani.

Pia we fikiria tu, namna Luis Suarez alichofanya Atletico Madrid. Alionekana sio lolote si chochote mbele ya Ronald Koeman.

Aliambiwa dhahiri haitajiki Barcelona.

Hata kama inawezekana ishu ya kubana matumizi kutokana na msala wa janga la corona, lakini kwa hadhi yake, hakupaswa kuachwa kihuni vile.

Lakini kwa vile dunia inaenda kwa kasi na mambo hubadilika, Suarez ameibuka shujaa wa Colchoneros.

Hata lile chozi lililomtoka walipokabidhiwa ndoo ya La Liga, lilikuwa na maana kubwa kwake. Ni ngumu kumwona mwanaume akimwaga chozi. Lakini alikuwa akilia kwa mengi. Sijui Koeman anajisikiaje kwa sasa kuona mtu aliyemdharau akigeuka shujaa wa waadui yao. Kidume kimemaliza msimu na mabao 21 katika mechi 32 tu za La Liga. Lakini kufunga bao lililoipa Atletico ubingwa wao baada ya misimu saba walisota katika La Liga.

Tukirudi hata hapa nchini, ni nani aliyewahi kuwaza mtu kama Lengai Ole Sabaya naye angekuwa msambweni! Yaani majuzi alikuwa DC wa Wilaya ya Hai, lakini ghafla leo ni mahabusu!

Dunia kweli inaenda kwa kasi na kasi yake huleta mabadiliko makubwa ndani ya jamii!

Tuacheni na ishu hizo za siasa, ni hivi majuzi tu wanachama wa Yanga waliaminishwa, msimu huu lazima chama lao libebe ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Kigogo mmoja alijibebesha msala, akidai kama timu yao isingebeba ndoo hiyo, aulizwe yeye!

Jeuri hiyo ilitokana na aina ya usajili uliofanywa Jangwani. Wanayanga walijiaminisha ni kweli wanaweza kubeba ndoo, waliyoimisi kwa misimu mitatu kwa aina ya wachezaji waliosajiliwa.

Pia kwa jinsi walivyopambwa. Kuanzia kwenye vyombo vya habari hadi kwa viongozi na wanachama, nyota hao wapya walipewa sifa za kipekee.

Hata hivyo, kwa kuwa dunia inaenda kwa kasi isivyo kawaida. Kila kitu kimebadilika! Upepo umewabadilikia na sasa, wanasubiri kulishuhudia kwa msimu wa nne mfululizo taji hilo likisalia Msimbazi.

Watani wao wana nafasi kubwa ya kulitetea tena. Viporo viwili ilivyonavyo mkononi sambamba na idadi ya mechi ilizonazo na hata ubora wa kikosi chao kwa sasa ni ngumu Simba waiubebe ubingwa huo.

Labda itokee miujiza ya pekee. Carlinhos aliyepokelewa kama mfalme juzi kati alionekana akiondoka kinyonge Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere kurudi kwao Angola.

Tayari kuna tetesi mastaa wengine waliosajiliwa msimu huu nao watafutika Jangwani. Unabisha nini ilihali juzi kati Injinia Hersi Said, kaweka wazi wamejipanga kufanya usajili mwingine wa kishindo. Misimu zaidi ya mitano iliyopita.

Hali inayoikuta Yanga, iliwatesa Msimbazi. Walipotishwa mswaki kwa misimu mitano mfululizo bila ya taji. Ndio, ilikuwa imekabidhiwa kwa kishindo taji lake la 2011-2012 kwa kuinyoosha Yanga mabao 5-0.

Baada ya hapo ubingwa ukawa ni wa Yanga na Azam, kabla ya kujikimboa msimu wa 2017-2018 wakati Yanga ikiwa haina Bilionea Yusuf Manji.

Misimu mitatu wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa kishindo, huku Jangwani wakitaabika huku wakiwa na hali mbaya kama ilivyokuwa enzi za watani wao walipowatania Wa Mchangani.

Hapo ndipo unapoweza kuamini dunia inaenda kwa kasi na kila kitu kinabadilika. Yanga iliyotesa na kuwaimba wenzao wa Simba kuwa wa Wahapahapa...Wamchangani, leo ndio waliobadilishiwa kibao. Wanaitwa Utopolo.

Hili jina hakuna wanayanga anayelifurahia. Ni kama tu walivyokuwa wakichukia Wanasimba walipoitwa wa Mchangani!

Kuna kila dalili kwamba huenda ule mzimu ulioisumbua Simba misimu mitano iliyopita kabla ya kujikomboa, utaisumbua pia Yanga. Simba ilikuwa inasajili na kuacha kila msimu. Hiyo ikawapa kazi rahisi Yanga na Azam kuwaburuza. Safari hii kibado kimehamia kwa Yanga. Kwa misimu minne sasa wanasajili na kuacha.

Inabadilisha makocha kila inapojisikia. Ni kama tu ilivyokuwa Simba enzi zile ikiongelea kwenye maisha inayoogelea Yanga kwa sasa.

Ukweli ulivyo ni kwamba kama Yanga haitazinduka na kubadilika, ijue mapema itaumia. Simba ilishtuka baada ya mateso ya muda mrefu.

Iliamua kuachana na mtindo wa sajili...acha...sajili tena acha! Kikosi kikajengwa na kuwapa nafasi wachezaji wakae pamoja. Leo wanakula shushu!

Hata Yanga inaweza kujikomboa hivyo. Kwa kuwa dunia inaenda kwa kasi na mambo kubadilika, nao ni lazima wabadilike. Wanayanga wawe na moyo wa uvumilivu kwa timu yao, kama alivyosema Hersi.

Yanga inahitajika kujengwa. Pia ipewe muda wa kukomaa na kurejesha makali yao kama zamani. Wanachama na mashabiki wao wasiwe na mihemko ya kutarajia makubwa ndani ya muda mfupi.

Pia, viongozi nao waache kuwapa matumaini makubwa kama walivyowaanimisha mwanzoni mwa msimu huu kuwa, wangerejesha ndoo, wakati wakijua ilikuwa ndoto za alinacha.

Wasiwape presha kubwa wachezaji wanaosajiliwa na kuaminishwa ni wakombozi wanaotegemewa kuikomboa timu yao.

Hii ndio iliyofanya kina David Molinga kuondoka akiwa hajaifanyia Yanga mambo makubwa.

Hii ndio itakayowaondoa kina Abdulrazack Fiston na Michael Sarpong kwa sababu ya kuishi chini shinikizo na presha kubwa ya kufanya makubwa ndani ya muda mfupi.

Kadhalika waache kuiangalia timu yao kwa sasa na kuipima na mafanikio ya Simba. Hata Simba walijichanganya sana kipindi kile, kwani nao wakiiangalia timu yao na mafanikio makubwa ya Yanga ile ya Yusuf Manji na kujikuta wakitafuatana uchawi kila mara kabla ya kujishtukia na kubadilika.

Yanga wanaweza kurejesha heshima yao, kama tu wataamua wenyewe kubadilika kifikra, kwamba hata Roma haikujengwa kwa siku moja. Wakubali kuvumilia mateso kwa muda mfupi waje kuneemeka kwa muda mrefu.

Ni lazima wabadilike kuanzia sasa kama kweli wanataka kurejesha heshima yao vinginevyo wajiandae kuteseka zaidi kwa muda mrefu kama walivyoteseka watani wao misimu kadhaa nyuma.

Watoto wa mjini wanasema kama mambo hayaendi, nenda wewe. Yanga kazi kwenu!


IMEANDIKWA NA BADRU KIMWAGA