Ukiniuliza mimi, Stars bora ilikuwa ya Poulsen

KWANZA nieleze kuhusu kichwa cha habari. Nazungumzia kipindi cha miaka 10 tu iliyopita.

Nimetazama mechi nyingi za Taifa Stars katika miaka 10 iliyopita; moja kwa moja uwanjani au kwa njia ya televisheni na niseme kwamba nilivutiwa sana na kikosi kilichokuwa kinafundishwa na Kim Poulsen.

Mbwana Samatta alikuwa wa moto sana mara nyingi akishambulia kutokea pembeni kushoto. Thomas Ulimwengu alikuwa akishambulia kutokea upande wa kulia. Wote walikuwa wachezaji wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Frank Domayo na Himidi Mao walikuwa miamba katikati ya uwanja huku Kelvin Yondani na Nadir Haroub wakiwa mbele ya Juma Kaseja. Kwanini niliipenda timu ile?

Niliipenda kwa sababu ya kasi yake na ulikuwa ukijua kabisa inacheza vipi. Uzuri ni kwamba ilikuwa inaundwa na vijana ambao Kim alikuwa anawafahamu tangu wakiwa wanaibuka kwenye mashindano mbalimbali likiwamo Kombe la Uhai.

Kikosi cha Stars kilichokuwa chini ya Marcio Maximo hakikuwa kibaya lakini mara zote nilimwona kama Mwalimu aliyeamini kwenye kujilinda zaidi na hakuwa akivutiwa na wachezaji walioonekana kuwa na vipaji zaidi kwenye timu.

Labda ni bahati mbaya lakini mimi nimekua nikishabikia timu mbili kubwa za soka; Simba kwa hapa nyumbani na Liverpool nchini England. Hawa wote hawajui mchezo wa kukaba. Kinachotakiwa ni kucheza kwa kuwapa burudani washabiki. Nakumbuka mechi moja kati ya Stars dhidi ya Ivory Coast iliyokuwa na nyota kama Yaya Toure, Didier Drogba, Koffi Ndri Romerick, Didier Zokora, Arthur Boka na Kolo Toure lakini waliondoka na viatu uwanjani dhidi ya Stars ya akina Domayo.

Kama mechi ile ingekuwa dhidi ya Stars ya Maximo, bila shaka Mbrazili yule ‘angepaki basi’ mpaka mwisho wa mchezo lakini Kim hakuwa hivyo. Jeuri ya kocha yule raia wa Denmark haikuwa nyumbani tu bali hata ugenini – kama ilivyokuwa dhidi ya Morocco ambapo Stars ilicheza kwa kiwango cha juu.

Nimesikia fununu kwamba Kim Poulsen anarejea kufundisha nchini ingawa haijaelezwa kinaga ubaga anakuja kuwa Kocha wa Stars au Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)? Kwa maoni yangu, huyu anafaa kuwa kocha na si mtu wa ofisini.

Kim ameshakaa Tanzania na anawajua vizuri watu wa mpira. Pasi na shaka yoyote, anajua kuwa nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF ni nafasi kubwa lakini ina ushawishi mdogo kwenye mpira wetu.

Ushawishi mkubwa uko kwenye kusimamia timu ya taifa. Kila Mtanzania ameweka akili yake kwenye timu yake na kama kuna jambo ambalo TFF inaweza kulifanya na faida au hasara yake kuonekana mapema ni kwenye kufanya uteuzi wa mwalimu wa Stars.

Kwa mwaka, Stars haina mashindano mengi sana. Mwalimu yeyote anayekuja Tanzania anaweza kabisa kupangiwa muda wa kutekeleza majukumu yake kama Kocha Mkuu wa Stars na pia kama kinara wa programu za mafunzo kwa wanamichezo wadogo.

Ni rahisi kwa Kim kuelewana na wachezaji wetu kwa sababu wengine bado wanamfahamu na kumheshimu. Ninaamini kuwa yeye si maamuma kabisa katika lugha ya Kiswahili. Hili ni jambo jema kwa wachezaji wetu – hasa wale ambao Kiingereza bado hawajakimanya vizuri.

Sidhani kama Watanzania wana imani tena na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, hasa baada ya kuondoshwa mapema kwa Stars kwenye mashindano ya (CHAN) yanayoendelea nchini Cameroon.

Sidhani pia kama TFF inaweza kumpata mwalimu wa gharama nafuu, anayeijua Tanzania na watu wake na wakati huohuo akawa na kiwango cha utaalamu alionao Poulsen. Ni wazi kwamba hii ni nafasi ambayo iko tayari kuchukuliwa na Kim. Jambo pekee ambalo najiuliza kuhusu TFF ni kuhusu mwelekeo wetu kama nchi kisoka. Ukimtazama Maximo, Salum Mayanga, Emmanuel Amunike na Etienne Ndayiragije, unapata mchanyato wa aina tofauti kabisa za walimu.

Umefika wakati sasa wa kumtaka Kim ashirikiane na wataalamu wetu kututengenezea mfumo imara unaoweza kuitwa mfumo wa Kitanzania. Hilo litegemee na malezi ya wachezaji wetu, vipaji vyao, udhaifu wao na mfumo wa kucheza.

Mambo ya Watanzania kufundishwa ‘Dutch Football’ hayana maana sasa katika dunia sasa. Pengine ingekuwa Maneromango Style – labda watoto wengi wangejitumbukiza kwenye mchezo huo.

Karibu sana Kim.


Imeandikwa na Ezekeil Kamwaga