Ukimuona refa kachomolea jezi uwanjani nishtue!
Muktasari:
- Hata hivyo, mara mechi inapoanza utaona mmoja baada ya mwingine akichomoa jezi hizo tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa mechi husika.
KAMA wewe ni shabiki na mpenzi wa soka, naamini mara kibao umeshaona wachezaji wakiingia uwanjani wakiwa wamechomekea jezi zao. Huwa hivyo pale wanapokaguliwa na kabla ya kuanza kwa mechi wakionekana kuwa smati.
Hata hivyo, mara mechi inapoanza utaona mmoja baada ya mwingine akichomoa jezi hizo tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa mechi husika.
Hata wale wanaoingia kutokea benchi. Pale wanapokaguliwa na mwamuzi wa akiba huonekana wamechomokea jezi zao, lakini akiingia uwanjani kuanza kucheza huchomoa jezi hizo na kuendelea na yao.
Sio kama hakuna wachezaji wanaochomekea jezi mwanzo mwisho. Wapo na mmoja ya wachezaji hao ni winga wa Yanga, Maxi Nzengeli. Huyu mwamba buana ni nadra kumuona akichomolea jezi yake hata itokee kitu gani. Yaani yeye kwa dakika 90 huwa amechomokea na kuwa smati na hata ikitokea amechomoa ili kushangilia bao kwa staili ya kufikisha ujumbe. Punde baada ya shangilio hilo, huchomekea tena na kuendelea kuwa yule yule Maxi Nzengeli.
Yupo pia Boniface Maganga. Naye anasifika kwa kuchomekea jezi mwanzo mwisho.
Hakuna anayejua sababu ya wachezaji kupenda kuchomolea wawapo uwanjani, japo hawabanwi na sheria au kanuni ya kuchomokea muda wote, isipokuwa ni ule utaratibu wa kuwa smati uwanjani. Lakini ni nadra sana kumkuta mwamuzi iwe anayesimama kati kupuliza kipenga au wale wasaidizi wanaoshika vibendera au kukaa mezani kama waamuzi wa akiba, wakiwa wamechomolea jezi zao.
Je, umeshawahi kujiuliza kwa nini waamuzi wanachomekea mwanzo mwisho uwanjani hadi pale pambano linalopomalizika.
Kama wewe umeshawahi kuona mwamuzi amechomolea jezi yake akiwa uwanjani anachezesha pambano, tafadhali we nishtue tu!
Hapa chini ni sababu za waamuzi wanaochezea mechi za soka kuwachomokea mwanzo mwisho hata itokee dharura ya aina gani kama Mwanaspoti lilivyozungumza na baadhi yao na kufafanua bila kujali wanachezea mechi za Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship au michuano gani...!
WALA SIO SHERIA!
Mwanaspoti limegundua kwamba licha ya kwamba waamuzi wanachomokea mwanzo mwisho na kuonekana kama niu muhimu sanba kwao, lakini kumbe wala hilo, halipo kisheria wala kanuni.
Ila ni kwamba hata ikitokea kwa bahati mbaya refa akiwa katika majukumu yake uwanjani jezi ikachomoka, basi wenzake watamjulisha hilo ili kujiweka sawa.
Katika mahojiano baina ya Mwanaspoti na baadhi ya waamuzi hao, wanafichua kitu kikubwa wanachokizingatia ni kusimamia maadili ya kazi yao hata kama halipo kisheria ama kikanuni moja kwa moja ila imekuwa kama ni lazima.
WASIKIE WENYEWE
Mwamuzi mstaafu, Mathew Akrama ambaye kwa sasa ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT Lumala lilipo mkoani Mwanza, anasema halipo kisheria wala kikanuni, wanachokizingatia ni kuwa mfano wa usimamizi wa sheria za mpira wa miguu uwanjani.
"Inampasa mwamuzi kuwa kioo wa kusimamia sheria, inampasa kuwa mfano wa unadhifu mbele ya wachezaji, ikitokea akiwa rafu basi atafungua milango kwa wachezaji kufanya vitu vya hivyo, mfano mwamuzi akiwa rafu hata wachezaji hawawezi kumheshimu," anasema Akrama.
JONESIA RUKYAA
Mwamuzi wa kike mwenye beji ya FIFA, Jonesia Rukyaa anasema sababu ya kuchomekea muda wote wanaokuwepo uwanjani ni kuzingatia maadili ya kazi yao.
"Mwamuzi akiwa uwanjani naweza nikamfananisha na baba mwenye nyumba anapokosa nidhamu basi mke na watoto hawawezi wakawa na maadili mema, hivyo mwamuzi anapokuwa rafu mchezaji hawezi kuwa nadhifu," anasema Jonesia na kuongeza;
"Mfano tulikuwa tunaona Uarabuni mwamuzi wa kike anafunga ushungi, lakini lazima uendane na jezi ili kuwa smati, hilo naliona kwa Tanzania kwa sasa, kujibu swali lako lipo katika maadili ya kazi na sio sheria ama kanuni na ikitokea jezi ikachomoka wa pembeni yako atakusaidia kwa kukuonyesha kwa ishara.
"Wachezaji wengi hawachomekei ila na wao ingefaa wachomekee, changamoto kuna muda wanaanguka chini, hivyo akili zao haziwezi muda wote kufikiria jezi, wapo kwa ajili ya kuzipambania timu zao, ila na wao kama kuna vitu hawajavizingatia wanatolewa nje ya uwanja wajiweke sawa."
ABDALLAH KAMBUZI
Mwamuzi wa zamani, Abdallah Kambuzi anasema wanapokuwa uwanjani lazima wawe mfano wa kila kitu kuanzia katika mavazi,lugha ili kuepuka vurugu zinazoweza zikatokea wakati wa mechi.
"Kipindi nilichokuwa nachezesha, nilikuwa navaa kaptura yenye kamba nilikuwa nafunga kabisa kuhakikisha jezi haichomoki, pia refa haifai kukunja soksi, tunafanya hivyo kuwa kioo cha unadhifu kwa wachezaji hata ikitokea bahati mbaya lazima wenzako watakusaidia,"anasema na kuongeza;
"Wachezaji ni vijana na umaarufu una mambo mengi, vipi mwamuzi akiwa rafu mchezaji ataiga kitu gani na ndiyo maana wachezaji smati wanachomekea muda wote pia hilo linawasaidia kuonekana watu wanaojitambua katika jamii, mfano wapo wanaopata dili za nguo kutokana na muonekano wao."
NASSOR SAID
Mwamuzi na Mwenyekiti wa zamani wa waamuzi, Nassor Said anasema: "Katika maelekezo ya kisheria inasisitiza kutumia busara, ndio maana waamuzi wanakuwa nadhifu, lakini halipo kisheria wala kikanuni."
Anaongeza; "Zamani wakati nachezesha hatukuwa tunachomekea kwa sababu nidhamu ilikuwa ya hali ya juu, ila hiki ni kizazi kingine na ni jambo la busara, ingawa neno busara huwa mara nyingi nawashauri waamuzi wasilichanganye na hisia, kwani wawapo ndani ya uwanja wao ni king of the ground."
UKWELI ULIVYO
Kwa mujibu wa mpira wa miguu, kuchomekea jezi kuna maana kadhaa, lakini si sheria ngumu kwa kila mtu.
1. Kwa nini wachezaji wanachomekea jezi?
Nidhamu na muonekano mzuri: Kuonekana nadhifu na mchezaji yuko tayari.
Kuepuka kushikwa jezi: Jezi ikiwa imechomekwa ni ngumu kwa mpinzani kuivuta.
Desturi/tamaduni za timu: Baadhi ya timu au makocha hupenda wachezaji wao wawe wamechomekea kama ishara ya umakini.
Wachezaji wa nafasi fulani (mf. mabeki au viungo wa zamani) wamezoea hivyo tangu mwanzo wa taaluma zao.
2. Je, ni sheria au kanuni?
Kwa wachezaji:
Sio sheria rasmi ya FIFA kwamba mchezaji lazima achomekee jezi muda wote wa mechi.
Lakini:
Mwanzoni mwa mechi au baada ya mchezaji kuingia uwanjani, mwamuzi anaweza kumtaka mchezaji arekebishe jezi yake ili ionekane nadhifu.
Ikiwa jezi iko juu sana au imevaa vibaya, mwamuzi ana haki ya kuzuia mchezo kidogo.
3. Vipi kuhusu waamuzi?
Waamuzi hawalazimiki kuchomekea jezi muda wote kama wachezaji kwa sababu:
Jezi zao zimetengenezwa kipekee (mara nyingi ni fupi au zinakaa vizuri bila kuchomekwa).
Wanakimbia sana, wanainama, wanageuka — jezi ikichomekwa inaweza kuwa isiyofaa au isiyotoa uhuru wa mwendo.
Kanuni za mavazi ya waamuzi zinasisitiza zaidi utofautishaji wa rangi, uwazi na urahisi wa utendaji, si kuchomeka jezi.
4. Kanuni za FIFA kuhusu mavazi ya wachezaji
Kwa mujibu wa Sheria ya 4 ya FIFA (Equipment of Players):
Mchezaji anatakiwa kuvaa:
Jezi
Bukta
Soksi
Viatu
Kinga za miguu (shin guards)
* Hakuna sehemu inayosema jezi lazima ichomekwe muda wote wa mechi.
Lakini:
Mwamuzi ana haki ya kuhakikisha mchezaji anaonekana nadhifu kabla ya kuanza au baada ya kuingia uwanjani.
Jezi ikiwa imevaa vibaya au inaonyesha maandishi yasiyoruhusiwa, mchezaji anaweza kuzuiwa hadi arekebishe.
5. Kwa nini waamuzi hawachomekei jezi?
Jezi zao hutengenezwa zifit moja kwa moja.
Wanahitaji uhuru mkubwa wa mwendo (kukimbia, kuinama, kugeuka).
Kanuni kwa waamuzi zinalenga:
Rangi tofauti na timu
Urahisi wa kutambuliwa
Utendaji, si mitindo
MASTAA WAKALI WA KUCHOMOKEA
Achana na Maxi Nzengeli au Maganga, huko Ulaya kuna wachezaji maarufu wanaojulikana kwa kuchomekea jezi zao.
Hapa chini ni mifano ya wachezaji ambao karibu kila mara walionekana wamechomekea jezi:
David Beckham, nyota wa zamani wa kimataifa wa England aliyetamba na klabu mbalimbali ikiwamo Manchester United na Real Madrid– nidhamu na mwonekano safi.
Zinedine Zidane, staa wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa mwenye asili ya Algeria aliyetamba na klabu mbalimbali barani Ulaya– mtindo wa kiungwana na umakini mkubwa.
Steven Gerrard, nahodha wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England– ishara ya uongozi na uwajibikaji.
Xavi Hernández– mpira wa nidhamu, akili na utulivu.
Toni Kroos – hadi leo anapendelea muonekano wa kitaalamu.
Sergio Busquets– hasa enzi zake Barcelona na kwa wengi wao, kuchomekea jezi kulikuwa sehemu ya utambulisho wao uwanjani.